Wananchi wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma wamemwua askari mmoja na kumjeruhi mwingine kwa kutumia mawe, baada ya askari hao waliokuwa doria, kumwua kwa kumpiga risasi mwendesha pikipiki (bodaboda).

Askari Polisi, PC Yohana namba 7771 alipoteza uhai katika eneo la Ngwinde kutokana na waendesha pikipiki hao kushikwa na hasira za kuuawa kwa mwenzao aliyetambulika kwa jina la Makisio Ngonyani (27), mkazi wa kijiji hicho, na hivyo kuamua kupiza kisasi.

Akizungumza na kipindi cha Radio One Stereo Nipashe, Kamanda wa Polisi mkoani Ruvuma, Deusdedith Nsimeki amethibitisha kutokea kwa tukio hilo jana majira ya saa 8 mchana na kusema kuwa askari polisi wakiwa katika sare zao, walikuwa wamemfuatilia mwendesha pikipiki aliyekuwa amevunja sheria kwa kubeba abiria wawili na aliposimamishwa alikaidi.


 Baada ya kumkamata ndipo iliyopotokea purukushani ambapo risasi iliyofyatuliwa na askari ilimjeruhi mtu mmoja kidoleni kabla ya kumpata marehemu kwenye paji la uso, na kusababisha kifo chake papo.

Kamanda Nsimeki amesema, baada ya kuona hivyo, wananchi walichukua miti mikavu na mawe na kuanza kumshambulia PC Yohana na kusababisha kifo chake.

Askari aliyejeruhiwa, Konstebo Venance Kamugisha yupo katika hospitali ya Songea Mjini, kwa matibabu ya majeraha aliyoyapata kichwani na kusababisha kupoteza damu (bleeding excessively).

Kamanda Nsimeki amesema jeshi hilo bado linaendelea na uchunguzi ili kupata ripoti kamili.
Chanzo: MPEKUZI
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top