FIFA imesema kumekuwa na shutuma kupitia taarifa mbalimbali za vyombo vya habari nchini kuwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imeonesha nia ya kuingilia uendeshaji wa TFF.
Kwa mujibu wa barua Machi 10 mwaka huu ya FIFA kwenda kwa Rais wa TFF, Leodegar Tenga, vyombo vya habari vimemkariri Waziri (Dk. Fenella Mukangara) kuwa Serikali imeiagiza TFF kutumia Katiba ya mwaka 2006 katika uchaguzi wakati tayari imeshafanyiwa marekebisho.
“Pia imeelezwa kuwa TFF imetakiwa kufanya Mkutano Mkuu pamoja na ule wa uchaguzi kwa tarehe ambazo zimepangwa na Serikali. Vilevile imeelezwa kuwa Serikali inakusudia kuunda Kamati ya Muda iwapo TFF haitatekeleza maagizo yake,” imesema sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome Valke.
FIFA imesema iwapo yaliyoripotiwa na vyombo vya habari yatathibitika kuwa kweli, maana yake huo ni uingiliaji wa wazi wa Serikali kwa shughuli za TFF.
“Tunapenda kuwakumbusha kuwa wanachama wote wa FIFA wanatakiwa kuendesha shughuli zao kwa uhuru bila kuingiliwa na mtu mwingine kama ilivyoelezwa katika ibara za 13 na 17 za Katiba ya FIFA.
“Hivyo kama maagizo hayo yanayodaiwa kutolewa na Serikali yatatekelezwa, suala hili litapelekwa katika mamlaka za juu za FIFA kwa hatua zaidi ikiwemo kuisimamisha Tanzania kama ambavyo inakuwa pale panapokuwa na uingiliaji wa Serikali,” imesema barua hiyo.
Barua hiyo ambayo nakala yake pia imetumwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) imeelezea baadhi ya athari ambazo Tanzania itakumbana nazo endapo itasimamishwa ni timu za taifa pamoja na klabu kutoshiriki mechi za kimataifa kwa mujibu wa Ibara ya 14 ya Katiba ya FIFA.
Vilevile si TFF au wanachama wake na maofisa wengine watakaoweza kunufaika na programu za maendeleo, kozi au mafunzo yanayotolewa na FIFA na CAF.
“Madai ya uamuzi uliofanywa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ni ya kusikitisha kutokana na ukweli kuwa FIFA ilishatangaza itatuma ujumbe wake kuchunguza jinsi hali ilivyo kwa sasa na kutoa mapendekezo yake. Kutokana na hali hii, ujumbe wa FIFA uliokuwa uje kuchunguza (suala la uchaguzi) itabidi usubiri kwa vile ni muhimu kushughulikia tatizo hili kwanza.
“Katika mazingira haya tunaomba ueleze msimamo huu wa FIFA kwa mamlaka zinazohusika (Serikali) na athari ambazo mpira wa miguu wa Tanzania utakumbana nazo. Tunakushuru na tunatarajia utatufahamisha kila hatua inayoendelea katika suala hili,” imesema barua hiyo.
LIGI YA VODACOM KUENDELEA J’MOSI
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea Jumamosi (Machi 16, 2013) kwa mechi tatu zitakazochezwa katika miji ya Mwanza, Dar es Salaam na Manungu, Turiani mkoani Morogoro.
Toto Africans inayopigana kukwepa kurudi daraja la kwanza itakuwa mwenyeji wa Mgambo Shooting kutoka Tanga katika mechi itakayochezwa Uwanja wa CCM Kirumba.
Vinara wa ligi hiyo Yanga wataumana na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Taifa wakati Uwanja wa Manungu utakuwa mwenyeji wa mechi ya Mtibwa Sugar na Coastal Union.
UCHAGUZI TAFCA KUFANYIKA MOROGORO
Uchaguzi wa viongozi wa Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) utafanyika Jumamosi (Machi 16 mwaka huu) mjini Dodoma ambapo wajumbe wanatakiwa kuripoti siku moja kabla ya uchaguzi.
Wagombea waliopitishwa kuwania uongozi na Kamati ya Uchaguzi ya TAFCA chini ya uenyekiti wa Ramadhan Mambosasa ni Oscar Don Koroso (Mwenyekiti), Lister Manyara (Makamu Mwenyekiti) na Katibu (Michael Bundala).
Wengine ni Gabriel Gunda (Katibu Msaidizi), Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania- TFF (Wilfred Kidao) wakati wagombea ujumbe wa Kamati ya Utendaji ni Jemedali Saidi, George Komba na Magoma Rugora.
KIM KUTAJA KIKOSI CHA KUIKABILI MOROCCO
Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Kim Poulsen
Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Kim Poulsen anatarajia kesho (Machi 13 mwaka huu) kutaja kikosi chake kitakachoivaa Morocco.Mkutano huo wa Waandishi wa Habari utafanyika saa 5 asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itacheza na Morocco kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Machi 24 mwaka huu.
MECHI YA SIMBA, COASTAL YAINGIZA MIL 37/-
Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Coastal Union iliyochezwa juzi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 36,820,000 kutoka na watazamaji 6,284.
Viingilio katika mechi hiyo namba 138 iliyomalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 8,265,752.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 5,616,610.17.
Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 4,202,924.97, tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi sh. 2,521,754.98, Kamati ya Ligi sh. 2,521,754.98, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 1,260,877.49 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 980,682.49. TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment