UBABE unaolalamikiwa na wabunge wa upinzani dhidi ya Spika wa Bunge, Anne Makinda na Naibu wake, Job Ndugai, umeendelea kupingwa kila kona, huku waziri mwandamizi katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, naye amejitokeza kupinga namna shughuli za Bunge zinavyoendeshwa.
Baadhi ya wabunge waandamizi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamefikia hatua ya kusema kuwa kwa hiki kinachotokea sasa, Makinda na Ndugai wameshusha heshima na hadhi ya Bunge iliyoachwa na Samwel Sitta, aliyejulikana kama Spika wa Kasi na Viwango.
Baadhi ya akina mama wamefikia mahali pa kusema kuwa rekodi mbaya inayowekwa na Makinda bungeni inawaharibia wanawake, hasa wale waliokuwa wanawaza kuwania nafasi za uongozi wa juu, na waliodhani mama huyu angeweza kuwa mfano mwema wa akina mama katika uongozi.
Sambamba na waziri huyo, pia Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba, amedai wabunge wa CHADEMA hawatumwi na Katibu Mkuu wao, Dk. Willibrod Slaa kufanya vurugu bungeni bali wanatetea haki zao.
Kwa upande wao, baadhi ya wabunge wa CCM waliokataa kutajwa, wamewalalamikia Makinda na Ndugai kuwa uendeshaji wao wa shughuli za Bunge, unawapa sifa wapinzani.
Makada hao wa CCM walisema kuwa hoja binafsi mbili zilizowasilishwa na wabunge wa upinzani na kisha kuondolewa katika mazingira ya kutatanisha, zimewapa sifa zaidi wapinzani.
Akizungumza na Tanzania Daima mjini Dodoma, waziri huyo mwandamizi aliyeomba kuhifadhiwa jina lake, alisema kuwa haungi mkono kiti cha spika kuondoa hoja hizo kwa sababu zozote zile.
"Hoja ya Mnyika ilihusu tatizo la maji jijini Dar es Salaam. Ni tatizo kubwa sana na kila mkazi wa jiji hilo anajua. Ukiiondoa kwa sababu za kukiuka kanuni, mwananchi ambaye hajui kanuni hatakuelewa.
"Mwananchi anajua Mnyika katoa hoja nzito kumaliza tatizo la maji, wabunge wa CCM wamekataa. Haya mengine ya kanuni sijui hoja gani ijadiliwe kwanza, mwananchi haelewi," alisema waziri huyo.
Waziri huyo ambaye ni maarufu kutokana na msimamo wake katika nyadhifa mbalimbali alizowahi kushika, alisema kuondolewa kwa hoja ya Mnyika kuhusu tatizo la maji Dar es Salaam, kumewaweka pabaya sana wabunge wa CCM wa mkoa huo.
Alisema ili CCM ibaki salama na ishinde majimbo ya Mkoa wa Dar es Salaam mwaka 2015, lazima serikali ihakikishe inatekeleza ahadi iliyotoa bungeni wakati wa kujibu hoja ya Mnyika, kwamba ifikapo mwaka 2015, tatizo la maji litakuwa historia katika jiji hilo.
Alipendekeza kuwa ili kiti cha spika kiendeshe mijadala ya hoja binafsi zenye kugusa moja kwa moja matatizo ya wananchi, ni bora akakaa na watoa hoja hata zaidi ya mara tatu kujadiliana nao ili inapokuja bungeni isikwamishwe na kanuni.
Alitahadharisha kuwa wapinzani ni wajanja, kwani hoja wanazoibua zinagusa matatizo halisi ya wananchi, na wabunge wa CCM wanapopingana nao, hawawezi kueleweka.
Kauli ya waziri huyo inaelekeana na ile ya Dk. Slaa aliyoitoa juzi, akidai kuwa kiti cha spika chini ya Makinda kimepwaya kwa maamuzi tofauti na ya wakati ule wa Bunge la Tisa chini ya Spika Samuel Sitta.
“Mimi nasema afadhali ya Sitta mara kumi kuliko huyu Makinda. Sitta alikuwa na aibu ya kupindisha sheria, na ilikuwa ukimbana kwenye hoja anakubaliana na hoja yako kwa manufaa ya Watanzania,” alisema Dk. Slaa.
Naye mmoja wa wabunge wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, alisema  kuondolewa kwa hoja ya Mnyika ni kitanzi kwao.
"Kwenye kikao cha ndani, CCM tulishapanga kukwamisha na kuiondoa hoja ya Mnyika. Lakini kama ingefika hatua ya kuchangiwa, ningechangia kwa ukali zaidi kuishambulia serikali itimize ahadi yake,” alisema bila kutaka kutajwa.
Wiki iliyopita, Mbunge wa Ubungo, Mnyika na wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (CHADEMA), waliwasilisha hoja binafsi, lakini ziliondolewa.
Mbunge mwingine wa upinzani aliyeleta hoja binafsi ni James Mbatia (NCCR Mageuzi).
Mbatia aliye mbunge wa kuteuliwa na rais, alileta hoja nzito ya udhaifu wa elimu nchini ambayo ilizua mjadala mkubwa.
Hoja ya Mbatia iliyozua mjadala mkubwa bungeni, ilipingwa na wabunge wote wa CCM na baadaye Naibu Spika, Ndugai aliipitisha kibabe huku wabunge wote wa kambi rasmi ya upinzani wakisusia na kutoka nje.
Hoja ya Mnyika ambayo ilihusu uboreshaji wa huduma ya maji katika Jiji la Dar es Salaam, iliondolewa baada ya Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe kuja na hoja ya kutaka iondolewe kwa madai kuwa tayari serikali imetenga sh trilioni 1.8 kwa ajili ya kuboresha huduma na miundombinu ya maji.
Pia alisema hoja hiyo iondolewe kwa vile inazungumzia tatizo la maji katika Jiji la Dar es Salaam wakati tatizo la maji ni la nchi nzima.
Hata hivyo, Mnyika tayari alishafanyia marekebisho hoja yake kwa kuingiza utekelezaji wa miradi ya maji nchi nzima.
Alipanua wigo wa hoja yake kwa kuingiza masuala muhimu kuhusu Programu ya Maji Safi na Mazingira Vijijini (RWSSP), maarufu kama Mradi wa Vijiji Kumi ambao unatekelezwa katika halmashauri za Dar es salaam na wilaya zote nchini.
Nassari alileta hoja kuhusu matatizo yanayolikabili Baraza la Mitihani nchini (NECTA) na kupendekeza marekebisho yake.
Hata hivyo, hoja hiyo iliondolewa kwa kile Spika Makinda alichosema kuwa kukithiri kwa vitendo vya utovu wa nidhamu kwa wabunge wakati wa kujadili hoja hizo binafsi.

Lipumba anena
Mwenyekiti wa CUF, Prof. Lipumba amesema kuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Slaa hakuwatuma wabunge wake kufanya vurugu bungeni bali wanafanya hivyo kudai haki zao.
Kauli ya Lipumba inakuja huku kukiwa na upotoshaji unaoenezwa kuwa Dk. Slaa ndiye anachochea vurugu hizo kwa wabunge wake.
Badala yake mwanasiasa huyo alifafanua kuwa wabunge hao walikuwa na haki na kujenga hoja katika madai yao ya msingi, hasa kwa kuwakilisha matatizo ya wananchi wao.
Akizungumza jana na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam, katika viwanja vya Mahakama Kuu, Prof. Lipumba alisema kuwa kupindisha hoja binafsi ya Mnyika si haki na maadili ya kiti chao.
Lipumba alisema kuwa kuwapinga wabunge hao na kuziondoa hoja zote binafsi wanazowasilisha kwa ajili ya matatizo ya wananchi si haki, na inaonesha upungufu katika kiti hicho hasa katika kutenda haki.
“Inasikitisha spika na naibu wake hawafuati utaratibu ndiyo maana sisi CUF tumependekeza katika katiba mpya spika asiwe mbunge,” alisema.
Siku mbili zilizopita, Bunge lililazimika kuahirisha vikao kabla ya muda wake kutokana na kutoelewana kwa wabunge wa upinzani, kiti cha spika na serikali kwa upande mwingine, wakati wa kujadili na kupitisha hoja binafsi za wabunge.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba, alisema kuwa inasikitisha Bunge kuwa na hali hiyo wakati hoja binafsi inatakiwa iheshimiwe.
Alisema kuwa kuzuia hoja binafsi ya mbunge si jambo jema na kumtaka Naibu Spika, Ndugai kutumia hekima badala ya msuli.
“Kutumia msuli haifai, na kinachoonekana dhahiri alipania kufifisha hoja ya upinzani. Kiti cha spika kinataka mtu mwenye busara na hekima, yaani imeonekana kuwa kiti hicho kinakwamisha hoja za upinzani,” alisema.
Chanzo: Tanzania Daima
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top