MWANAFUNZI wa kidato cha sita katika shule ya sekondari ya wavulana ya Songea mkoani Ruvuma amekutwa amekufa baada ya kujinyonga kwenye mti uliopo kandokando ya njia kwenye eneo la milima ya matogoro ya hifadhi ya msitu ya taifa nje kidogo ya manispaa ya Songea.

Kaimu kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma mrakibu mwandamizi wa polisi George Chiposi alisema  kuwa tukio hilo lilitokea januari 21 mwaka huu majira ya 12.30 asubuhi huko katika eneo la milima ya matogoro 

Kaimu kamanda Chiposi alimtaja mwanafunzi huyo aliyekutwa amekufa baada ya kujinyonga kuwa ni Ahabu Richard Ng’ondya (21) wa kidato cha sita katika shule ya sekondari ya wavulana ya Songea ambapo alidai kuwa siku hiyo ya tukio watoto wawili ambao walikuwa wakipita njiani majira ya saa za asubuhi ghafla waliona kama kuna mtu ananing’inia kwenye mti mrefu ambao upo kandokando ya njia hiyo.

Watoto hao baada ya kuona hali hiyo walikimbia na kukutana na mtu aliyejulikana kwa jina la Osward Kahongo walimwonyesha tukio hilo ambaye nae pia aliwasiliana na polisi ambao walifika kwenye eneo la tukio wakiwa wameongozana na daktari.

Alisema baada ya polisi kufanya uchunguzi ulibaini kuwa alikuwa ni mwanafunzi wa shule ya sekondari ya wavulana ya Songea ambaye anadaiwa aliondoka kwenye eneo la shule katika mazingira ya kutoroka siku chache kabla ya kutokea tukio hilo.

Alibainisha zaidi kuwa upelelezi wa awali wa polisi umebaini kuwa chanzo cha kujinyonga kwa mwanafunzi huyo ni kwamba alikuwa amefukuzwa shule na uongozi wa shule baada ya kutofanya mitihani ya majaribio hivyo uongozi wa shule ulimtaka arudi nyumbani kwao Matamba Uwanji wilaya ya Makete mkoani Njombe ili akamlete mzazi wake.

Alieleza zaidi kuwa baada ya kuambiwa hivyo mwanafunzi huyo alitoeka kwenye eneo la shule na kwenda kusikojulikana hadi hapo alipokutwa akiwa amekufa kwa kujinyonga, hata hivyo alieleza kuwa mwili wa marehemu umesafirishwa kwenda Matamba Uwanji nyumbani kwa wazazi wake kwa ajili ya mazishi.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top