JAJI Mkuu wa Zanzíbar Omar Othmani Makungu

JAJI Mkuu wa Zanzíbar Omar Othmani Makungu amesema  kuwepo kwa Mahakama ya watoto nchini kutasaidia kupunguza mrundikano wa kesi zinazowakabili watoto mahakamani na kupatikana haki zao kwa wakati.
Jaji Makungu ameyasema hayo alipokuwa akifungua Mahakama ya Watoto Zanzibar huko Vuga ikiwa ni shamra shamra ya siku ya Sheria duniani inayoazimishwa Februari 7 kila mwaka.
Amesema lengo la kufunguliwa Mahakama hiyo ni kukabiliana na changamoto ya ongezeko la kesi zinazohusu Watoto na kuwapatia haki zao za msingi kwa wakati.
Aidha ameongeza kuwa Mahakama hiyo itakuwa ni mazingira rafiki kwa watoto ambayo yatawasaidia kuweza kujieleza pamoja na kutoa ushahidi bila ya hofu.
Jaji Makungu amefahamisha kuwa wanatarajia kuanzisha Mahakama ya Watoto kwa upande wa Pemba sambamba na kuweka mahakama ndogo ndogo katika kila wilaya ili kuweza kuondoa usumbufu kwa wananchi.
Nae katibu Mkuu Wizara ya Ustawi wa Jamii maendeleo ya Wanawake na Watoto Fatma Gharib Bilali amewataka wazee kushirikiana na mahakama hiyo ili kuweza kutatua matatizo mbali mbali yanayowakabili watoto ikiwemo kurekebisha tabia na kukufatilia nyendo zao.
“Maendeleo yeyote lazima yawe na changamoto zake jamii lazima iwasaidie watoto kuwalinda na vishawishi vya watu wabaya” alisema Katibu huyo.
Nao Wawakilishi kutoka Mashirika ya Kimataifa ya UNICEF na Save The Children wameishukuru Mahakama Zanzibar kwa ushirikano wao wa kuweza kuanzisha mahakama ya watoto ambayo itaweza kutetea na kulinda haki za mtoto na ustawi wake.
IMETOLEWA NA  MAELEZO ZANZIBAR  05/02/2013.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top