WADAU WAMTAKA MALINZI AREJESHWE URAIS TFF,KAMPENI NAZO ZASITISHWA .
Baadhi ya wadau wa michezo wamesema kitendo kumuengua JAMAL MALINZI aliyekuwa mgombea URAIS wa TFF kilichofanywa na kamati ya Rufaa ya shirikisho la kandanda Tanzania TFF ni kukandamiza na kurudisha nyuma michezo.
Wadau hao kwa kauli moja wamesema wako tayari kulipeleka suala hilo kwa mahakamani  ili kuhakikisha haki inataendeka.
Ramadhani Mgeni  maarufu dogo macho wa Simba ni miongoni mwa wadau waliopendekeza kuwa jina la Jamal Malinzi linarejeshwa katika orodha ya wagombea ili kupambana na Athumani Nyamlani ambaye amebaki kama mgombea.
Wadau wengine walioongea na vyombo vya habari walikuwa Salum mkemi na na Suleimani Kato wamedai maendeleo ya soka hayawezi kufikiwa kama mizengwe itaendelea katika mchezo huo.
Hata hivyo katibu mkuu wa Shirikisho Angetile Osiah amesema hawezi kuyatolea ufafanuzi malalamiko ya wadau kuwa baadhi ya majina yameondolewa kimizengwe wakati kuna sheria,kanuni na taratibu zilizotumika kuwaengua wagombea husika.
Baadhi ya wagombea ambao rufaa zao zimedunda ni Michael Richard Wambura aliyekuwa anawania nafasi ya makamu rais wa TFF Omari Nkurulo aliyekuwa akigombea nafasi ya Urais TFF.
KAMPENI ZA UCHAGUZI TFF ZASITISHWA KWA MUDA
Katika hatua nyingine kamati ya uchaguzi ya TFF imesitisha kampeni za uchaguzi wa TFF na bodi ya Ligi Tanzania zilizotakiwa kuanza hapo Jumatano Februari 13 mpaka itakapotamkwa vinginevyo.
Ifuatayo ni sehemu ya taarifa hiyo iliyotolewa na kamati ya uchaguzi ya TFF.
1. Kamati ya Uchaguzi, kwa mamlaka iliyonayo kupitia Kanuni za Uchaguzi za TFF Ibara ya 3(1), 6(1) (g) na (l), 10(5), 11(6) inayosomeka pamoja na Ibara ya 14(1) na (2) na pia Ibara ya 26(5) na (6), imesitisha zoezi la kampeni za uchaguzi wa TFF na TPL Board lililokuwa lianze kesho tarehe 13/02/2013 hadi hapo itakapowatangazia, ili kuhakikisha kuwa mchakato wa uchaguzi unakidhi kikamilifu matakwa ya Kanuni za Uchaguzi na Katiba ya TFF.

2. Tarehe za Uchaguzi Mkuu wa TFF na TPL Board zinabaki kama zilivyopangwa.
          
3. Taarifa hii inazingatia pia Ibara ya 2(4) ya Kanuni za Uchaguzi za TFF inayoagiza uongozi uliopo madarakani kuendelea na kutekeleza majukumu ya Shirikisho hadi hapo mchakato wa uchaguzi utakapokamilika.

Deogratias Lyatto
MWENYEKITI
KAMATI YA UCHAGUZI TFF

WATANZANIA WATAKIWA KUWA WAZALENDO KWA TIMU ZAO
Shirikisho la kandanda Tanzania TFF limewataka mashabiki kuwa wazalendo na kujitokeza kushangilia timu za Simba na Azam ambazo mwishoni mwa wiki zitacheza mechi za kimataifa za kimashindano  barani Afrika.
Katibu mkuu wa shirikisho hilo Angetile Osiah amesema kitendo cha mashabiki kuzishangilia timu za nje badala ya kuangalia timu za nyumbani zinawakatisha tama wachezaji uwanjani.
Pia ameongeza kuwa viongozi wa klabu shiriki katika michuano ya kimataifa kuwa na ukarimu kwa timu pinzani kama sheria na kanuni za CAF zinavyoelekeza.
’Nguvu ya washabiki ni muhimu katika kuziweza timu hizo kufanya vizuri katika mechi hizo za nyumbani dhidi ya Al Nasir Juba ya Sudan Kusini na Club Libolo ya Angola.Aliongeza katibu huyo.

Azam itacheza Jumamosi (Februari 16 mwaka huu) dhidi ya Al Nasir katika mechi ya Kombe la Shirikisho wakati Simba itaikabili Club Libolo kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayofanyika Jumapili. Mechi zote zitachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
                
LYON, YANGA KUUMANA UWANJA WA TAIFA
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inamaliza raundi ya 16 kesho (Februari 13 mwaka huu) kwa mechi kati ya wenyeji African Lyon dhidi ya Yanga itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi Martin Saanya kutoka Morogoro inakutanisha timu zenye mazingira tofauti. Wakati Yanga wakiwa ndiyo vinara wa ligi hiyo kwa pointi 33, African Lyon ambayo sasa inanolewa na Salum Bausi inakamata mkia ikiwa na pointi tisa tu.

Nayo Toto Africans itaikaribisha Polisi ya Morogoro kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza katika mechi itakayochezeshwa na mwamuzi Jacob Adongo kutoka Musoma. Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 20,000 utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Mgambo Shooting na Oljoro JKT.

Nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Mecky Maxime ambaye sasa ni kocha wa Mtibwa Sugar ataiongoza timu yake hiyo katika mechi dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Manungu ulioko Turiani, Morogoro. Ni kwenye uwanja huo huo ambapo Mtibwa Sugar katika mechi yao iliyopita walichapwa mabao 4-1 na Azam.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top