Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA, Freeman Mbowe.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo kimeendelea na mchakamchaka wake ulioanzia bungeni wa kutaka hoja zake zisikilizwe baada ya kutupiliwa mbali kimizengwe bungeni.
Wabunge wa upinzani waliowasilisha hoja zao ni pamoja na Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia aliyetaka mfumo wa elimu nchini ufumuliwe au kuboreshwa.

Hata hivyo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alitetea mfumo wa elimu uliopo kabla ya hoja hiyo kuondolewa kabisa.

Hoja nyingine ni kero ya maji jijini Dar es Salaam iliyotolewa na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika ambayo nayo iliondolewa baada ya Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe kueleza kuwa Serikali inaendelea kutatua tatizo la mbunge huyo.

Hali hiyo ilizua vurugu na matokeo yake hoja nyingine binafsi za wabunge, ikiwamo ya Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasari aliyetaka kujadiliwa kwa mwenendo wa Baraza la Mitihani la Taifa na jinsi linavyoathiri mfumo wa elimu nchini, ziliahirishwa kwa muda usiojulikana.

Mbali na kuzitupilia mbali hoja hizo, Bunge hilo lilimalizika likiifuta Kamati ya Bunge ya Mashirika ya umma iliyokuwa ikiongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.


Baada ya wabunge hao kuvutana bungeni, wameamua kufanya maandamano na mkutano wa hadhara jijini Dar es Salaam ili kuwaeleza wananchi kilichotokea Bungeni na kuweka mikakati zaidi.

Mkakati wa kumng’oa Spika
Katika mkutano wa hadhara, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho (Bara), Zitto Kabwe anasema Spika wa Bunge, Anna Makinda ameshindwa kuwajibika na hivyo anapaswa kung’olewa kutokana na kutaka kuirudisha nchi kwenye kipindi cha kashfa ya Akaunti ya Madeni ya Nje ya Benki Kuu (EPA).

Akizungumzia kitendo cha Spika Makinda kuifuta (Poac), Zitto aliyekuwa Mwenyekiti wa kamati hiyo, anasema imefutwa kwa mbinu za CCM kuzima sauti ya wabunge wa upinzani wanaozungumzia maslahi ya wananchi.

Huku akishangiliwa na umati wa wananchi waliohudhuria mkutano huo, Zitto anataja mbinu ya kwanza ya kumng’oa spika kuwa ni kuwasilisha hoja ya kutokuwa na imani naye, ambayo imeshakamilika inasubiri wakati wake.

“Njia ya pili tuandamane hadi pale shule ya msingi Bunge… au tutumie namba zake (za simu) kumpigia na kumtumia ujumbe wa simu za mikononi…” anasema Zitto.


Akizungumzia zaidi kuhusu kamati hiyo, Zitto anataja sababu ya kufutwa kwa kamati hiyo kuwa ni utendaji wa kamati hiyo uliogundua matumizi ya zaidi ya Sh1 trilioni kutoka kwenye mifuko ya pensheni zilizotumika katika kampeni za CCM, na ujenzi wa vyuo vikuu vya Dodoma, Hombolo na Chuo Kikuu cha Arusha Nelson Mandela.

“Spika lazima ajue kwamba mamlaka yapo kwa wananchi na yeye ni msimamizi tu wa vikao vya Baraza la Wananchi liitwalo Bunge. Anna Makinda lazima adhibitiwe, vinginevyo nchi yetu itaumia,” anasema Zitto.

Zitto aligusia pia sakata la Mtwara akisema kamati iliyofutwa ililitaka Shirika la Maendeleo ya Mafuta (TPDC) kuonyesha mkataba wa ujenzi wa bomba la mafuta, wakaahidi kuupeleka ifikapo Aprili mwaka huu.

“Tulipowataka TPDC watuletee mkataba wa ujenzi wa bomba la gesi wakasema uko wizarani. Katibu Mkuu ambaye anapaswa kwenda kujieleza kwenye Kamati ya Nishati na Madini hakwenda kwa kuwa kamati hiyo pia imefutwa. TPDC wakasema watauleta Aprili. Ndiyo hivyo kamati yetu nayo imefutwa.”

Chanzo: Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top