Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt Hussein Mwinyi |
Waziri wa afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hussein Mwinyi ameitaka bodi ya maabara binafsi za afya kuchukua hatua kwa wale wanaokwenda kinyume na sheria ikiwepo kusimamisha huduma na kuwapeleka mahakamani wale watakaokaidi sheria ya kuratibu huduma za maabara binafsi za afya.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo alipokuwa akizindua bodi mpya
ya maabara binafsi za afya .Alisema sheria hiyo iliyopitishwa na Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
kuanza kutumika mwaka 1998 ilikuwa na lengo la kuboresha huduma za maabara pamoja na kufanikisha utoaji wa huduma bora za
afya nchini.
“Uboreshaji wa mabadiliko ya sekta ya afya ni vema
ufanyike sambamba na uboreshaji wa huduma za maabara ikiwemo uzingatiwaji wa
maadili ya utoaji wa huduma za maabara ili kuepuka athari zinazoweza kutokea
kwa mtoa huduma au anayehudumiwa yaani mgonjwa”alisema
Aidha, aliitaka bodi hiyo kuratibu na kukagua
majengo,vifaa,vitendanishi na kuhakikisha usahihi wa majibu ya vipimo ili
kuleta ubora wa matokeo ya uchunguzi wa magonjwa pamoja na kutoa nafasi kwa
wataalamu wa maabara kuanzisha huduma hiyo hapa nchini.
“Kazi ya bodi hii ni ya muhimu sana kwani utoaji wa
huduma ya tiba haukamiliki iwapo hakuna huduma ya uchunguzi wa magonjwa,ikiwemo
maabara,hivyo maabara inapofanya kazi zake kwa usahii,inampa nafasi nzuri
mganga kuwa na usahii wa tatizo la mgonjwa na kutoa dawa inayostahili na
kutuonesha umuhimu wa kuwa na wataalamu wazuri wa maabara”.
Hata hivyo Waziri huyo ameitaka bodi hiyo kupitia na kufanya
maboresho mapya ya sheria, kanuni na miongozo iliyopo ili iandane na mabadiliko
yanayojitokeza na kuweza kusimamia na kusajili maabara zote nchini.
Awali akisoma hotuba
yake Mwenyekiti wa bodi hiyo Dkt. Magraret Mhando alisema bodi yake inatarajia
kuhakikisha kuwa vifaa na vitendanishi vyote vinavyotumika nchini vina ubora
unaokubalika na vimeorodheshwa katika orodha ya vifaa na vitendanishi vya
maabara ya afya pamoja na kusajili na kuandikishwa maabara na maduka yote kwa
mujibu wa sheria.
Bodi mpya ya maabara binafsi za afya inaundwa na wajumbe
wapatao kumi inatarajia kumaliza muda wa utendaji wake kwa miaka mitatu mwaka 2015.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment