Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana nchini kutoka Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel
akisisitiza kwa wajumbe wa mkutano wa tathmini ya mbio za Mwenge mwaka
2012 kuhusu serikali kufuatiliaji maendeleo ya miradi inayozinduliwa
wakati wa mbio za Mwenge mjini Zanzibar.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Ali Nassoro Lufunga akizungumza na viongozi
na waratibu wa mbio za Mwenge kutoka maeneo mbalimbali nchini kuhusu
maandalizi ya mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2013.Mkoa wa Shinyanga
ulikuwa mwenyeji wa kilele cha mbio za Mwenge kwa mwaka 2012.
Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
Serikali
inaandaa utaratibu wa kufuatilia maendeleo ya miradi yote
inayozinduliwa wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru ili kuhakikisha kuwa
miradi hiyo inakua endelevu na kuwanufaisha wananchi.
Kauli
hiyo imetolewa leo mjini Zanzibar na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo
ya Vijana nchini kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
Prof. Elisante Ole Gabriel wakati akitoa tathmini ya mbio za Mwenge wa
Uhuru mwaka 2012 na maendeleo ya miradi iliyozinduliwa wakati wa mbio
hizo kwenye mkutano wa viongozi na waratibu wa mbio za Mwenge kutoka
maeneo mbalimbali nchini.
Amesema
serikali ina wajibu wa kufuatilia kwa karibu miradi yote iliyozinduliwa
na Mwenge wa Uhuru 2012 katika Halmashauri za wilaya, manispaa na Miji
ili kuhakikisha kuwa gharama kubwa iliyotumika wakati wa uanzishaji na
ujenzi wa miradi hiyo inawanufaisha wananchi kutoka kizazi kimoja hadi
kingine ili kutunza hadhi na heshima ya Mwenge wa Uhuru.
Amesema
mbio za Mwenge wa uhuru zimezindua miradi mingi nchini yenye thamani ya
mabilioni ya fedha na kuongeza kuwa si dhamira ya serikali kuona kuwa
mwenge wa uhuru unatumika tu kuzindua miradi ya maendeleo bali
kuhakikisha uendelevu wa miradi hiyo.
“Mbio
za Mwenge wa Uhuru kila mwaka zinazindua miradi mikubwa inayogharimu
fedha nyingi, lazima tufanye tathmini ya miradi yote inayozinduliwa na
hatutapenda kuona mwenge unatumika tu kuzindua miradi kwa maana sherehe,
tutapenda kuwa na taarifa za maandishi juu ya hali ya miradi hiyo ili
itolewe kwenye tathmini ya mbio za mwenge kwa miaka inayofuata”
amesisitiza Prof. Gabriel.
Amesema kuwa utaratibu huo wa ufuatiliaji utawahusisha wakuu
wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa Halmashauri zote ambazo Mwenge wa
Uhuru utazindua miradi katika maeneo yao ili kutoa fursa kwa wananchi
kuendelea kunufaika na miradi hiyo na mbio za Mwenge wa Uhuru.
Aidha
Prof. Gabriel ametoa wito kwa wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini
kuhakikisha kuwa miradi yote inayozinduliwa na Mwenge wa Uhuru inapewa
kipaumbele katika usimamizi na ufuatiliaji.
Kwa
upande wake Bw. Wito Mlemelwa mmoja wa wakimbiza Mwenge wa Uhuru mwaka
2012 akitoa taarifa ya tathmini ya mbio za Mwenge kwa wajumbe wa
mkutano huo kwa niaba ya kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa ametoa wito
kwa watendaji na viongozi wa maeneo mbalimbali kuhakikisha kuwa miradi
yote inayotarajiwa kuzinduliwa na Mwenge wa Uhuru inakamilishwa kwa
ubora na viwango ili kuepuka kukataliwa.
“Natoa
wito kwa watendaji wa maeneo mbalimbali wawe makini wahakikikishe kuwa
miradi yote inayozinduliwa na Mwenge wa uhuru inakidhi ubora na viwango
vilivyowekwa kulingana na gharama halisi ya fedha iliyotumika kwa
sababu Mwenge wa Uhuru hautahusika kuzindua miradi iliyo chini ya
kiwango” amesisitiza Bw. Mlemelwa.
Katika
kipindi cha mwaka 2012 mbio za Mwenge wa Uhuru nchini zilizidua miradi
273 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 158.
0 comments:
Post a Comment