MAKAMU wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania    Dkt Mohammed Gharib Bilal
MAKAMU wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Mohammed Gharib Bilal, amewataka maofisa wa Kamisheni ya  Utalii Zanzibar kuwashirikisha kikamilifu wananchi ili waweze kuendeleza sekta ya utalii nchini na kufaidika nayo.


Hayo ameyasema leo huko Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja wakati wa ufunguzi wa hoteli yenye hadhi ya nyota tano, iitwayo Gold Hotel.


Amesema njia ya kuwashirikisha wananchi    itawafanya waweze kufaidika na matunda ya utalii hasa kupata ajira na kuongeza kipato.


“Mjiulize mnafaidika kwa kiasi gani katika utalii, vipi unachangia uchumi wa Serikali ya Zanzibar na  Tanzania kwa jumla,  lakini  pia ni lazima utalii huu uchangie moja kwa moja kwa wananchi”, alisema.


Alisema njia za kuwafaidisha wananchi ni kuwaajiri na kuwasomesha vijana elimu ya utalii itakayowawezesha kuifanyia kazi katika mchanganyiko wa watalii na wageni kiujumla.


Aidha Dkt. Bilal alifahamisha njia za kulikuza soko la utalii nchini, akisema kuna umuhimu mkubwa kuwasomesha watu wanaowatembeza wageni ili waijue vyema historia ya Zanzibar na mazingira, na kwa hivyo waweze kuwashawishi wageni kubakia nchini kwa muda mrefu.


Njia nyengine, alisema ni pamoja na kuwafundisha namna ya kuwapokea wageni, kuwashawishi kutumia pesa zao na kutoa miongozo ya kuleta sifa katika mazingira ya visiwa vya  Zanzibar na fukwe zake.


Dkt Bilal alisema miongozo hiyo na mengine mingi, ni muhimu sana na endapo itafuatwa, ni wazi kuwa soko la utalii litakua kwa kasi kubwa.


Aidha aliwaeleza viongozi wa Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA), wazingatie na kufikiria kwa makini  kuwavutia wengi wakiwemo wawekezaji wa ndani ili kuijengea sura nzuri Zanzibar kwa kuchangia miji na vijji, na kuwataka katika uwekezaji huo waangalie njia za kutunza  silka na  utamaduni wa Mzanzibari.


Makamu wa Rais alifahamisha kuwa sekta ya utalii inakua kwa kasi kubwa duniani na zaidi ya dola trilioni mbili za Kimarekani zinazopatikana katika nchi nyingi hutokana na mchango wa utalii, ambao pia umeajiri watu milioni 98 duniani kote.


Nae Mkurugenzi Mtendaji wa ZIPA Salum Nassor, alisema mpaka sasa jumla ya miradi 511 imeidhinishwa na mamlaka yake katika sekta mbalimbali, ambapo wawekezaji wageni ni 340 na wenyeji 171.


Amesema sekta ya utalii peke yake ina miradi 328 sawa na asilimia 64.19 ambapo kati ya hiyo, wenyeji wanamiliki miradi 214 na wageni 114.


Mkurugenzi huyo alisema kufunguliwa kwa hoteli hiyo ni ishara ya mafanikio, kwani itaweza kuhamasisha sekta nyengine kama vile  biashara, kilimo na uvuvi ambavyo vitapelekea kukua kwa uchumi wa nchi. Hoteli hiyo mpya yenye vyumba 66 inatarajia kuajiri wafanyakazi 200.

Mbali na idadi hiyo ya vyumba vya wageni vya daraja mbalimbali, hoteli hiyo ina kumbi kadhaa za mikutano, nyumba tatu zinazojitegemea (villa) ambapo kila moja ina nyumba mbili.



 
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top