Taarifa kutoka idara ya ulinzi
ya Marekani Pentagon zinasema kuwa mmoja wa wanzilishi wa kundi la Al
Shabaab Ahmed Godane ameuawa.
Marekani imesema kuwa kuuawa kwa Godane ni hatua
kubwa sana katika harakati dhidi ya wapiganaji hao wamekuwa mwiba
mkali kwa mataifa ya kanda ya Afrika Mashariki na hata kwa serikali ya
Somalia yenyewe.
Katibu wa Pentagon Nchini Rear
Admiral John Kirby ametangaza kuwa Ahmed Godane ameuawa katika
oparesheni iliyofanywa nchini Somalia Jumatatu wiki hii.
Kwa Mujibu wa Admiral Kirby, kuuawa kwa Godane
ni pigo kubwa zaidi kwa kundi hilo la Al shabaab na itasaidia
kukabiliana na ugaidi unaofanywa na kundi hilo eneo la Afrika Mashariki.
Marekani imekuwa ikishirikiana na washirika wake
wakuu kukabili wapiganaji hao wa AL shabaab ambapo katika miaka ya hivi
karibuni wamezidisha mashambulio sio tu nchini Somalia bali hadi nchi
jirani.
Wiki iliyopita Kikosi cha kulinda amani chini ya
mwavuli wa Muungano wa Afrika AMISOM kikishirikiana na majeshi ya
serikali ya Somalia kilianzisha oparesheni kali kuwasaka wapiganaji hao
wa AL shabaab ambapo mwanzoni mwa wiki hii Marekani ikajiunga
katika oparesheni hiyo ambapo walishambulia msafara ambao Ahmed Godane
alishukiwa kuwa ndani.
Walioshuhudia waliambia BBC kuwa muda mfupi
baada ya msafara huo kushambuliwa, ndege za kivita za helikopta
zinazoaminiwa kuwa za Marekani zilishuka na kubeba maiti zote zilizo
kuwepo. Kwa hiyo kwa muda hakukuwa na thibitisho lolote iwapo Godane
mwenyewe aliuawa au la.
Upande wa AL shabaab nao walianza kukusanya watu
katika kijiji karibu na eneo hilo la Shebeele ambako shambulio
lilifanywa na kuwaua au kuwateka wengijne ambao hadi sasa hawajulikani
waliko.
AL shabaab hawakuzungumzia iwapo Godane alikuwa miongoni mwa waliouawa.
Leo asubuhi kulikuwa na picha zilizo sambazwa
katika mtandao ambazo hazikuthibitishwa zilizodai kuwa ni Ahmed Godane
bado alikuwa hai.
Al shabaab hawajasema lolote baada ya tangazo la Pentagon kuthibitisha kifo cha Godane.
BBC
0 comments:
Post a Comment