NI mshtuko , binadamu tumefikia hapa? Ndiyo maneno yaliyowatoka mamia
ya wananchi waliofika katika eneo la Bonde la Mbweni Mpiji Manispaa ya
Kinondoni jijini Dar es Salaam, baada ya kushuhudia shehena ya mifuko
iliyokuwa na viungo vya binadamu.
Katika eneo hilo, MTANZANIA ilishuhudia mifuko mikubwa mieusi ya
nailoni ikiwa na viungo mbalimbali vya binadamu vikiwa vimechunwa
ngozi.
Viungo hivyo ambavyo vilionekana nyama zake zikiwa zimekauka ni
pamoja na mafuvu ya vichwa, sehemu ya kifua cha binadamu, miguu, mikono,
moyo na mapafu.
Licha ya baadhi ya viungo kuonekana wazi kwa juu, vilikuwa havitoi
harufu jambo lililotafsiriwa kuwa vilikuwa vimepuliziwa dawa kali ya
kuondoa harufu.
Baadhi ya mashududa wa tukio hilo, waliiambia MTANZANIA kuwa miili hiyo ilitupwa eneo hilo tangu Jumapili Julai 20, mwaka huu.
Mmoja wa shuhuda wa tukio hilo, Super Kaijunga (45) alisema alikuwa mtu wa kwanza kuona viungo hivyo.
Alisema hali hiyo, ilisababisha kuwaita wananchi wengine wanaoishi
jirani na eneo hilo kabla ya kutoa taarifa kwa jeshi la polisi.
Alisema shehena hiyo, ilitupwa eneo hilo usiku wa kuamkia Jumapili
kwa sababu, ingawa wananchi wengi wanapita eneo hilo hawakutambua ni
kitu gani.
Kutokana na shehena hiyo kutotoa harufu, hakuna mtu
aliyejishughulisha kuigusa mifuko hiyo mpaka jana jioni, baada ya
baadhi ya wanawake wanaogonga kokoto katika eneo hilo walipokwenda eneo
hilo.
Alisema wanawake hao, walipofika eneo hilo walianza kufungua mifuko
hiyo kwa lengo la kuichukua kwa ajili ya kuhifadhia kokoto ndipo
walipokutana na viungo vya binadamu.
“Mimi jana (juzi) mpaka nimelala hapa na hii mifuko ilikuwa hapa
hakuna aliyeigusa. Jana ndiyo dada mmoja akaniita akaniambia nije
anionyeshe kitu cha ajabu. Ndiyo tukaja hapa tukaona hivi viungo
nikaanza kutoa taarifa,” alisema Kajuna.
Kutokana na kusambaa kwa taarifa za tukio hilo, wananchi wengi
walifahamu jana kuanzia saa 11 jioni hali iliyowalazimu kutoa taarifa
katika kituo cha Bunju na Wazo.
Polisi walifika eneo la tukio na kuanza kazi ya kuchukua mabaki ya
miili na kuijaza kwenye mifuko kisha kuipeleka katika Hosptali ya
Taifa ya Muhimbili kwa uchunguzi zaidi.
Pamoja na vitu vingine, mifuko hiyo mikubwa ndani ilikuwa na
vitaambaa maalumu ambavyo huvaliwa kifuani na madaktari kwa ajili ya
kuzuia uchafu pindi wanapofanya upasuaji wa mgonjwa.
Kutokana na tukio hilo, wananchi wengi wamejiuliza maswali mengi
huku baadhi wakisema kuwa viungo hivyo yawezekana vilitoka katika moja
ya hospitali kubwa.
“Kama viungo hivi ni vya hospitali kwa nini vitupwe huku wakati huwa
kuna sehemu za kuteketeza vitu kama hivi na kwa nini vichunwe ngozi,”
walisema baadhi ya wananchi waliokuwa katika eneo hilo.
Akizungumza na MTANZANIA kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Kipolisi wa Kinondoni Camilius Wambura alisema mifuko hiyo yenye
viungo vya binadamu iliyokutwa eneo la tukio ni zaidi ya 85.
Alisema baadhi ya viungo vilivyokutwa ni pamoja miguu, mikono na vichwa.
Alisema Jeshi la Polisi linalazimika kuvipeleka viungo hivyo Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa uchunguzi zaidi.
Baadhi ya wananchi walisema vungo hivyo vilifikishwa hapo na gari dogo maarufu kama kirikuu.
Kutokana na hali hiyo, gari moja la aina hiyo lilikuwa likienda
kwenye eneo hilo na lilipoona watu liligeuza na kukimbia kabla ya
kuzuiwa na vijana waendesha pikipiki.
Baada ya kukamatwa lilifikishwa katika kituo cha polisi Bunju hali
iliyofanya wananchi kujaa wakisema gari hilo lilikuwa limebeba viungo
vingine.
Hata hivyo baada ya polisi kulikagua gari hilo walibaini lilikuwa
limebeba mayai mabovu na vifaraka waliokufa walivyokuwa wakienda
kuvitupa katika eneo lililokuwa imetupwa viungo hivyo.
Kutokana na taharuki hiyo, polisi walilazimika kufyatua risasi za moto
hewani ili kutawanya umati wa wananchi waliokuwa wamefurika kwenye eneo
hilo.
Mtanzania
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment