Mtoto aliyeibwa, Merryn Reppyson
MTINDO mpya wa kuiba watoto jijini Dar es Salaam, umezusha hofu kwa
wazazi na walezi hali inayofanya baadhi yao kuhofia kutoka nyumbani na
kuwaacha watoto wao na wasichana wa kazi.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini katika kipindi cha wiki moja,
watoto wanne wameibwa na watu wasiojulikana na kutokomea nao katika
mazingira ya kutatanisha.
Moja ya tukio ambalo linaendelea kuvuta hisia za watu wengi ni lile
lililotokea eneo la Changanyikeni karibu na Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam.
Katika tukio hilo, Merryn Reppyson (3), alipotea Julai 15, mwaka huu baada ya mtu asiyejulikana kumchukua kutoka nyumbani kwao.
Akizungumza na MTANZANIA jana, mama mzazi wa Merryn, Elida Fundi,
alisema mtu aliyemuiba mtoto wake alifika nyumbani kwake na kuomba
kwenda msalani.
Elida alisema alipokutana na dada wa kazi mlangoni mtu huyo alimuulizia Merryn na wazazi wake.
Alisema baada ya mtu huyo kufika ndani ya nyumba aligonga mlango
akidhani kuwa mtoto yupo peke yake, lakini baada ya kugonga na kusikia
sauti ya mtu mzima ikimkaribisha alilazimika kuomba kuingia msalani.
“Huyu mtu alivyokuwa akiingia getini kwangu alipishana na dada
mlangoni, alihisi mtoto atakuwa ndani peke yake, baada ya kukuta kuwa
ndani kuna mtu mwingine tofauti na dada aliyepishana naye getini,
alilazimika kuomba kwenda msalani.
Dada aliyekuwa pale nyumbani alimuelekeza choo cha nje, alivyotoka
huko alikuta mtoto akiwa pale nje akamchukua na kuondoka naye, hicho
kilikuwa ni kitendo cha kama dakika tano tu.
Nimechanganyikiwa kabisa hapa, mtoto ameibwa na hatujampata mpaka
sasa, aliyemuiba anaonekana anatufahamu kwa sababu dada anasema alikuwa
anakuja siku moja moja hapa nyumbani na kutuulizia mimi na mume wangu
wakati anajua muda huo tunakuwa kazini.
Lakini pia alikuwa anamfahamu mtoto wangu mpaka kwa jina, akija hapo
anakuwa anamuita kabisa kwa jina, anamuuliza mama yupo? Baba yupo,”
alisema Elida.
Alisema kuwa mtu aliyemuiba mtoto huyo alifika nyumbani kwake kwa siku tatu tofauti na siku ya tatu ndipo alipomuiba.
Alifafanua dada aliyemkaribisha mtu huyo, alishangaa baada ya kuona mtu aliyeomba kujisaidia ameondoka bila kuaga.
Alieleza pia kuwa dada huyo alishangaa kutomuona mtoto nje hata hivyo, akajipa matumaini kuwa atakuwa ameingia chumbani.
“Dada wa kazi ambaye alikuwa amepishana na yule mgeni getini,
aliporudi nyumbani alimuulizia Merryn kwa kuwa hakumuona ndipo
walipoanza kumtafuta huku wakiwauliza majirani ambao walidai alipita na
mjomba wake ambaye alikuwa anaenda kumnunulia ndizi,” alisema.
Alisema wakati wakiendelea kumtafuta mtoto huyo walifika kwenye genge
lililo karibu na nyumba yake na kuambiwa kuwa mtoto huyo alifika hapo
na mtu aliyejitambulisha kuwa ni mjomba wake na kumnunulia ndizi kisha
wakaondoka.
“Tukio hili limenishangaza kwa kuwa hatujawahi kugombana na mtu,
itakuwa tu wamemchukua ili kututisha au tuwape pesa, lakini hatuna
ugomvi na mtu,” alisema Elida.
Alisema tangu kutokea kwa tukio hilo ambalo limeripotiwa katika kituo
cha polisi cha Changanyikeni, mpaka sasa hakuna taarifa zozote
zilizotolewa zinazohusiana na upatikanaji wa mtoto huyo.
Alisema majibu ambayo wamekuwa wakiyapata kutoka polisi ni kuwa uchunguzi bado unaendelea.
Wakati matukio hayo yakiendelea msichana, Islam Yasin (16), amepotea
katika mazingira ya kutatanisha uko Mbezi Msakuzi nje kidogo ya Jiji la
Dar es Salaam.
Islam ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya
Sekondari Mpigi Majohe, alipotea tangu Julai mosi hadi sasa hajulikani
alipo.
Taarifa za kupotea kwake zimeripotiwa katika kituo kidogo cha polisi
Mbezi kwa Yusuf na kufunguliwa jalada lenye kumbukumbu ya RB/6451/2014.
Akizungumza na MTANZANIA jana, mama mzazi wa binti huyo, Conses
Buberwa, alisema katika kipindi cha wiki mbili wamekuwa wakimtafuta
binti yake bila mafanikio.
Alisema yeyote mwenye taarifa za kupotea kwa msichana huyo atoe
taarifa katika kituo chochote cha polisi kilichopo jirani naye au apige
simu namba 0657004332.
Siku ya tukio, Islam alikuwa amevaa blauzi nyekundu na kubeba kanga
doti moja za aina tofauti ambazo alizihifadhi kwenye mkoba wake.
Kauli ya Polisi
Akizungumza na MTANZANIA, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni,
Camillius Wambura, alithibitisha kutokea kwa matukio hayo huku akisema
jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wake.
“Ni kweli tumepata taarifa hizo tunazifanyia kazi ili tuweze kujua ni
kina nani waliowaiba watoto hao, lakini bado ninaendelea kukusanya
matukio ya aina hii kutoka katika vituo vyote vya polisi ili tuweze
kubaini ukubwa wa hali ya matukio haya,” alisema Wambura.
Waziri Simba
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba,
aliliambia gazeti hili kuwa wizi huo unatokana na wazazi kutokuwa makini
katika masuala ya ulinzi kwa watoto.
“Jukumu la wizara ni kulinda haki za watoto, ulinzi wa mtoto binafsi
ni kazi ya mzazi Serikali haiwezi ikaweka polisi kila nyumba yenye
watoto kwa ajili ya ulinzi,” alisema Waziri Simba.
Alisema hivi sasa wazazi wamekuwa hawana muda na watoto wao na hata kushindwa kufuatilia taarifa za watoto wao.
“Serikali itaendelea kuwatafuta watu wanaofanya vitendo vya ukatili
wa watoto na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria,” alisema.
Ripoti ya utafiti uliofanywa na Chama cha Wanahabari Wanawake
Tanzania (Tamwa) katika mikoa 18 ya Tanzania Bara na Visiwani, imebaini
kuendelea kushamiri kwa vitendo hivyo huku matukio 996 ya udhalilishaji
yakiripotiwa kutokea katika wilaya sita za Zanzibar.
Kati ya matukio hayo, 242 yalihusu ubakaji, vipigo vilikuwa 388, ndoa
za utotoni 42, kutelekezwa 96, mimba za utotoni 228, ambapo kwa upande
wa Tanzania Bara ukionyesha kuwa Wilaya ya Babati mkoani Manyara
inaongoza ikiwa na matukio 132.
Ripoti ya Utafiti wa Ukatili dhidi ya Watoto Tanzania, iliyotolewa na
Serikali pamoja na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef)
mwaka 2011, ilidhihirisha kuwa msichana mmoja kati ya watatu na mvulana
mmoja kati ya saba nchini Tanzania hukumbwa na unyanyasaji wa kijinsia
kabla ya kufikisha umri wa miaka 18.
Mtanzania
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment