Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed
Gharib Bilal akiagana na Rais wa Malawi, Profesa Arthur Peter Mutharika,
baada ya shughuli za maadhimisho ya Sherehe ya miaka 50 ya uhuru wa
Malawi kukamilika katika uwanja wa Civo, jana Julai 06, 2014. Nyuma yake
ni Mama Asha Bilal.
Wa pili (kushoto) ni Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, Rais wa Malawi Profesa
Arthur Mutharika akifuatiwa na mkewe, Mheshimiwa Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal, Mama Asha
Bilal na viongozi wengine wakifuatilia sala maalum ya kuombea nchi ya
Malawi wakati wa sherehe za miaka 50 ya uhuru wa nchi hiyo zilizofanyika
jana Jumapili Julai 06, 2014 katika uwanja wa Civo jijini Lilongwe,
Malawi.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed
Gharib Bilal akiongozana na Mwenyeji wake Makamu wa Rais wa Malawi
Saulos Klaus Chilima kukagua gwaride maalum la makaribisho kwa
Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Tanzania baada ya kuwasili kwenye uwanja wa
Ndege wa Lilongwe kwa ajili ya kuhudhuria sherehe za miaka 50 ya uhuru
wa Malawi zilizofanyika Jumapili tarehe Julai 06, 2014.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mwenyeji wake Makamu wa Rais wa Malawi, Saulos Klaus Chilima, wakifurahia ngoma za asili za
Malawi, wakati wa mapokezi kwenye Uwanja wa Lilongwe, alipowasili
kuhudhuria sherehe za miaka 50 ya uhuru wa Malawi zilizofanyika Jumapili
tarehe Julai 06, 2014.
(PICHA ZOTE NA OMR)
MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA AIWAKILISHA TANZANIA KATIKA MAADHIMISHO YA MIAKA 50 YA UHURU WA MALAWI
Julai 06, 2014 Lilongwe.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
leo Jumapili Julai 06, 2014 ameiwakilisha Tanzania katika maadhimisho
ya miaka 50 ya Uhuru wa Malawi, sherehe zilizofanyika katika Uwanja wa Civo jijini Lilongwe.
Katika sherehe hizo pamoja na Makamu wa Rais wa Tanzania, pia alihudhuria Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe, Waziri Mkuu wa Msumbiji na viongozi mbalimbali waliowakilisha nchi kutoka Afrika.
Sherehe hizo zilianza kwa ibada ya misa asubuhi na kisha kuhamia katika uwanja wa Civo mchana ambapo Rais wa Malawi Prof. Athur Peter Mutharika alikagua gwaride na kisha kuwasha Mwenye wa Jubilee ya miaka 50 na baadaye
kulihutubia taifa.
Akizungumza katika sherehe hizo, Rais Mutharika alisisitiza kuhusu umuhimu wananchi wa Malawi kuwa wamoja na akaeleza nia yake ya kujenga umoja kwa nchi zinazoizunguka Malawi pamoja na zile za Kusini mwa Afrika.
Baada ya hotuba hiyo, sherehe hizo ziliendelea na mchezo wa soka baina ya timu ya taifa ya Malawi na Msumbiji.
Malawi ilipata uhuru wake mwaka 1964
ikiongozwa na Rais wake wa kwanza Dkt. Kamuzu Banda hadi mwaka 1994.
Baada ya mwaka huo alifuata Rais Dkt. Bakili Muluzi aliyetawala kuanzia mwaka 1994 hadi 2004.
Baaada ya mwaka huo alifuata Rais Profesa
Bingu wa Mutharika aliyetawala hadi mauti yalipomkuta mwaka 2012. Dkt.
Joyce Banda aliyekuwa Makamu wa Rais wa Mutharika alichukua madaraka na
kukaa hadi mwaka huu 2014 ambapo Malawi iliingia katika uchaguzi mkuu na
kisha Rais Profesa Arthur Peter Mutharika aliposhinda uchaguzi huo na
hivyo kuwa Rais wa nne wa Malawi.
Katika sherehe hizo Mheshimiwa Makamu wa Rais pia
alifuatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
Mheshimiwa Mahadhi Juma Maalim na Mheshimiwa Makamu wa Rais amerejea
nyumbani Tanzania Julai 07, 2014 tayari kuendelea na majukumu mengine ya
kitaifa.
Imetolewa na: Ofisi ya Makamu wa Rais
Julai 06, 2014 Lilongwe: Malawi
0 comments:
Post a Comment