Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe
ZIPO sababu na vipo visingizio. Visingizio ni vitu au ni mambo yale ambayo tunayalaumu ili tu kukwepa kukilaumu kile hasa kinachohusika na matatizo yetu.

Kwa mfano, mtu akiambiwa kuwa barabara anayotaka kuitumia ina miiba mikali na yeye akaamua kuendelea kuifuata, akichomwa na miiba anaweza kuchagua kulaumu kisingizio au sababu.
 
Kisingizio ni rahisi sana kwani anaweza kusema amechomwa na miiba kwa sababu viatu vyake vilikuwa laini sana na hivyo miiba ikapenya – na ni kweli inawezekana viatu ni laini na ni kweli miiba imepenya. Lakini sababu hasa ni kuwa hakusikiliza maonyo na hakujiandaa ipasavyo.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambacho ni kipenzi na chaguo la mamilioni ya watu wanaotaka mabadiliko mazuri ya kisiasa nchini, kinakabiliwa na uchaguzi wa kuamua kutafuta visingizio au kutafuta sababu ya kwanini kinapata shida kushinda chaguzi hizi ndogo na kinahitaji kutumia nguvu kubwa sana kushinda viti vichache sana.

Matokeo ya chaguzi za udiwani zilizofanyika Jumapili yameonyesha kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeendelea kuwa kizingiti (kisiki labda ni neno zuri zaidi) cha upinzani Tanzania kwani bado hakijaonyesha dalili ambazo tunahubiriwa kila siku kuwa kiko tayari kuondoka madarakani.

CHADEMA na tatizo la kupendwa
Nimewahi kuandika mara kadhaa huko nyuma, lakini ifae kurudia tena hapa; CHADEMA inasumbuliwa na tatizo la kupendwa sana. Katika huku kupendwa haitaki kujiangalia kama imevaa nguo nzuri au la; haitaki kuangalia kama vipodozi vinaendana na rangi ya ngozi yake au hata kama rangi ya midomo imevaa vizuri au imeenda hadi mashavuni!
Ukijua kuwa unapendwa au unapendeka unaweza kujikuta unaanza kunata; kuringa au kujiona. Unajiona kuwa wewe ndio wewe hakuna mwingine na kuwa wanaokusema ama wanakuonea wivu au hawawezi kujipara kama wewe!

Katika kufanya hivyo mtu hajioni makosa yake na ukichelewa sana hata watu ambao walikuwa marafiki hawakuonyi tena wanakuacha tu huende kujiaibisha mwenyewe hadi siku ile picha yako itokee kwenye gazeti moja la udaku umesaula kama popo kwenye paa la pango! Ukijiona mzuri usishangae watu wakakuacha udhurike!

CHADEMA inapendwa na hili halina shaka; wapo watu wanaipenda kiasi cha kutoa mali na hali zao kuitetea na kuipigania. Wapo wenye kuipenda kiasi cha kufa; na wapo waliokufa kwa ajili ya CHADEMA au katika mazingira ya kukitetea chama.

Maelfu kama siyo mamilioni ya Watanzania wanaiona CHADEMA kama mkombozi wao na wanaiona kama chama mbadala wa CCM na ni kwa sababu hiyo matokeo ya uchaguzi huu mdogo uliopita yamewagusa watu hawa si kwa namna ya kufurahisha au kufariji; yamewaacha na maswali ambayo bado hawajayapatia majibu yake.

CHADEMA isifiche kichwa kama mbuni
Jambo baya zaidi katika kutafuta visingizio ni kujaribu kujifanya huoni tatizo au hutaki kuliona tatizo. Mbuni ni ndege mwenye umbo kubwa, lakini pia mwenye kichwa kidogo ukilinganisha na umbo lake. Fikiria mbuni ajaribu kujificha kwa kuchomeka kichwa mchangani au nyuma ya kijiti akiamini kuwa haonekani.

Kufanya hivi ni kutokuwa mkweli kwa sababu alichofanya ni kujificha yeye asione siyo yeye asionekane. Ni kwa sababu hiyo msemo wa kutokuficha kichwa mchangani upo; kwamba kuna wakati inabidi tuwe tayari kuuona ukweli na tusijizibe wenyewe kuona kwa kudhani hatuonekani.

CHADEMA inapaswa kukubali kosa lake kubwa ambalo limeendelea kuwasumbua sasa, na kwa muda mrefu sasa wamekuwa kama mbuni na kichwa mchangani. Wakati umefika wauone ukweli.

Visingizio hivi si vya kweli
Maelezo ambayo yamekuwa yakitolewa mara kwa mara kuelezea kutokufanya vizuri zaidi kwa CHADEMA au kuhalalisha kuwa wamefanya vizuri kulinganisha na huko nyuma yamepitwa na wakati kwani hayatoshi kuelezea kwanini CCM bado inatamalaki! Baadhi ya maelezo ambayo tumeyasikia huko nyuma na yanatolewa tena hivi sasa ni haya:

CCM inatumia nguvu za dola kuminya upinzani, watu wanauza shahada zao, Tume ya Uchaguzi inapendelea CCM, Daftari la Wapiga Kura halijaboreshwa hivyo wanachama na mashabiki wengi wa CHADEMA hawapigi kura, CCM wameshinda kwenye kata zao na wao ndio wamepoteza zaidi kuliko CHADEMA.

Hivi ndivyo visingizio vikubwa vya kufanya vibaya kwa CHADEMA au kutokufanya vizuri zaidi kama ilivyotarajiwa au kuaminiwa. Ninaposema ni visingizio sitaki kueleweka kuwa navipuuzia kuwa havina maana au si vya kweli; la hasha.

Ninachosema hasa ni kuwa hizi siyo sababu hasa za kwanini CHADEMA inashindwa kuigaragaza CCM na kuwapa furaha wanachama na mashabiki wake badala ya kushinda sehemu ambazo watu walitarajia itashinda au kufanya mgaragazo (upset) moja kama ya Njombe. Sasa tukikubali hoja hizi tunakubali visingizio na hivyo tutakuwa tunasubiri tena maelezo kama haya Chalinze na Kalenga!

Kosa kuu la CHADEMA
Binafsi naamini kosa kubwa la CHADEMA kuhusiana na hizi chaguzi ndogo ndogo lilifanywa kabla ya uchaguzi wa 2010 na limeendelea kufanywa baada ya uchaguzi ule uliolitetemesha taifa na kutikisa ngome za CCM. Kosa hili ni CHADEMA kukubali kwenda kwenye uchaguzi chini ya tume ile ile, sheria zile zile, mfumo ule ule wa uchaguzi! Kosa hili linatokana na CHADEMA kuamini katika wema wa CCM na hisani ya serikali kuwa yumkini wataweka mazingira mazuri ya kuusaidia upinzani ushinde! Hili ni kosa kubwa zaidi la kimkakati na litaendelea kuwang’ata CHADEMA kwenye makalio hadi watakapolikubali na kulisahihisha.

Kitendo cha CHADEMA kuendelea kukubali kushiriki chaguzi hizi chini ya sheria zile zile mbovu (zisizoweka utaratibu mzuri wa kusimamia uchaguzi, au kuandikisha wapiga kura) na mfumo ule ule (wenye kupendelea CCM) ni kukubali matokeo yake!

Nimewahi kuandika huko nyuma – nafikiri ilikuwa wakati wa uchaguzi wa Arumeru Mashariki na hata ule wa Kiteto – kuwa CHADEMA inapokubali kuingia uwanjani huku inajua sheria za mchezo ni mbovu, refa amenunuliwa, na hakuna uwezekano wa “fair play” basi inakuwa imekubali na matokeo!

Ndiyo maana kwenye michezo mingine watu wanagomea kabisa kwenda uwanjani kwa sababu hawaamini kuwa mchezo utakuwa huru na wa haki kwa pande zote. Uchaguzi wa Tanzania tayari umethibitisha kuwa hauwezi kuwa wa haki na huru kwa kadiri ya kwamba mfumo wetu haujajengwa katika kutetea haki za raia! Unaweza vipi kuwa na uchaguzi ambao watu hawaandikishwi kupiga kura?

Hili ni kosa kubwa; haya yote ambayo nimeyaita ni visingizio ni matokeo tu ya kosa hili! Kwa kukubali kuendelea kushiriki chaguzi hizi chini ya mfumo na sheria hizi mbovu CHADEMA inapoteza haki ya kulalamika!

Kitu cha kwanza ambacho wengi tulikiona kabla ya uchaguzi wa 2010 ni kuwa mvuto wa Dk. Slaa ulishtua sana CCM kiasi kwamba kama watu wangekuwa wanaruhusiwa kujiandikisha kupiga kura wakati wa kampeni, matokeo yangekuwa tofauti sana. Mfumo wetu wa kujiandikisha kupiga kura ni lazima ubadilishwe.

Baada ya uchaguzi ule, nilitarajia – na niliandika hili kwa kina – kuwa CHADEMA wangepigania kuhakikisha kuwa mfumo wa kuandikisha watu kupiga kura ungebadilishwa; mojawapo ni kulifutilia hili ‘daftari la wapiga kura’ la kitaifa!

Sioni mantiki kwanini kuwe na daftari moja (kwa maana ya kuwa orodha moja inayosimamiwa na tume). Kwanini watu wasiandikishwe kupiga kura kwenye halmashauri zao? Kuna ubaya gani kuwa na mfumo unaoruhusu watu kujiandikisha kupiga kura muda wowote wa mwaka na kuwa endapo uchaguzi unatokea basi majina yaliyoko kwenye orodha hiyo kwa kipindi cha siku thelathini zilizopita ndiyo yatatumika badala ya miaka kama ilivyo sasa!

Hivi hili kweli tunahitaji ma-genius kutoka Uingereza kuja kutusaidia kuona linafanyika? Hivi mbona hili halina gharama kubwa ya hivyo?

Siyo tu kupigania suala la uandikishwaji, lakini Sheria ya Uchaguzi na Tume ya Uchaguzi vilitakiwa kufanyiwa mabadiliko. Badala yake ndugu zetu CHADEMA wakakubali kanyaboya la “Katiba Mpya” ambalo liliwazuia kupigania mabadiliko mengine kwani mambo yote wameambiwa “kwenye Katiba Mpya”.

Kila mtu akitaka kutoa wazo wanaambiwa “subirini Katiba Mpya” wakati sote tunajua kuwa katiba mpya isipopita katiba ya sasa itatumika na kimsingi mifumo ya sasa itatumika! Lakini CHADEMA wamekubali!

Sasa wafanye nini?
Binafsi nina mapendekezo machache tu ya kuwasaidia ndugu zetu hawa, kama wanaweza kusaidika kwa kweli.

Mosi, ni kutangaza kutoshiriki uchaguzi wa Kalenga na Chalinze kama Tume ya Uchaguzi haitowapatia wananchi wa huko haki ya kujiandikisha kupiga kura, wale ambao hawajaandikishwa.

Hoja kuwa ati wakijitoa CCM watapita ni hoja isiyo na msingi; tayari majimbo hayo yalikuwa ya CCM na kama wakiyarudisha basi wayarudishe huku wakijua kuwa wamewaburuza watu. Kukubali kushiriki ni kukubali matokeo yake na kwa kweli kutumia gharama zisizo za lazima.

Pili, kuweka shinikizo kwa Tume ya Uchaguzi kubadilisha utaratibu wake wa kuboresha daftari la wapiga kura na kutaka utumike mfumo mzuri wa kuliboresha katika vipindi vinne vya mwaka (yaani kila baada ya miezi mitatu).

Hii ina maana kuwa mtu yeyote ambaye anataka kujiandikisha kupiga kura au kubadilisha taarifa zake anaweza kufanya hivyo wakati wowote ndani ya miezi mitatu kabla daftari halijaboreshwa (updated) katika robo ile ya mwaka. Hii ina maana ya kuwa daftari la wapiga kura litakuwa la wakati mno kuliko ilivyo sasa.

Tatu, CHADEMA ifikirie sana juu ya namna ya kuwashawishi watu ambao si wana-CHADEMA au wapinzani kupigia kura wagombea wake. Hili ni jambo la muhimu sana kwa sababu tunakoelekea tofauti ya ushindi itakuwa si kwa wanachama na mashabiki kupigia kura chama bali kwa wale wasio wanachama na wasio mashabiki kushawishiwa kupiga kura.

Kwa mfano, katika kata nyingi inaonekana bado CHADEMA haijaweza kuwashawishi watu wengi zaidi wasio CHADEMA kupigia kura. Kwanini? Hili linahitaji kufanyiwa utafiti kidogo.

Nne, CHADEMA isidharau ukweli mmoja ambao labda wapinzani na wale wapenda mabadiliko wakati mwingine hatuamini kuwa ni kweli; CCM ina watu wenye kuipenda na wanaipenda kweli kweli. Hili nitaliangalia kidogo kwa kina wiki ijayo, In Shaa Allah.

Wakati mwingine katika kufikiria tunapendwa sana tunajisahau kuwa wapo wengine ambao nao wanapendwa. Labda tunafikiri tunapendwa kwa sababu tunatoka nadhifu sana, mkwanja wa nguvu na ujiko wa kila namna, na katika mazingira hayo tunasahau kuwa labda wengine wanapendwa pia kwa sababu nyingine!

Kudhania kuwa watu wengi wanaichukia CCM ni kutokuwa wakweli kwa sababu matokeo lukuki yanaonyesha kuwa CCM bado inapendwa na watu na wengine hata kama hawakubaliani nayo sana, lakini bado wako tayari kuipa kura yao kuliko kupeleka upinzani; hili nalo linahitaji jibu: kwanini?

Kwanini wapo watu, tena wengine maskini kabisa, na wamechoka hadi ulimi, lakini watu hao hao wenye kulalamikia shule, maji, elimu, afya wakipewa nafasi kuchagua bado wanaichagua CCM? Kwanini? CHADEMA isipuuzie hili jibu na hawa ndio watu ambao inatakiwa itafute mbinu ya kisasa ya kuwafikia kwani ndio tofauti ya kushindwa na kushinda!

Ni matumaini yangu kuwa hoja yangu itazua mjadala na kuona kama kweli visingizio vinavyotolewa vinatosha na kama sababu niliyoisema mimi ina ukweli wake au na mimi natafuta visingizio tu ila sababu yenyewe nimeikwepa pia. Au na msomaji anatafuta kisingizio cha kwanini sababu yangu siyo ya kweli!? Heri ya Mwaka Mpya kwa wasomaji wangu!
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top