Ripoti iliyotolewa na viongozi watatu wa zamani wa
mashitaka ya uhalifu wa kivita inasema kwamba kuna ushahidi wa kutosha
wa kuthibitisha kuwa Syria imewatesa na kuwaua karibu wafungwa 10,000
tangu kuanza harakati za kumpinga Rais Bashar Al-Asaad.
Wachunguzi walipekua maelfu ya picha za wafungwa
waliokufa zilizotolewa nchini Syria na mpiga picha mmoja wa jeshi
aliyetoroka kazi.
Wanasema miili mingi ilikuwa imekonda na mingine mingi kupigwa na kunyongwa.
Mmoja wa waandaaji wa ripoti hiyo, Professa
Geoffrey Nice, aliiambia BBC kuwa wingi na uhakika wa ushahidi uliotolewa
unaonyesha wazi kuwa Serikali ilihusika katika ukatili huo.
Uchunguzi huo ulifadhiliwa na Serikali ya Qatar
inayowaunga mkono waasi wa Syria. BBC imejaribu mara kadhaa kupata
majibu ya Serikali ya Syria kuhusu madai hayo lakini Serikali haijatamka
lolote.
Madai kuwa wafungwa wamekuwa wakiteswa na kuuawa
katika magereza ya Syria yamekuwa yakitolewa mara kwa mara na
wakereketwa wa haki za kibinadamu tangu maasi yaanze nchini humo miaka
mitatu iliyopita.
Hata hivyo madai ya sasa yana upya fulani kwa njia ya kipekee.
Habari hizi zina ushahidi kutoka kwa wandani wa
Serikali wenyewe; mpiga picha wa kitengo cha jeshi cha polisi
aliyetoroka kazi amewasilisha maelfu ya picha ambazo alipiga kabla ya
kutoroka.
Na wachunguzi wa kimataifa, waliokuwa viongozi
wa mashtaka sasa wanaamini kuwa picha walizoona za miili iliyoharibiwa
vibaya, iliyopewa nambari na kupigwa picha mara kadhaa, ni ushahidi wa
kuaminika.
Zaidi ya miili 11,000 ilipigwa picha ingawa bado
kuna wasiwasi kuwa kuna maelfu ya watu ambao walizuiliwa magerezani
lakini sasa hawajulikani waliko.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment