
Frederick Sumaye
WAZIRI Mkuu mstaafu Frederick Sumaye amewananga wanaomuita kuwa
muasisi wa takrima akidai kuwa uelewa wao ni mdogo juu ya suala hilo.
Wiki iliyopita, Sumaye akiwa katika ibada ya harambee ya kuchangia
ujenzi wa ukumbi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi katika Parokia ya
Mawella, alidai kuwa uchaguzi wa sasa nchini umegubikwa na rushwa na
vishawishi vingi badala ya kuzingatia ubora, uhodari na tabia ya
anayesaka uongozi.
Kufuatia kauli hiyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis
Mgeja, alimjia juu Sumaye na kusema kuwa ni kama analamba matapishi yake
mwenyewe kwa sababu ndiye aliasisi rushwa ya uchaguzi.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano jana kwa njia ya simu, Sumaye
alisema kuwa ni upuuzi kwa wanaomuita muasisi wa sheria hiyo kwa kuwa
Bunge ndilo lenye jukumu la kutunga sheria.
Sumaye alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tatu sio muasisi wa sheria
ya takrima kama inavyoelezwa, bali suala hilo lilianza miaka ya nyuma na
ikalazimu kufanyiwa marekebisho na Bunge.
“Hii sheria ilitoka katika Local Government na kuja katika uchaguzi
mkuu, na Bunge ndilo lililopitisha sheria hiyo, sasa kama kuna kikundi
cha watu kinajitokeza na kuniita mimi muasisi, hao watakuwa hawana
uelewa wa suala hilo,” alisema.
Alisema kuwa hata kupitia hotuba yake aliwahi kueleza kuwa sheria
hiyo inapaswa isitumike vibaya, lakini hao wanaompinga juu ya rushwa
ndio vinara wa kupindisha sheria hiyo.
Waziri Mkuu huyo mstaafu alisema kuwa nia ya Bunge kuweka sheria hiyo
ilikuwa njema, lakini baadhi ya viongozi, hasa wanaowania nyadhifa
mbalimbali ndio wanaoiharibu.
Sumaye alisema kuwa kutokana na sheria hiyo kuharibiwa, ni vyema
Bunge likaangalia namna ya kuiondoa ili kuepusha chaguzi kutawaliwa na
rushwa.
“Nafikiri uelewa wa wanaonipinga ni mdogo na hawana ufahamu kuhusiana
na suala hilo, imefika wakati sasa kuona umuhimu wa kuiondoa sheria
hiyo, hasa kwa Bunge ambao ni muhimili unaohusika na kutunga sheria
kwani maana halisi ya takrima imeharibiwa,” alisema.
Alisema kuwa takrima ilikuwa ni lengo jema kwa kundi linaloshirikiana
na mgombea kuweza kupewa chakula baada ya kumaliza kampeni na sio
kumwaga fedha kama inavyojitokeza sasa.
Katika hotuba yake aliyotoa katika ibada hiyo, Sumaye alisema
kiongozi hutafutwa na jamii husika kutokana na ubora wake na siyo
vishawishi vyake.
“Kama nilivyokwishaeleza, uongozi hautafutwi kwa udi na uvumba wala
kwa rushwa, bali anayefaa kuwa kiongozi hutafutwa na jamii husika
kutokana na ubora wake na siyo vishawishi vyake.
Ni ukweli ulio wazi kuwa leo chaguzi zetu zimegubikwa na rushwa na
vishawishi vingi na siyo ubora, uhodari wala tabia ya anayetaka nafasi
hiyo ya uongozi,” alisema.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment