Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe
Polisi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Dar es Salaam,
wanatajwa kuwa wahusika wakuu wa kusaidia wahamiaji haramu kuingia
nchini, kinyume cha sheria.
Septemba mwaka jana, mfanyakazi wa Wakala wa Ndege
za Serikali, Dominic Bomani alimwambia Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison
Mwakyembe alipotembelea uwanjani hapo kuwa wapo wahamiaji haramu ambao
wamepewa nafasi nyeti za ajira katika uwanja huo. Dk Mwakyembe aliahidi
kufuatilia suala hilo.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa polisi katika
baadhi ya viwanja vya ndege wamejenga mtandao na watumishi wengine,
wakiwamo wa Idara ya Uhamiaji ambao huwawezesha raia wa kigeni hasa
kutoka nchi za Ethiopia, Somalia na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo
(DRC), kuingia nchini bila ya kuwa na nyaraka zinazokubalika kisheria.
Tukio la karibuni zaidi ni lile la kuingizwa
nchini kwa raia watatu wa Pakistani ambao licha ya kukamatwa katika
Uwanja wa Ndege wa zamani (Terminal – I) kutokana na kutokuwa na hati za
kusafiria, wala nyaraka zozote zinazowaruhusu kuingia nchini, baadaye
waliachiwa na kuingia nchini katika mazingira ya kutatanisha.
Chanzo chetu uwanjani hapo kilisema: “Hawakuja na
hati za kusafiria wala nyaraka zozote na waliachiwa huru katika
mazingira ya kutatanisha.”
Chanzo hicho kiliwataja Wapakistani hao kuwa ni
Hussein Amir, Ahmad Tahmir na Shakeel Muhamadadi ambao walifika nchini,
Oktoba Mosi, 2013 saa kumi na moja jioni kwa ndege ndogo ya kukodi
ambayo ilikuwa ikitokea Zanzibar.
Baada ya kufika, walishukia Terminal 1 na baadaye
kwenda kuswali katika msikiti wa karibu, lakini kabla ya kutimiza azma
yao hiyo, walikamatwa na polisi kisha kufunguliwa hati ya kukamatwa (RB)
namba JNIA/1005/2013.
Mapema baada ya kuwasili kwao, wageni hao
walipokewa na Dereva Teksi, Shami Maringo ambaye alikiri kwamba
aliagizwa kuwapokea, lakini kabla ya kuanza safari waliomba kwenda
msikitini kuswali kwa sababu ilikuwa tayari ni saa 12:00 jioni.
Maringo alisema aliwapokea raia hao watatu baada
ya kupewa majina yao na Mtanzania mwenye asili ya Asia ambaye alimwambia
baada ya kuwapokea awapeleke Kariakoo.
“Nilipewa majina matatu kwenye karatasi na mhindi
mmoja, nikaambiwa hao watu watafika saa 10 jioni. Walipofika
nikawatambua lakini tulikamatwa,” alisema Maringo.
Maringo pia alikamatwa na kuambiwa kuwa ataachiwa baada ya mtu aliyemwagiza kuwapokea raia hao atakapofika.
Alisema siku ya pili asubuhi, mtu huyo ambaye hata
hivyo, alisema hamfahamu kwa jina, alifika polisi na Maringo pamoja na
raia hao waliachiwa huru. Maringo anasema hakuweza tena kuwapeleka kwa
sababu gari lake lilipata pancha.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa tukio la kukamatwa hadi
kuachiwa kwa raia hao wa Pakistani lilimhusisha Ofisa Upelelezi Kituo
cha Polisi cha JNIA, Denis Moyo.
Chanzo chetu cha habari kinaeleza kuwa ili kufuta
ushahidi wa tukio hilo, taarifa za wahamiaji hao haramu hazikuandikwa
katika kitabu cha rekodi za polisi kama inavyotakiwa.
Kauli za wahusika
Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege, Seleman
Hamis anasema taarifa hizo ni za kushtua kwani hakudhani kama mambo kama
hayo yanaweza kutendeka kwani ulinzi mkali umewekwa uwanjani hapo.
“Nashukuru kwa taarifa hizi, unajua nyinyi
waandishi wa habari ni wa muhimu sana katika habari za uchunguzi na
mnaweza kutusaidia katika kazi zetu,” alisema.
Kamanda Hamis alisema inawezekana kabisa kuwa watu
wanafanya vitendo vya uhalifu huo pasipo polisi kufahamu. Hivyo
wananchi hawana budi kutoa ushirikiano ili kuutokomeza.
Moyo ambaye pia ni Msaidizi wa Mkuu wa Makosa ya
Jinai wa JNIA alipoulizwa kuhusu madai hayo badala ya kujibu, aliuliza
maswali mengi, huku akitaka apewe majina ya baadhi ya wahamiaji hao.
Baada ya kupewa, aliomba apewe dakika chache kisha
apigiwe tena na alipopigiwa simu baada ya dakika 20 alisema: “Nashukuru
kwa taarifa nitazifanyia kazi, ilimradi umenipa taarifa basi
nitazifanyia kazi.”
Kabla ya kutoa majibu hayo, ilisikika sauti ya
mwanamke ambaye hakufahamika ikimwelekeza: “Mwambie kwamba suala hilo
litashughulikiwa.”
Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa JNIA,
Felisia Mtenga alikanusha kuwapo kwa taarifa hizo na kusema hakuna suala
kama hilo katika uwanja huo ingawa alimtaka mwandishi kuzungumza na
Moyo.
Kwa upande wake, Meneja wa Usalama wa Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Clemence Jingu alisema hafahamu suala
hilo na haliwezekani kufanyika katika uwanja huo akisema ni lazima mgeni
yeyote anayefika awe na hati ya kusafiria, tiketi ya kurudi na viza.
Hata hivyo, alisema hakuna tatizo iwapo wageni
wanafika na ndege ya kukodi wakitokea Zanzibar kwani uwanja wa huko
unatakiwa kuhakikisha kuwa wana nakala zote za kusafiria na wanapofika
Dar es Salaam hufika kama watu wa kawaida hivyo, hakuna haja ya
kuangaliwa upya.
“Kila uwanja wa kimataifa una sheria zake, akitua Zanzibar
halafu akakodi ndege kuingia Dar es Salaam, hana haja tena ya kuonyesha
documents (nyaraka) zake, anaingia kama mwenyeji tu,” anasema Jingu.
Alipoelezwa kuwa wapo wahamiaji haramu wanaoingia
kupitia JNIA moja kwa moja kutoka nje alisema ni vigumu mno...
“Haiwezekani wakawahonga, uhamiaji, polisi wa uwanja wa ndege na kila
mtu, ni vigumu. Lakini kama kuna suala kama hilo sijalisikia na
silifahamu. Zungumza na watu wa Uhamiaji.”
Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Naibu Kamishna
wa Uhamiaji, Abbas Irovya alipoulizwa alisema: “Tunashukuru kwa taarifa,
lakini nafikiri tukipata ushahidi kamili kama muda wa tukio,
waliohusika na jinsi matukio hayo yanavyofanyika, tutashukuru zaidi kwa
sababu mtakuwa mmetusaidia.”
Mamlaka za Zanzibar
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdani Makame
alisema ingawa ameishika nafasi hiyo Zanzibar kwa muda mfupi lakini
anafahamu kuwa kuna tatizo la wahamiaji haramu.
“Ni pana, linahitaji mshikamano wa kila kitengo.
Kama wahamiaji wametokea Pakistani lazima watakuwa wameanza kufanya
mchezo huo tangu huko walipotoka kwa hiyo ni tatizo mtambuka,” alisema
Kamishna Makame.
Alisema Uwanja wa Ndege Abeid Amani Karume
unakabiliwa na uhaba wa watenda kazi jambo ambalo alikwishapelekewa
malalamiko na RPC wake.
Mkurugenzi wa Uwanja huo, Juma Salehe alisema
hajapata taarifa hizo... “Zipo tuhuma za hapa na pale ambazo huwa
tunazifanyia kazi na iwapo zinatushinda tunazipeleka ngazi za juu,
ingawa kwa tukio la hao raia wa Pakistani, sijalisikia.”
Alisema suala la wahamiaji haramu limesambaa kwani
hata uhamiaji nao huenda wanahusika kwani ndiyo wanaohakiki hati za
kusafiria na visa.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment