Jeshi nchini Sudan Kusini limewataka wananchi wote kuondoka kutoka mji wa Bentiu ambao ulitekwa na waasi watiifu kwa makamu wa zamani wa Rais Riek Machar.

Aidha jeshi hilo linasema kuwa linakaribia kuutwaa mji huo ambao hivi karibuni umekuwa kitovu cha mapigano yanayoendelea nchini humo.

Msemaji wa jeshi Philip Aguer, amedokeza kuwa wanajeshi wa serikali wako viungani mwa mji huo na kuwa wanakabiliwa na upinzani mdogo sana katika juhudi zao za kuuteka mji huo.

Taarifa zinasema kuwa mapigano yameripotiwa kutokea katika mji wa Bentiu kati ya wanajeshi wa serikali na waasi watiifu kwa Riek Machar ambao wamekuwa wakiudhibiti mji huo.

Umoja wa Mataifa ambao umekuwa ukiwahifadhi watu 8,000 katika mojawpao ya kambi zake viungani mwa mji huo, ulisema kuwa kikosi chake cha wanajeshi nchini humo kimekatiza uhusiano wowote wa kijeshi na serikali na kwamba liko tayari kukabiliana na mashambulizi yoyote.

Maelfu ya watu wamekuwa wakiukimbia mji huo wenye utajiri wa mafuta na ambao ni mji mkuu wa jimbo la Unity, huku majeshi ya serikali yakijiandaa kuupigania.

Mpatanishi mkuu kwenye mazungumzo ya kusitisha vita kati ya pande zinazozozana, Seyoum Mesfin, mjini Addis Ababa Ethiopia, anasema kuwa ana matumaini kuwa mwafaka wa amani utaweza kupatikana.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top