Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi , Dk David Mathayo.…
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha.
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi , Dk David Mathayo.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamisi Kagasheki.
Rais Jakaya Kikwete amekubali kutengua uteuzi wa mawaziri wanne kufuatia shutuma nzito dhidi yao katika sakata la Operesheni Tokomeza Ujangili zilizotolewa Bungeni na Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ikiongozwa na Lembeli (Mb).
Taarifa ya kutenguliwa huko iliyotolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, iliwataja mawaziri hao kuwa ni Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii) ambaye awali alitangaza kujiuzulu, David
Mathayo (Mifugo na Uvuvi), Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani) na Shamsi
Vuai Nahodha (Ulinzi na JKT).
"Rais ameamua kuchukua uamzi wa kutengua uteuzi wa Mawaziri wote wanne pamoja na Dk David Mathayo"
Waziri Pinda alifafanua zaidi kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo hakuhusika moja kwa moja hivyo kupoteza nafasi hiyo haimaanishi kuwa hafai kupewa nafasi ya uwaziri.
"atakuja (Rais) kuliona hilo lingine ambalo limejitokeza kwa maana hiyo ya pengine pengine katika sura tofauti kidogo kwa maana ya kutengua leo haina maana kuwa hawezi kumpa nafasi katika nafasi nyingine ya uwaziri".
Msimamo wa Kamati
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na mazingira, James Lembeli alisisitiza kuwa Dk. Mathayo anahusika moja kwa moja katika sakata hili kwa vile kutowajibika kwa Wizara yake ni chanzo cha mifugo kuingia katika hifadhi.
"Huwezi kutibu tatizo la mifugo kuingia hifadhini bila kuihusisha Wizara ya Mifugo"
Lembeli aliwashangaa watu wanaomtetea DK. Mathayo na yeye mwenyewe alivyopata ujasiri wakati akitetewa na baadhi ya wabunge walioona kuwa ameingizwa katika sakata hili bila sababu za msingi.
"Ukiona mtu anatetewa kwa hoja zisizo na mashiko kuna kitu. Mawaziri wengine wametetewa lakini hatukuona munkari ambayo Waziri wa Mifugo na Uvuvi alisimama na kushangilia wakati wabunge wakisema ameingizwa kinyemela kwenye sakata hili"
Kagasheki
Lembeli alifafanua zaidi kuwa chimbuko la matatizo sio Waziri Kagasheki bali Katibu mkuu wake aliyeandaa mpango kazi usiotekelezeka uwandani. Kama haitoshi, andiko la mwisho la mpango kazi huu halikupelekwa kwa Waziri Kagasheki ili aupitie.
Lembeli alilieleza Bunge pia kuwa mfumo uliopo unaowawajibisha mawaziri na kuwaacha watendaji wengine utaendelea kuifanya serikali ibadilishe mawaziri kila mara bila ufumbuzi wa tatizo kupatikana.
Hivyo Kamati ikashauri kuwa serikali ianze kuwawajibisha hata watendaji wengine wanaohusika na kupanga mipango isiyotekelezeka katika Wizara kwa vile kufanya hivyo kunaweza kuwa ni suluhu ya kubadilisha mawaziri kila mara.
"Kiwepo kipengele kinachowataka watendaji wote walioshiriki kuandaa mpango kazi usiotekelezeka wawajibishwe"
"Tukitaka kuondosha tatizo la nyoka ambaye kila siku anagonga vifaranga ni kumsaka nyoka aliko na kumbonda kichwa! mambo yataenda!" Alisema Lembeli.
Aidha, Bunge lilielezwa na Kamati hii kuwa kuna tatizo kubwa la rushwa katika Wizara ya Maliasili na Utalii ambapo watu hutumia simu kukusanya fedha. Hivyo, Kamati ikashauri serikali kulifanyia kazi.
Hatima ya Nchimbi na Nahodha
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk
Emmanuel Nchimbi na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi
Vuai Nahodha katika taarifa ya Waziri Mkuu na ile ya Kamati ya bunge hawakupata utetezi wa moja kwa moja kuwa hawakuhusika katika sakata hili kama ilivyotokea kwa Dk. David Mathayo na Balozi Hamis Kagasheki.
Baadhi ya Mawaziri waliotajwa kwa kutowajibika vyema ni pamoja Dk David Mathayo David (Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi),
Hawa Ghasia (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa-Tamisemi), Dk Kawambwa, Celina Kombani (Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma).
Hii inawafanya wadadisi wa mambo kujiuliza idadi ya Mawaziri wanaowajibika, nia yao na uwezo walio nao wa kutosha kumsaidia mteuzi wao kutekeleza majukumu waliyopewa.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment