DUNIA
haiishi vituko! Chacha Makenge (36) mzaliwa wa Kijiji cha Kisangula,
Mtukula, Serengeti mkoani Mara anaishi jijini Dar lakini ndani ya
handaki aliloligeuza chumba kwa miaka minne sasa, ni ajabu lakini ni
kweli.
Akizungumza na mwandishi wetu hivi karibuni nje ya handaki hilo
lililopo mita chache kutoka majengo ya biashara ya Mlimani City, Makenge
alisema alichukua uamuzi huo baada ya rafiki yake (jina linahifadhiwa)
kumchomea nyumba na kuteketeza samani zote.
“Ilikuwa mwaka 2009 mwanzoni rafiki yangu huyo ndiye alinipa sehemu
ya kiwanja chake nijenge nyumba. Nikawa naishi hapo huku nikiendelea na
shughuli zangu za kila siku.
“Siku moja akabadili mawazo, akanitaka nihame katika eneo lake bila kunipa sababu, nilimwomba anipe muda nitafute pa kwenda.
“Julai 2009 akaja na polisi, akanikamata na kunipeleka Kituo cha Polisi cha Stakishari, nilipowauliza kosa langu, hawakunieleza.
“Baada ya siku mbili majirani walikuja kuniona na kuniambia kwamba nyumba yangu imechomwa moto na kila kitu kilichokuwa ndani kimeteketea, aliyefanya hivyo ni rafiki yangu. Nilijisikia vibaya sana.
“Siku iliyofuata majirani walikuja tena kituoni wakaniwekea dhamana.
Nilipofika kwangu nilikuta majivu tu, iliniuma sana, nililia lakini
sikupata ufumbuzi. Kwa vile nilikuwa sina pa kwenda ilibidi niwe nalala
palepale nilipochomewa nyumba nikisaidiwa chakula na majirani.
“Siku iliyofuata, saa nne usiku nilivamiwa na watu wanne, wakiwa na
mapanga na marungu, nilipambana nao mpaka wakaondoka. Kesho yake
nilikwenda kwa mwenyekiti wetu wa serikali ya mtaa, Jumanne Malima
kumweleza yaliyonipata, alisikitika, akaniandikia barua kwenda Polisi
Stakishari.
“Nilipofika kituoni sikusikilizwa, badala yake walinikamata tena na
kuniweka ndani wakidai kwamba nimefunguliwa kesi ya kumjeruhi mtu kwa
panga. Hawakukubali niwekewe dhamana.
“Julai 31, 2009 nilifikishwa Mahakama ya Mwanzo Ukonga na baadaye
nilipelekwa Mahabusu ya Gereza la Keko, nikawa napelekwa mahakamani hadi
Septemba mwaka huo ambako nilihukumiwa kwenda jela miezi 9.
“Nilitumikia maisha ya jela hadi Desemba 10, 2009 nikatolewa kwa
msamaha wa Rais Jakaya Kikwete. Nilikwenda kuishi kwa ndugu zangu huku
wakifuatilia sababu ya kufanyiwa vitendo hivyo bila mafanikio.
“Maisha ya kwa ndugu hayakunifurahisha kwani hata wao walikuwa na
majukumu mengi, niliamua kuendelea na kazi zangu za sanaa pia utunzaji
wa mazingira na bustani kwa watu wakawa wananilipa fedha.
“Ndipo nilipoamua kutafuta sehemu iliyotulia ili niweze kuishi,
nikapata hapa, ni jirani na Mlimani City. Nilichimba handaki kubwa kama
unavyoliona, kwa chini kuna kitanda ninacholalia.
“Kwa hakika hapa sipati shida, wala kelele. Kwanza ni tulivu sana,
nimefikia hatua ya kuishi kama mnyama kutokana na mateso na bugudha
nilizopata, wengi hawajui nilipo, nipo katika pori hili kwa miaka minne
sasa,”alisema Makenge.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment