Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa akichangia hoja kwenye mjadala wa
kupitisha mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2014/15.
Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa amesema ana shaka kama
Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Result Now), utafanikiwa kutokana na
Kitengo cha Utekelezaji, Ufuatiliaji na Tathmini ya Miradi ya Maendeleo
kilicho chini ya Ofisi ya Rais (PDB) kukosa meno.
Akichangia mjadala wa hoja ya Mapendekezo ya
Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2014/2015, Lowassa alisema tatizo
kubwa linaloikabili nchi ni viongozi kushindwa kutekeleza mipango
mbalimbali ya maendeleo.
“Tatizo la nchi hii mnazungumza mambo mengi lakini
hakuna utekelezaji,” alisema Lowassa wakati akichangia mjadala huo
uliowasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu),
Stephen Wassira, wiki iliyopita.
Mbunge huyo wa Monduli (CCM), Lowassa ambaye pia
ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Mambo ya Nje alisema itakuwa vigumu kwa
PDB kutekeleza wajibu wake wakati hakina meno ya kusimamia utekelezaji
wa mipango ya Serikali.
Kitengo cha PDB kinachoongozwa na Omar Issa
kiliundwa mwaka huu na kutengewa kiasi cha Sh29 bilioni na kulalamikiwa
na Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika wakati wa kikao cha Bunge cha
Bajeti 2013/14.
Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa ni sehemu ya
jitihada za Serikali kuinua uchumi kutoka wa chini hadi kufikia wa kati
ifikapo mwaka 2025.
“Nataka mjiulize maswali machache. Je, hawa PDB wana meno?” alisema Lowassa na kuongeza:
“Tunazungumza lakini mjue kuwa `discipline’
(nidhamu) ya wenzetu wa Malaysia ni tofauti na hapa kwetu. Hapa kuna
uswahili mwingi wa kukaa bila kutekeleza mambo, mnaamua bila
kutekeleza.” Huku akishangiliwa na baadhi ya wabunge, Lowassa aliitaka
Serikali kuwa na mipango michache ambayo itaweza kuifuatilia kwa
ukaribu na kuitekeleza. Alipendekeza kuwa ajira, elimu na kuendeleza
reli kuwa vipaumbele muhimu.
“Kinatakiwa chombo ambacho kinaweza kufanya uamuzi
mgumu unaotekelezeka kwelikweli. Bila kuwavika joho la kufanya uamuzi
ili kuwarahisishia utekelezaji wa kazi yao na wakawa na ‘function’
itakuwa ni kazi bure. Ni uamuzi mzuri kuanzisha mpango huu lakini
msipoangalia itakuwa kazi bure. Lazima wawe na meno ya kuuma
mkishakubaliana mambo yafanyike.”
Kila mtu analalamika
Lowassa alisema sasa Tanzania imekuwa nchi ya kila mtu kulalamika, kuanzia viongozi hadi wananchi.
“Wananchi na viongozi wote wanalalamika
haiwezekani kukawa na jamii ya aina hii, lazima awepo mtu mmoja
anayefanya uamuzi na anayechukua hatua. Bila kuchukua hatua tutaendelea
kulalamikiana tu” alisema.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Mpango wa Matokeo Makubwa uliingizwa nchini kwa kurudufiwa
kutoka Malaysia, ambayo ilipopata uhuru mwaka 1957 ilikuwa katika
kiwango sawa na Tanzania katika maendeleo ya kiuchumi lakini sasa ina
rekodi ya juu kiuchumi barani Asia. Mpango huu pia unatekelezwa Nigeria
na Rwanda na umeonyesha mafanikio makubwa katika nchi hizo.
Katika kutekeleza mpango huo, Serikali imeanza na
wizara sita; Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Kilimo, Chakula na Ushirika,
Maji, Uchukuzi, Fedha na Nishati na Madini.
Ajira
Akizungumzia suala la elimu, Lowassa alisema:
“Huwezi kuzungumza mipango bila kuzungumza ajira, kuna Watanzania wengi
waliomaliza darasa la saba, kidato cha nne na sita wapo mitaani na
hawana ajira. Tusipoangalia watakuja kula sahani moja na sisi.”
Alisema katika mkutano wa Benki ya Dunia (WB) na
Shirika la Fedha Duniani (IMF) mwaka huu, walizungumzia mdororo wa
uchumi kwa nchi za Ulaya na moja ya nchi hizo ambayo ni Hispania,
ilieleza jinsi ilivyoweza kujinasua kwa kuweka kipaumbele cha ajira.
“Hispania walitoa mfano kuwa walikuwa na ukosefu
wa ajira kwa asilimia 50, waliamua katika bajeti yao kujikita katika
kuzalisha ajira. Kila mwekezaji aliyekwenda katika nchi hiyo alipewa
masharti ya kuwekeza katika ajira ya vijana. Kimsingi tunatakiwa kuwa na
takwimu za kujua tumezalisha ajira ngapi ndipo tutajua uchumi wetu
unakua kwa kiasi gani,” alisema.
Lowassa alisema baada ya miaka mitatu nchi hiyo
imetoka kuwa miongoni mwa nchi zisizo na ajira na kusisitiza kuwa
mipango mingine ni migumu kutekelezeka kama nchi haitakuwa na ajira.
Alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Fatma Mwasa na
Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Elibariki Kingu kutokana na kitendo chao cha
kuwapa ajira wanafunzi waliohitimu vyuo vikuu baada ya kuwapatia
matrekta na mashamba.
Elimu
Lowassa alisema kuna tatizo la msingi katika elimu
ya Tanzania. “Nilitegemea wahusika wangepata taarifa ya Tume ya
Serikali kuchunguza kushuka kwa kiwango cha elimu ili kujua matatizo
yaliyopo katika elimu na nini cha kufanya.”
Mwanzoni mwa mwaka huu Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliunda tume
ya watu 15 kuchunguza sababu za idadi kubwa ya wanafunzi wa kidato cha
nne kuvurunda katika matokeo ya mtihani huo mwaka 2012.
Tume hiyo tayari imeshakamilisha kazi na kukabidhi ripoti hiyo serikalini, lakini mpaka sasa bado haijawekwa hadharani.
“Haitoshi kumchukua mwanafunzi aliyemaliza chuo
kikuu wakati akienda katika soko la ajira wakati shahada yake haimsaidii,
mtu ana shahada lakini kazi hakuna.”
“... Kunatakiwa kufanyika mjadala nchi nzima
kuzungumza juu ya matatizo na nini kifanyike. Nchi isipokuwa makini
katika hili itaachwa katika ushindani uliopo sasa kwenye Jumuiya ya
Afrika Mashariki (EAC) na nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya
Kusini mwa Afrika (SADC).”
Awafagilia Magufuli, Mwakyembe
Akizungumzia uendelezaji wa Reli ya Kati alisema
pamoja na juhudi zinazofanywa na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli
kujenga barabara, alisema zinaharibika kwa kasi kutokana na kuzidi kwa
kiwango cha uzito wa malori.
“Reli ya Kati inatakiwa kuangaliwa kwa haraka
maana malori yanayotembea katika barabara yatapungua kwa kuwa mizigo
itakuwa inachukuliwa na treni,” alisema. Licha ya kusifu kazi
inayofanywa na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe Lowassa alisema
foleni jijini Dar es Salaam zinashusha uzalishaji, kwani watu wengi
wanatumia muda mwingi barabarani kuliko kufanya shughuli za maendeleo.
“Serikali haiwezi kukaa hivi hivi, ‘this is a
disaster’ (hili ni janga), mtafute njia ya kuangalia mnafanyaje kumaliza
foleni ya Dar es Salaam, jambo hili lifanyike sasa,” alisema.
Uamuzi mgumu
Lowassa alisema pia Tanzania haitakiwi kuendelea
kulumbana na Uganda, Rwanda na Kenya zinazotaka kuitenga katika Jumuiya
ya Afrika Mashariki (EAC), badala yake ichukue uamuzi mgumu wa
kushirikiana na nchi nyingine.
“Wao wameamua kuanzisha ushirikiano na Sudan
Kusini, Tanzania inaweza kuanzisha ushirikiano na Jamhuri ya
Kidemokrasia Kongo (DRC) ambako ni kuzuri zaidi na kikubwa kinachotakiwa
kufanyika ni kuifufua Reli ya Kati,” alisema.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment