Mwili wa marehemu Omary Mkumbo huyo ukitolewa tayari kupelekwa chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa
MWANAFUNZI wa kituo cha masomo cha The Dream Centre
aliyetarajiwa kufanya mtihani wa Kidato cha Nne ulioanza jana,
Omary Mkumbo (25) mkazi wa Mwangata ‘C’ mjini Iringa amejiua kwa
kujinyonga akihofia kufeli mtihani.
Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Ramadhani Mungi, aliwaambia
waandishi wa habari jana kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 3, mwaka huu,
saa 2:45 huku akiacha ujumbe chumbani kwake ukisomeka: “Buriani
nimechoka kufeli mtihani.”
Kwa mujibu wa kamanda, katika barua hiyo ndefu aliyoiandika kijana
huyo alisema kuwa amefanya hivyo si kwa kupenda bali amechukizwa na
hatua ya kufeli mara kwa mara mitihani anayofanya, hivyo kuamua kujiua
ili kuepuka aibu katika mtihani ujao.
Alisema kijana huyo aliyekuwa akiishi na kaka yake pamoja na mdogo
wake, kabla ya kujinyonga alimtuma mdogo wake dukani na kisha yeye
kujifungia chumbani baada ya kuona hakuna mtu ndani ya nyumba.
Mungi aliongeza kuwa marehemu alikuwa alitumia muda wake mwingi
kujisomea kwa kujiandaa na mtihani huo, pia alikuwa ni mtu wa kusali
wakati wote.
Shangazi wa marehemu, Betha Nzogu (60), alisema mtoto wake huyo
alitarajiwa kuanza mitihani jana ikiwa ni mara ya nne tangu alipohitimu
kidato cha nne ambapo mara zote alifeli lakini hakuonyesha kukata
tamaa.
Alisema kabla ya marehemu kuchukua uamuzi huo alimsaidia kuchinja kuku
ambao yeye huwandaa na kuuza na kwamba hata baada ya kumaliza
kazi hiyo alirudi nyumbani kwake na kuanza kufua nguo.
Nzogu alisema baadaye akiwa hajui chochote, alikata sehemu ya kamba na kwenda kuifunga chumbani kwake na kuitumia kujinyonga.
“Ninasikitika sana kwani hakuna alichotuambia kuhusu mtihani huo,
alifanya mtihani mwaka juzi akafeli, akarudia mwaka jana akafeli na sasa
alitarajia kufanya kwa mara ya tatu,” alisema.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mwangata ‘C’, Salehe Mgimwa alithibitisha kujinyonga kwa kijana huyo.
0 comments:
Post a Comment