Zitto Kabwe
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), Zitto Kabwe amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania analipwa sh milioni 384 kwa mwaka, sawa na sh milioni 32 kwa
mwezi pasipo kukatwa kodi.
Hii ni mara ya pili kwa Zitto kutangaza hadharani mishahara ya
viongozi wakuu wa serikali, akiwa ameanza na ule wa Waziri Mkuu,
aliyesema analipwa takribani sh milioni 26 kwa mwezi.
Akiwahutubia wananchi mjini Igunga jana, ukiwa ni mwendelezo wa ziara
yake ya kuimarisha chama Kanda ya Magharibi, Zitto ambaye pia ni mbunge
wa Kigoma Kaskazini alisema kuwa sababu ya kutaka mishahara ya viongozi
wakuu wa nchi ijulikane, ni kuzuia mianya ya watu wachache kuiibia nchi
kutokana na usiri wa jambo hilo.
Zitto alisema hoja ya msingi si kiasi wanacholipwa viongozi hao
walioajiriwa na wananchi, bali ni usiri unaofanywa juu ya kiwango hicho
jambo alilosema kuwa linaweza kutumiwa na wajanja kuendelea kuinyonya
nchi.
Alisema ni jambo la kusikitisha kuona mwalimu anayelipwa mshahara wa
sh 220,000 kwa mwezi akikatwa kodi, huku viongozi wa kuchaguliwa wakiwa
wanapokea mishahara mikubwa pasipo kukatwa kodi licha ya kuhudumiwa kila
kitu na serikali.
Aliongeza kuwa katiba ya sasa Ibara ya 43(1), inaeleza kuwa rais
atalipwa mshahara pamoja na malipo mengine, huku ibara hiyo hiyo kifungu
cha pili ikizuia mshahara na marupurupu kupunguzwa, hali aliyoelezea
kuwa ni muhimu katiba mpya ikabadilisha sheria hizo kwa manufaa ya nchi.
“Kwa hiyo hata kesho kama Dk. Willibrod Slaa akiwa rais na akataka
kupunguza mshahara wake, kwa katiba hii hawezi na hili jambo si sahihi
kwani viongozi wa ngazi hizi wanapata kila kitu bure kutoka serikalini,”
alisema Zitto.
Akiwa katika Kata ya Choma, Zitto alikagua kilichokuwa kiwanda cha
kuchambulia pamba cha Giner ambacho kimeacha kufanya kazi tangu mwaka
1998.
Alisema kufa kwa viwanda vingi vya uzalishaji nchini kumechangiwa kwa
kiasi kikubwa na Serikali ya Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin
Mkapa, akidai kuwa alishindwa kutofautisha suala la uwekezaji na
biashara huru.
“Ni serikali ya Mkapa ndiyo ilitufikisha hapa katika kupotea kwa
viwanda nchini, wao walidhani biashara huru ni kuwapa wawekezaji viwanda
vyetu na serikali kujiweka pembeni, sasa nchi imebaki kutegemea uchumi
wa uchuuzi badala ya uzalishaji,” alisema.
Alisema sera ya uwekezaji katika Serikali ya CCM ilichukuliwa kama
fursa ya viongozi wa chama hicho kujinufaisha na mali za serikali pasipo
kujua wataendeleza vipi.
Zitto alisisitiza kuwa kila mara CHADEMA imekuwa ikisisitiza bungeni
juu ya kupiga marufuku usafirishaji wa pamba kwenda nje kama malighafi,
na badala yake wakitaka viwanda vifufuliwe kwa ajili ya kutoa ajira kwa
Watanzania.
Alirejea kusisitiza sera ya hifadhi ya jamii kwa wakulima akisema
imefikia wakati serikali kupitia SSRA ione umuhimu na ulazima wa
kuhakikisha wanaongeza Watanzania wenye hifadhi ya jamii kwa kuanza
mfumo maalumu wa hifadhi ya jamii kwa wakulima (Supplementary scheme for
social security to small holder farmers).
“Ninapendekeza serikali ichangie nusu kwa nusu na mkulima ili kuvutia
uwekaji akiba katika nchi na kuwa na sera ya uwekezaji katika maeneo
yatakayomwinua mkulima kama miundombinu ya umwagiliaji, mikopo nafuu kwa
wakulima kwenye pembejeo na nyumba na bima ya afya.
“Nimezungumzia umuhimu wa uwazi katika matumizi ya fedha za umma
ikiwemo malipo ya watumishi na viongozi wa umma. Nimewaeleza wananchi wa
Nzega kuwa siku ya Jumanne kamati yangu ya Hesabu za Serikali (PAC)
itaanza kukagua mahesabu ya vyama vya siasa nchini,” alisema.
Zitto alisema vyama vya siasa vinatumia fedha za umma takribani sh
bilioni 20 kila mwaka kama ruzuku, kwamba ni haki ya wananchi kujua
fedha zinatumika namna gani.
Alisema kuwa wananchi wa Nzega wana changamoto nyingi sana. Kwamba
wakulima wa pamba walipewa madawa feki ya kuua wadudu, michango ya hovyo
hovyo ni mingi mno na unyanyasi wa wana-CHADEMA ni mkubwa vijijini.
0 comments:
Post a Comment