Na Gideon Mwakanosya Songea
Watu wawili wamepoteza maisha kwa nyakati tofauti mkoani Ruvuma ambapo tukio la kwanza linamhusisha mwanamke mmoja na la pili ni la mwanafunzi kuuawa na mwanafunzi mwenzake.
Katika tukio la kwanza, mwanamke mmoja Agatha Honde (55)
mkazi wa mtaa wa Nonganonga kata ya Mletele katika Halmashauri ya Manispaa ya
Songea Mkoani Ruvuma ameuawa kwa kukatwakatwa sehemu mbalimbali za mwili hasa
kichwani na mme wa shangazi yake kwa tuhuma za wivu wa kimapenzi.
Habari zilizopatikana jana mchana
mjini Songea ambazo zimethibitishwa na kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma
Deusdedit Nsimek zimesema kuwa tukio hilo limetokea juzi majira ya kati ya saa
3.30 na 4.00 asubuhi huko katika mtaa wa Nonganonga nje kidogo ya manispaa ya
Songea.
Kamanda Nsimek alifafanua kuwa
inadaiwa siku ya tukio huko katika kata ya Mletele mtaa wa Nonganonga Agatha
Honde (55) aliuawa kwa kukatwakatwa sehemu mbalimbali za mwili na kusababisha
kifo chake hapohapo na Dickson Mahundi ambaye baada ya kufanya tukio hilo alikimbia na kutokomea kusikojulikana na
polisi inaendelea kumsaka.
Alieleza zaidi kuwa katika tukio
hilo pia Mahundi alimjeruhi Agatha Honde (22) ambaye ni mke wake kwa
kumkatakata na upanga kichwani na kusababisha atokwe na damu nyini kichwani hadi
kupoteza fahamu na kwamba kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Serikali ya
Mkoa Songea (HOSO) ambako anaendelea kupata matibabu na hali yake bado sio
nzuri.
Aliongeza kuwa kulingana na
upelelezi wa wali wa polisi umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni kulipa
kisasi ambapo inadaiwa kuwa Mahundi mwaka uliopita alimchumbia Agatha na kumuoa
ambaye kwa kipindi cha mwaka mzima alikuwa anaishi naye na kwamba kabla
hajamuoa, Agatha alikuwa akiishi na shangazi yake Agatha Honde(55) ambaye
alikuwa mlezi wake.
Kabla wanandoa hao hawajaoana
Mahundi inadaiwa kuwa alificha tatizo alilokuwa nalo la kutokuwa na nguvu za kiume
ambalo lilimfanya ashindwe kufanya tendo la ndoa na mke wake kwa kipindi chote
jambo ambalo mke wake alilazimika kwenda kutoa siri hiyo kwa shangazi yake.
Kamanda Msimek alisema kuwa Agatha
hivi karibuni aliamua kutoroka kwenda kwa shangazi yake na kumweleza bayana
tatizo la mme wake ambapo shangazi yake alipoelezwa aliamua kuwajulisha wazazi wa
Agatha na baadaye kiliitishwa kikao cha familia cha pande zote mbili, kwa
mwanaumme na mwanamke, ambacho baada ya kulisikiliza tatizo hilo na kuliona
kuwa ni gumu kiliazimia kumtafutia tiba asilia Mahundi jambo lililomfanya
Agatha abaki nyumbani kwa shangazi yake wakati akisubiri tiba ya asili ya
mmewe.
Alisema kuwa juzi majira ya saa 3
asubuhi Mahundi aliamua kuchukua upanga na kumfuata mkewe nyumbani kwa shangazi
yake ambako alikuwa akiishi na alipofika alikuta nyumba imefungwa milango yote
ambapo majirani walimweleza kuwa wamekwenda shambani kuchimba mihogo jambo
lililomlazimu kwenda kuwafuata ambako aliwakuta kisha alianza kuwashambulia kwa
kuwakatakata na upanga na inadaiwa shangazi wa mke wake ndiye aliyeanza kupata
kipigo na kufa papo hapo na baadaye alianza kumpa kipigo mke wake
kilichomsababishia majeraha makubwa mwilini.
Hata hivyo Kamanda Msimek alisema
kuwa Polisi inaendelea kumsaka mtuhumiwa ambaye anadaiwa kuwa amekimbilia mkoa
wa jirani na kwamba akipatikana atafikishwa mahakamani atafikishwa mahakamani
kujibu mashtaka yanayomkabali.
Mganga mfawidhi wa hospitali ya
serikali ya Mkoa Dk. Benedict Ngaiza alipoulizwa na Nipashe kwa njia ya simu
amethibitisha kuwepo kwa majeruhi Agatha Honde (22) ambaye amelazwa katika wodi
ya majeruhi akiwa anaendelea kupata matibabu na hali yake bado sio nzuri wakati
maiti moja ya tukio hilo ipo katika chumba cha kuhifadhia maiti ikisubiri
kuchukuliwa na ndugu wa marehemu.
Mwanafunzi auawa
Katika tukio lingine mwanafunzi mmoja wa shule ya msingi
Mwenge iliyopo katika kijiji cha Mtina Wilaya ya Tunduru Mkoa wa Ruvuma
amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu kwenye kituo cha afya kijijini hapo
baada ya kujeruhiwa vibaya kichwani kwa kupigwa na mchi na mwanafunzi mwenzake
Yasin Maya(13).
Akizungumza na mwandishi wa habari hii jana
mchana ofisini kwake kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma Deusdedit Msimek
amemtaja aliyefariki dunia kuwa ni Mohamed Yahaya (15) ambaye inadaiwa kuwa
Oktoba 12 mwaka huu majira ya saa 3.30 asubuhi huko katika kitongoji cha Mwenge
kilichopo kata ya Mtina Mohamed alifariki dunia wakati anapelekwa kutibiwa.
Alisema kuwa inadaiwa siku hiyo
ya tukio Mohamed alijeruhiwa kichwani kwa kupigwa na mchi kufuatia kuwepo
ugomvi mkubwa kati yake na Yasin Maya ambaye ni mwanafunzi mwenzake wa shule ya
msingi ya Mwenge ambapo alifafanua kuwa ugomvi huo ulifanyika nje ya eneo la
shule hiyo ambapo Mohamed akiwa darasa la sita alikuwa na tabia ya utoro na
Yasin Maya ni mwanafunzi wa darasa la tano katika shule hiyo.
Hata hivyo, kamanda Msimek
alisema kuwa mtuhumiwa Yasin Maya amekamatwa na polisi na upelelezi kuhusiana
na tukio hilo unaendelea ili kubaini chanzo cha tukio hilo.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment