Marais wa Sudan na Sudan Kusini wamekubaliana kubuni
mikakati ya kusuluhisha maswala yote yanayotatiza uhusiano wa pande hizo
mbili.
Viongozi hao walikutana leo wakati wa mkutano wa faragha katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba.
Aidha vingozi wa kamati sita
wakiwemo, mawaziri kutoka nchi hizo mbili pia walikutana wakati wa
mkutano hio na kujadili maswala kuhusu nchi hizo mbili.
Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir Mayardit
alielezea furaha yake kwa kufikia makubaliano ya pande hizo mbili
akisema kuwa serikali yake itajitolea kuhakikisha kuwa makubaliano hayo
yatatekelezwa.
Kwa upande wake Rais Umar al-Bashir alisema kuwa
mkutano ulifanikiwa na kuongeza kuwa serikali yake itajitolea
kuhakikisha kuwa makubaliano waliyoafikia yanatekelezwa.
Marais hao walifanya mkutano wa faragha muda
mfupi baada ya Bashir kuwasili na wajumbe wake wa Sudan katika Ikulu ya
Rais mjini Juba.
Kwa mujibu wa shirika la habari la SUNA, baadhi
ya masuala yaliyojadiliwa kwenye mkutano huo ni mambo tete kuhusu
Abyei, usalama pamoja na kutekelezwa kwa makubaliano ya ushirikiano kati
ya nchi hizo mbili.
Mnamo siku ya Jumatatu, waziri wa mambo ya nje
wa Sudan Kusini Barnaba Marial Benjamin, aliambia kituo cha redio cha
Sudan CRN kuwa marais hao wawili watazungumzia mgogoro wa Abyei katika
kutaka kuboresha uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Kuhusu swala la kura ya maoni kuhusu Abyei ,
waziri alisema kuwa Muungano wa Afrika hauruhusu uamuzi wa pande moja
kuhusu kura ya maoni.
Aliongeza kuwa Kura ya maoni lazima iruhusiwe na nchi hizo mbili na kuidhinishwa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.
Aidha alisema kuwa sudan Kusini inashurutishwa
na makubaliano ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili na kwa hivyo
haiwezi kuunga mkono kura ya maoni inayoshinikizwa na upande mmoja.
Hata hivyo alisema anaelewa kwa nini jamii ya
Abyei iliamua kupiga kura ya maoni kujitenga na ni kwa sababu ya masaibu
waliyoyapitia.
Alisisitiza kuwa Muungano wa Afrika na Sudan
lazima ziisikilize jamii ya Abyei na kukubaliana kuhusu tarehe ya
kufanyika kwa kura ya maoni kuhusu kutaka kujitawala wenyewe.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment