Viongozi wa vyama vya Siasa,(kushoto)Isaack Cheyo(UDP), Nancy
Mrikaria (TLP), Fahmi Nassoro Dovutwa (UPDP), James Mbatia
NCCR-Mageuzi, Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), Philip Mangula (CCM) na Dk
Willibrod Slaa (Chadema) wakiwa wameshikana mikono baada ya kikao cha
pamoja jijini Dar es Salaam jana.
Serikali inatarajia kuandaa hati ya dharura ili kuwezesha
kufanyika kwa maboresho ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya
Mabadiliko ya Katiba ambayo yatajadiliwa upya katika Mkutano wa Bunge
unaoanza Oktoba 29 mjini Dodoma.
Tayari vyama vya upinzani na chama tawala
vimekubaliana taratibu muhimu za kufuata ili maboresho hayo yaweze
kupita ndani ya Bunge. Muswada huo haukuwa umepangwa kujadiliwa katika
mkutano ujao wa Bunge ndio maana itabidi iombwe hati hiyo ya dharura.
Hatua hiyo ni ushindi kwa vyama vitatu vya upinzani vya Chadema, CUF na
NCCR- Mageuzi, ambavyo vilipinga muswada huo wakati wa mkutano uliopita
wa Bunge Septemba, mwaka huu.
Muswada wa sheria hiyo uliopitishwa Septemba na
Bunge ulisusiwa na wabunge wa vyama hivyo wa upinzani kwa maelezo kuwa
una kasoro kwenye baadhi ya vipengele.
Hata hivyo, wabunge wa CCM waliamua kuendelea na
mjadala na kupitisha muswada huo kitendo ambacho kilisababisha mvutano
mkubwa uliomfanya Rais Jakaya Kikwete kukutana na viongozi wa vyama vya
siasa vyenye wabunge kumaliza tofauti zao.
Mbatia asoma tamko la vyama
Akisoma tamko la vyama vya siasa mbele ya
waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia
alisema hatua ya Serikali itakuja baada ya vyama vya siasa kufikia
mwafaka wa vipengele vinavyotakiwa kufanyiwa marekebisho kwenye muswada
huo.
Mbatia alisema kuwa tayari kazi hiyo imefanyika na mapendekezo yao yameshapelekwa serikalini ingawa hakutaka kuingia kwa undani walichopendekeza katika marekebisho hayo.
Mbatia alisema kuwa tayari kazi hiyo imefanyika na mapendekezo yao yameshapelekwa serikalini ingawa hakutaka kuingia kwa undani walichopendekeza katika marekebisho hayo.
Vyama vilivyokutana ni pamoja na CCM, Chadema,
CUF, NCCR -Mageuzi, TLP. Pia vyama vya UDP na UPDP vilishiriki kwa niaba
ya vyama visivyo na wabunge.
Mbatia alisema hatua inayofuata ni vyama kuunda
kamati yao na Serikali kuunda yake ili kukubaliana kwa pamoja maeneo
muhimu ya marekebisho.
Alisema lengo la hatua hiyo ni kuufanya mchakato wa Katiba kuwa shirikishi baada ya kamati hizo kumaliza kazi yake.
“Baada ya hapo, Serikali itaandaa hati ya dharura
ili marekebisho yapelekwe haraka katika Mkutano wa Bunge unaoanza Oktoba
29, “aliongeza Mbatia.
Mbatia alisema wanataka kabla ya Bunge la Katiba
halijaanza basi sheria husika ifanyiwe marekebisho. “Tunawaomba
Watanzania hasa wabunge waunge mkono juhudi hizi za vyama na Serikali
ili kuhakikisha mchakato wa Katiba Mpya unakuwa shirikishi. Wabunge
waridhie marekebisho haya na kuyapitisha,” alisema mbunge huyo wa
kuteuliwa na Rais.
JK awapa goli wapinzani
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
CCM, ambayo wabunge wake walipitisha muswada kwa
kauli moja, iliweka kando tofauti zake za kiitikadi na kimtizamo na
kuungana na Chadema, CUF, NCCR- Mageuzi na vyama vingine vya upinzani.
Kitendo hicho cha CCM kilikuja baada ya Rais
Kikwete kukutana na viongozi wa vyama vya siasa vyenye wabunge na vile
visivyokuwa na wabunge, wiki iliyopita na kuvitaka vyama hivyo kukaa
pamoja na kutoa mapendekezo ili yafanyiwe kazi na Serikali.
Kitendo hicho ni sawa na ushindi wa vyama vya
upinzani kwani pamoja na kuwa wabunge wachache tofauti na CCM bado Rais
Kikwete aliamua kusikiliza hoja zao.
CCM na Chadema damu damu
Katika hatua ya kuashiria kuwa vyama hivyo viko
bega kwa bega, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangula na Katibu Mkuu
wa Chadema, Dk Willibrod Slaa walishikana mikono pamoja na viongozi
wengine watano wa vyama vya siasa na kutoa tamko la pamoja kuhusu
kuboresha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Tukio hilo la aina yake lilifanyika jana na
kuongozwa na Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia
Tanzania ambacho kilipewa jukumu na Rais kuratibu ukusanyaji wa maoni ya
maboresho ya muswada huo.
Mangula alipoulizwa kama wabunge wa CCM watakuwa
tayari kupitisha maboresho ya sheria hiyo itakaporejeshwa tena bungeni
alisema kwa kifupi; “Siwezi kuwasemea wabunge wa CCM.”
Alipobanwa zaidi kuhusu ushiriki wa CCM kwenye
umoja wa vyama hivyo. Alisema: “CCM haijawahi kuandaa rasimu yake ya
Katiba, ila nachojua ni kwamba kila chama kilipewa nafasi na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba kutoa maoni yake na CCM ni miongoni mwa vyama
hivyo. Katiba Mpya ni kitu kizuri kwa taifa letu.”
Serikali yakubali ombi la tume
Serikali imekubali ombi la Tume ya Mabadiliko ya
Katiba la kuongezewa muda wa mwezi mmoja kutokana na ugumu wa kazi ya
uchambuzi wa maoni yaliyotolewa na wananchi na asasi mbalimbali.
Habari zilizopatikana kutoka vyanzo vya habari
ndani ya Serikali na kuthibitishwa na Waziri wa Katiba na Sheria,
Mathias Chikawe zilisema kuwa awali kabla ya kuomba muda huo, tume hiyo
ilikutana na Rais Kikwete ili kuomba kuongezewa muda.
Maana yake ni kuwa Tume hiyo iliyoanza kazi Mei
Mosi, mwaka jana ilitakiwa kukamilisha kazi yake Novemba Mosi, mwaka huu
hivyo sasa kazi yake itakamilika Desemba. Akizungumza na gazeti hili
ofisini kwake jana, Chikawe alisema, “ Kwa nini wakataliwe kama wanaona
muda hauwatoshi.” Kwa mujibu wa Waziri Chikawe, muda waliomba
unakubalika kisheria na kwamba wanaweza kuongezewa hadi miezi miwili.
Alipoulizwa kama haoni muda huo utasababisha kuchelewesha
mchakato mzima wa Katiba, Waziri Chikawe alisema, haoni kama kuongezwa
kwa muda huo kutaathiri chochote.
“Nataka kuwahakikishia Watanzania hakuna haja ya kuwa na wasiwasi mchakato utaendelea kama kawaida kitakachoongezeka ni mwezi mmoja hivyo badala ya rasimu ya pili kukabidhiwa kwa Rais Novemba sasa itaenda mpaka Desemba,”alisema Waziri Chikawe.
Mwananchi
“Nataka kuwahakikishia Watanzania hakuna haja ya kuwa na wasiwasi mchakato utaendelea kama kawaida kitakachoongezeka ni mwezi mmoja hivyo badala ya rasimu ya pili kukabidhiwa kwa Rais Novemba sasa itaenda mpaka Desemba,”alisema Waziri Chikawe.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment