Ofisi imefungwa kwa kukosa fedha
Serikali ya Marekani imeamkia Jumanne kwa pigo kubwa la kufunga baadhi ya ofisi za umma kutokana na ukosefu wa fedha za kuziendeshea.

Hili limetokana na kukosekana maafikiano kati ya mabunge mawili ya congress juu ya bajeti mpya.

Bunge la uwakilishi lililo na idadi kubwa zaidi ya wanachama wa Republican limesisitiza kuchelewesha mpango wa rais Obama wa kutoa huduma ya afya ijulikanayo kama Obama- care kama moja wapo ya vigezo kabla ya kupitisha mswada.

Wabunge wa Republican katika bunge la wawakilishi wakishirikiana na Maseneta wao wanashinikiza sheria hiyo iondolewe au mpango huo usipewe fedha za kuusimamia kama moja ya masharti ya kuendelea kuipatia fedha serikali.

Sehemu kubwa za sheria hiyo aliyopitiwa mwaka 2010 imepewa uhalali na mahakama kuu ya Marekani, itaanza kutumika rasmi Jumanne.

Zaidi ya wafanyikazi wa umma laki nane wanatishiwa kutumwa likizo ya lazima bila malipo tena bila hakikisho ya kulipwa pindi suala hili litakapotatuliwa.

Hii ni mara ya kwanza serikali hiyo kulazimika kuchukua hatua kama hii katika miaka 17.

Ofisi inayosimamia bajeti ya ikulu ilitoa taarifa kwa mashirika ya serikali kuanza kufunga ofisi zao kwa mpangilio, muda mfupi kabla ya kugonga saa sita usiku.

Obama aghadhabishwa

Rais Barack Obama aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, ''Wamefanya hivyo. Kundi la wanachama wa Republican wamelazimisha kufunga ofisi za serikali kwasababu ya kupinga tu Obama- care, badala ya kuidhinisha bajeti ya ukweli.''

Tayari inadaiwa dola imeshuka.
Watafiti wanasema kuwa makisio yanaonesha kuwa iwapo tatizo hili litaendelea kwa zaidi ya wiki tatu, na ofisi hizi kufungwa zaidi ya asili mia 0.9% ya pato la Marekani itapotezwa.

Mwandishi wa BBC mjini Washington Mark Mardell anasema kuwa mgawanyiko wa kisiasa nchini Marekani ni mbaya sana kiasi kuwa serikali inashindwa kutekeleza majukumu yake.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top