MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Arusha ambaye amesimamishwa uongozi kwa tuhuma za usaliti, Samson Mwigamba, amesema kuwa hakupigana na Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe, kama ilivyodaiwa na baadhi ya magazeti.

Mwigamba alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa kuelezea kile kilichojiri mwishoni mwa wiki hadi akapigwa na baadhi ya wajumbe wa kikao, wakimtuhumu kwamba aliandika taarifa za uongo kwenye mtandao wa kijamii wa Jamii Forums akizungumzia masuala ya uongozi ndani ya chama.

Mwigamba alisema kuwa hata wakati akivutana na walinzi wa chama Mbowe hakuwa ndani ya chumba cha mkutano, hivyo akadai kuwa anashangazwa na wale waliosambaza taarifa hizo kwamba alipigana na kiongozi huyo ambaye pia ni Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Aliwataja wale aliodai walimpiga kuwa ni Katibu wa Bavicha Wilaya ya Arusha, Noel OLovaroya, walinzi wa chama pamoja na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, kwamba alijaribu bila mafanikio kumpiga na kitofali ambapo alikikwepa kwa kujiangusha chini na kujigonga kisogoni.

“Wakati vurugu zikianza Mbowe hakuwa ukumbini, nilimuona akija Lema na Olevaroya, ambapo Lema alishikwa kabla hajanifikia huku Olevaroya akiruka juu ya meza na kuja kunipiga ngumi, mimi kwa kujitetea ilibidi nimpige ngumi kabla hatujaamuliwa,” alisema.

Mwigamba alimtuhumu Lema kuwa amekuwa akimtishia kumuua kwa kipindi kirefu, ambapo siku ya tukio alirudia kauli hiyo kabla hajaenda kuchukua kitofali na kujaribu kumpiga nacho ambapo alikikwepa.

Alisema kuwa tayari alishatoa taarifa polisi na kupewa kumbukumbu: AR/RB/1759/2013 aliyoifungua Februari 12, mwaka huu, baada ya kuwa anapokea vitisho vya kuuawa kutoka kwa Lema kupitia simu yake ya kiganjani.

Kuhusu kusimamishwa uongozi, Mwigamba alisema kuwa ametii licha ya kuwa kikao kilichomsimamisha hakina mamlaka kisheria, huku akiweka wazi kuwa hayuko tayari kukihama chama hicho, kwani bado anaamini ndicho chenye uwezo wa kuleta mabadiliko nchini.

Hata hivyo, tuhuma za Mwigamba zilikanushwa na Katibu wa CHADEMA wa mkoa, Amani Golugwa, akisema ni uongo dhidi ya Lema, kwani kwenye taarifa yake aliyowasilisha juzi kwenye kikao cha uongozi wa kanda alimsifu mbunge huyo kwamba ameongoza harakati mbalimbali za ujenzi wa chama kwa mafanikio makubwa, zikiwamo kampeni za ushindi wa kata nne zilizofanya uchaguzi mdogo hivi karibuni.

“Kwa kipindi chote ambacho amekuwa hayuko kazini Lema amekuwa akimsaidia hata kukamilisha ujenzi wa nyumba yake maeneo ya Sokon 1, hata anavyokwenda kwenye kesi zake Dar es Salaam ni Lema amekuwa akimsaidia gharama.

“Hicho alichokizungumza kwenye mkutano wake juu ya malalamiko ndiyo anatudhihirishia kuwa amekuwa nyoka na mnafiki ndani ya kundi letu,” alifafanua katibu huyo huku akisema hakuna malalamiko yoyote juu ya suala hilo ndani ya chama.

Golugwa aliongeza kuwa baada ya kupitia kompyuta ya Mwigamba wamebaini mambo mengi machafu na ya hatari kwa mustakabali wa chama ambayo yanawagusa watu wengi.

Hata hivyo hakutaka kuingia kwa undani wala kuyafafanua akisema yatakisaidia chama katika uchunguzi wake zaidi, na kwamba tayari kikao cha Baraza la mkoa kimeshakaa na kimemwandikia Mwigamba barua ya ajieleze ni kwa nini asivuliwe uongozi ikiwa ni sehemu ya mchakato wa kulifikisha suala hilo mbele ya kikao cha Kamati Kuu ya Taifa.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top