KADA mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye ni muasisi wa
kundi la wabunge waliokuwa wakishinikiza hoja ya Serikali ya Tanganyika,
maarufu kama G55, Njelu Kasaka, ameibuka na kuwashangaa wabunge wa
chama hicho kupinga hoja ya muundo wa serikali tatu wakati ni yao tangu
awali ya kudai mabadiliko ya muundo wa Muungano.
Kasaka aliongeza kuwa hata Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius
Nyerere, aliona umuhimu wa muundo huo wa serikali tatu, isipokuwa alitoa
tahadhari kuwa kwa aina ya uendeshaji wa serikali uliokuwa unaendekezwa
kwa kuogopana na kulindana Muungano usingedumu.
Mwanasiasa huyo ambaye amewahi kuwa mbunge wa Lupa, alitoa kauli hiyo
jana katika mahojiano maalumu na gazeti hili jijini Dar es Salaam, huku
akiwaasa wabunge hasa wa CCM kuacha mzaha katika suala la katiba,
akisema ni muhimu na lisipoangaliwa kwa umakini linaweza kuliingiza
taifa katika machafuko.
“Wabunge wote watakapokuwa Dodoma wajue wana dhamana kubwa sana,
wasifanye mzaha na suala la katiba, ni suala muhimu kwani katiba mbaya
inaweza kuangamiza. Suala la kubadilishwa katiba halifanyiki kama
wanavyobadili sheria.”
“Wanapitisha leo, rais anasaini anawarudishia wakafanye mabadiliko, si
kitu rahisi. Wakumbuke kuwa wakiamua vibaya wataangamiza taifa kwa muda
mrefu na wakiamua vizuri watalisaidia taifa,” alisema.
Kasaka alitumia muda mwingi kuelezea historia ya kundi hilo (G55),
akisema lilianzishwa baada ya manung’uniko ya Wazanzibari kuwa wanaonewa
na Serikali ya Muungano.
“Wazanzibari walisema kuwa Serikali ya Tanganyika imejifanya kuwa ni
ya muungano ili kuitawala Zanzibar bila ridhaa ya Wazanzibari na kwamba
ilizuia Serikali ya Zanzibar kufanya mambo yake.
“Serikai tatu ni wazo la CCM, kwani wakati tunalianzisha vyama vya
upinzani vingine havijasajiliwa na vilivyokuwapo havikuwa na
wabunge, vilikuwa makundi ya wanaharakati wakati huo, waliunga mkono
kutaka mabadiliko,” aliasa.
Kasaka aliongeza kuwa hali ya wakati huo ilimuudhi kwani mtu wa Bara
alikuwa akitaka kwenda Zanzibar inabidi awe na hati ya kusafiria na
kuchukuliwa kama mgeni wakati wanazungumzia nchi moja.
“Nilipeleka hoja bungeni, ikaungwa mkono na Matheo Qares, Arcado
Ntagazwa, Mussa Nkhangaa, William Mpiluka (marehemu), Sebastian Kinyondo
(marehemu) na Jenerali Ulimwengu. Kwa ujumla niliungwa mkono na wabunge
55, ingawa baadaye wabunge karibu wote walituunga mkono tukaambiwa
halimo katika sera za CCM,” alisema.
Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo, serikali tatu au mabadiliko ya muundo wa Muungano kutoka wakati huo hadi sasa hayaepukiki na
kwamba, mtazamo wa Wazanzibari wanasema wapo tayari kutofautiana
katika mambo yote kisiasa au kiitikadi lakini hoja ya Uzanzibari
(identity ya nchi) haifi hadi utakapomwondoa Mzanzibari wa mwisho.
“Kumbuka kuwa aina ya Watanzania wa sasa si wale wa miaka 30
iliyopita, wakati huo walikuwa wanazaliwa, ila sasa wao ndio wasomi na
wasemaji katika mambo mengi.
“Nawatahadharisha wabunge waangalie idadi ya Watanzania sasa si ile
iliyokuwapo, mwamko wa sasa si ule wa miaka iliyopita. Mwaka 1993 -1995
watu waliokuwa wanajitambulisha ni wapinzani walikuwa wanazomewa, sasa
wale wanaojitambulisha CCM ndio wanaozomewa, wakubali mabadiliko,
serikali tatu haziepukiki na hii ilikuwa hoja ya wabunge wa CCM,”
alisema.
Kasaka alisema wabunge wakubali kufanya marekebisho ya sheria
iliyorejeshwa na rais, kwani serikali haiwezi kujitungia katiba, hivyo
wabunge wote hasa wa CCM wakubali suala la serikali tatu, wafanye
marekebisho mazuri ili kuondoa uwezekano wa mgogoro mkubwa kati ya Bara
na Zanzibar.
Alimpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kauli yake aliyoitoa mjini Dodoma
hivi karibuni ya kukemea vitendo vya rushwa ndani ya chama, akisema
itawaathiri kwenye Uchaguzi Mkuu ujao ikiwa hawatajirekebisha.
Alisema anakubaliana na Kikwete kwa asilimia mia moja kwamba CCM
isipoacha rushwa itaanguka, na isipoacha upendeleo na kulazimisha
wagombea wasiokubalika vilevile itakufa.
Kasaka alimtaka Rais Kikwete kuchukua hatua, asiishie kusema kwa vile
anaweza kutumia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa
masuala ya kisheria na mengine ya kiutendaji yapo chini ya uwezo wake.
“CCM watu hawachukuliani hatua, Makamu Mwenyekiti (Bara), Philip
Mangula, alilalamikia rushwa aliposhindwa uenyekiti wa Mkoa wa Iringa,
lakini aliishia kusema kuwa uongozi katika chama unapatikana kama bidhaa
gulioni, na alipochaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wala hajawahi
kuchukua hatua,” alisema.
Kasaka aliongeza kuwa hadi Rais Kikwete ameamua kujitoa kuyasemea hayo
nje, ni kwa sababu ndani ya CCM watu si wasikivu, wengine wana dharau.
“Ukiona mke na mume wanatukanana hadharani ujue ndani wametukanana vya
kutosha na imeshindikana, wameonyana imeshindikana, ndiyo maana
wanakuja hadharani kuja kukemeana mbele yetu,” alisema.
0 comments:
Post a Comment