MWALIMU Julius Nyerere aliwahi kusema kuwa mtu akikupa ushauri
wa kipumbavu, na akafahamu kuwa unafahamu kwamba ushauri anaokupa ni wa
kipumbavu, halafu wewe ukaukubali, atakudharau.
Jeshi la Polisi limejiingiza katika orodha ya kudharauliwa na Joshua
Mulundi. Labda pengine na Watanzania wengine wengi wameamua kulidharau
jeshi hilo kutokana na kituko lilichokifanya. Mulundi, ambaye
tunaaminishwa na Jeshi la Polisi kuwa ni raia wa Kenya, alilipa jeshi
hilo ushauri wa kipumbavu nalo likakubali.
Kijana huyu mdogo aliibuka siku moja jijini Dar es Salaam na hadithi
kuwa yeye alikuwa mmoja wa watu walioshiriki kumteka na kumtesa
aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Stephen Ulimboka.
Itakumbukwa kuwa Dk. Ulimboka alikutwa na madhara hayo wakati wa mgomo
mkali wa madaktari waliokuwa wakidai haki zao serikalini.
Kuteswa kwake kwa kiasi fulani kuliendana na hatua kadhaa za
kushughulikia tatizo hilo. Pamoja na hatua hizo, lakini kutekwa na
kuteswa kwa Dk. Ulimboka kwa namna ya kuhofisha, kwa kiasi kikubwa
kulisaidia kufifisha harakati na kuzima moto wa madaktari. Mgomo ukaisha
kwa ahadi tu. Haijulikani iwapo ahadi hizo zimetekelezwa au la.
Jeshi la Polisi, ambalo linapenda kujinasibu kwa umahiri wa kutumia
mbinu za kisasa kupata taarifa za kiintelijensia likamkamata kijana huyu
mara moja katika kanisa ambako alikuwa amekwenda kutubu dhambi zake.
Alifikishwa kituo cha polisi na kuhojiwa kwa kina. Polisi
walipojiridhisha wakaamua kutoka hadharani kwa kuwaita waandishi wa
habari na kutoa taarifa kwa umma. Katika taarifa hiyo, ambayo ilitolewa
katika kipindi ambacho jamii ilikuwa ikihitaji majibu ya kina kuhusiana
na aliyemtendea Dk. Ulimboka unyama, ilielezwa kuwa jeshi limekusanya
ushahidi na kujiridhisha kuwa kijana huyo kutoka Kenya alikuwa
ameshiriki kumteka na hatimaye kumtesa Dk. Ulimboka.
Wapo watu waliohoji iwapo Jeshi la Polisi lilikuwa na uhakika wa jambo
lililolitangaza, kwa sababu hadi wakati huo, Dk. Ulimboka, ambaye
maelezo yake yalionesha kuwa aliwafahamu watesi wake, alikuwa hajahojiwa
wala kutoa maelezo polisi. Walipohoji hivyo walidharauliwa na kuonekana
ni watu ambao wanataka kusababisha uchochezi.
Labda kwa lengo la kutaka kuzima mijadala ya kijamii iliyokuwa
imeshika kasi wakati huo, Mulundi alifikishwa mahakamani haraka na
kupelekwa rumande. Na kweli hatua hiyo ya kumfikisha Mulundi mahakamani
ilizima mjadala kuhusu kuteswa kwa Dk. Ulimboka ambao ulikuwa umeshika
kasi.
Lakini wapo watu wabishi ambao waliendelea kuhoji mantiki ya polisi
kushindwa kumhusisha mwathirika huyo katika kumtambua mtuhumiwa ambaye
hadi wakati huo alikuwa peke yake wakati taarifa zilizokuwapo zilionesha
kuwa kulikuwa na kundi la watu ambao walimteka na kumtesa Dk. Ulimboka
kabla ya kumtelekeza katika msitu wa Mabwepande.
Wiki chache baadaye, ofisi ya mwendesha mashitaka ilimfutia Mulundi
mashitaka kuhusiana na tuhuma za kumteka na kumtesa Dk. Ulimboka. Hili
lilifanyika kwa sababu serikali haikuwa na ushahidi wa kuthibitisha
tuhuma hizo dhidi ya kijana huyo.
Hatua hii ilithibitisha hoja za watu wengi kuhusiana na hatua ya
kumhusisha Mulundi ya kutekwa na kuteswa kwa Dk. Ulimboka wakati daktari
huyo mwenyewe alishasema kuwa anawafahamu watu waliokuwa wamemteka.
Lakini Mulundi hakuachiwa huru. Alikamatwa tena na kufikishwa
mahakamani na safari hii akifunguliwa kesi ya kulidanganya Jeshi la
Polisi. Kwa maneno mengine, jeshi hilo lilikuwa linakiri hadharani kuwa
limedanganywa. Lilikuwa linakiri kuwa lilikuwa limepewa ushauri usio na
maana nalo likaukubali.
Kesi hii ya pili haikuchukua muda mrefu. Mulundi akakutwa na hatia ya
kulidanganya Jeshi la Polisi na kuhukumiwa adhabu ya kifungo au kulipa
faini. Kijana huyo akalipa faini ya sh 1,000 ndiyo, shilingi elfu moja,
na kuachiwa huru. Hatua ya mahakama kumtia hatiani kijana huyo kwa
upande mwingine ilithibitisha pasipo na shaka kuwa Jeshi la Polisi
lilikuwa limedanganywa.
Na hii ni hali inayopaswa kutufanywa Watanzania tuwe na hofu. Kama
raia wa Kenya anaweza kuibuka tu na kusema uongo katika kesi nyeti kama
hii, ambao unachukuliwa mzima mzima na Jeshi la Polisi na kuutumia
kumfungulia kesi ambayo baadaye jeshi lenyewe linakuja kukiri kuwa si
sahihi, hivi kweli tuuweke wapi weledi wa wananchi kwa Jeshi la Polisi?
Ni imani yangu kuwa katika hili Jeshi la Polisi limepata funzo kubwa.
Sitarajii kuwa tutashuhudia kituko kingine kama hiki kuhusiana na Jeshi
la Polisi.
Lakini, kumalizika kwa kesi ya Mulundi kulidanganya Jeshi la Polisi
hakumaanishi kuwa kesi dhidi ya waliomteka na kumtesa Dk. Ulimboka nayo
imekwisha. Kwa sababu mara ya kwanza Polisi wamekiri kudanganywa, ni
wakati sasa wa wao kusahihisha makosa na kuhakikisha linawasaka na
kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wale wote waliohusika na tukio hilo
la kuhuzunisha.
Ni zaidi ya mwaka mmoja umepita sasa tangu Dk. Ulimboka atekwe na
kuteswa Juni mwaka jana. Kwa Jeshi la Polisi ambalo lina wataalamu wa
kutosha pamoja na vifaa, akiwamo mwathirika ambaye yupo tayari kutoa
ushirikiano, huo ni muda mrefu sana kupata taarifa zitakazowezesha
wahusika hawa wa ukatili huu wajulikane na kupatikana.
Kwa jinsi tukio hili lilivyo halioneshi kuwa na ugumu mkubwa sana wa
kuwabaini waliohusika na kuwachukulia hatua. Lakini jambo la kushangaza
ni kuwa hilo halijatokea na hakuna dalili kuwa linaweza kutokea siku za
hivi karibuni.
Kukamatwa, kushitakiwa na kuachiwa kwa Mulundi kunaonekana kuwa kama
sinema au tukio la kufunika kombe ili mwanaharamu apite. Majibu
yanayotolewa na Jeshi la Polisi kwa watu wanaohoji ni kipi kinakwamisha
kuwakamata waliomteka na kumtesa Dk. Ulimboka, hayaoneshi kuwa jeshi
hilo lina dhamira ya dhati kuimaliza kesi hiyo kwa namna ambayo
itawaridhisha Watanzania wengi.
Hii ni kasoro ambayo inapaswa kurekebishwa haraka kwa ajili ya kujenga
taswira nzuri ya Jeshi la Polisi lakini pia ni hatua nzuri ya
kuhakikisha kuwa haki imetendeka.
0 comments:
Post a Comment