Jakaya Mrisho Kikwete
MWENYEKITI wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya
Kikwete, ameonyesha wasiwasi wa chama hicho kushindwa katika uchaguzi wa
serikali za mitaa 2014 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 iwapo watendaji
wake wataendelea na vitendo vya rushwa.
Alisema kuwa kwa sasa chama hicho kikongwe kimepoteza matumaini kwa
Watanzania kutokana na vitendo ambavyo siyo vya kiungwana vinavyofanywa
na watendaji.
Kwa kusisitiza, Kikwete alisema hata kama CCM itashinda uchaguzi wa
2015, kama tabia walizonazo watumishi na viongozi ndani ya chama
hazitabadilika, ni wazi kuwa hakitapita kwenye uchaguzi wa 2020.
Rais Kikwete alitoa onyo hilo mjini hapa juzi usiku, alipokuwa
akifunga mafunzo maalumu ya siku nne kwa makatibu na wenyeviti wa
wilaya na mikoa wa chama hicho nchini nzima.
“Kama hatutabadilika katika suala la rushwa, mwaka 2015 tutakuwa na
wakati mgumu sana, na kama mwaka huo tutafanikiwa kuishika serikali,
basi mwaka 2020 hatutarudi tena madarakani.
“Najua rushwa ipo na mnaendelea kupokea shilingi laki mbili za ‘airtime’
(muda wa mawasiliano), ndugu zangu hatutafika, ama wengine watavuka na
wengine kukwama,” alisema.
Alisema tatizo la rushwa kwa viongozi wa chama hicho linazidi kuwa
kubwa kila siku hali ambayo inawapotezea imani wananchi ambao ndio
wapiga kura wao.
“Viongozi wa chama ndio mmekuwa mawakala wa kusambaza rushwa bila hata
aibu, nawaombeni tubadilike, kama tutaendelea hivi hali yetu itakuwa
ngumu sana katika chaguzi mbalimbali nawaambieni,” alisema Kikwete
ambaye alitumia muda wa saa mbili kufunga mafunzo hayo.
Alisema kuwa inasikitisha kuona kuwa wapo baadhi ya watu ambao
wameanza kujipitisha kwa viongozi wa chama na kuwapatia hela kwa ajili
ya kuwapigia debe ili wawachague katika nafasi mbalimbali za urais ama
ubunge.
Alisema kuwa kimsingi kwa sasa wapo watu ambao wameishaanza kuzunguka
na kujinadi kutafuta nafasi mbalimbali za kugombea, huku wakipenyeza
rushwa jambo ambalo linaendelea kukishushia hadhi chama hicho.
Akizungumzia chuki ndani ya chama, alisema Watanzania kwa sasa
wameishakuwa na akili zao, na hivyo hawataki kudanganywa kwani viongozi
wengi ndani ya chama hawajui hata ilani ya chama chao.
“Wapo baadhi ya viongozi ndani ya chama hawajui hata ilani ya chama
chao, wakipanda kwenye majukwaa wanaanza kuzungumzia ujenzi wa daraja
la Mkapa ama lile la Malagarasi, watu hawataki kusikia hayo, mtu wa
Ngara anataka kujua daraja lake limeishaje siyo la Mkapa,” alisema.
Hata hivyo, alisema kwa sasa vyama vya upinzani vinafanya kazi kubwa
zaidi ya kuwatembelea wananchi na kusikiliza kero zao tofauti na
ilivyo kwa CCM ambayo viongozi wake wapo mbali na wananchi.
“Wapo watu ambao wanadai kuwa chama kitafia mikononi mwangu, nataka
niseme kuwa hakifii mikononi mwangu, kitafia mikononi mwenu,”
alisisitiza.
Kikwete alisema kuwa siku hizi watu wana mbadala wa vyama vingine na
siyo CCM peke yao, na hivyo kuwataka viongozi wanaojihusisha na vitendo
vya rushwa waondolewe mara moja katika nafasi zao.
“Tuna vijana wengi kutoka katika vyuo mbalimbali ambao wanaweza
kufanya kazi kwa uadilifu wa hali ya juu, hivyo hatuna budi kuachana na
hawa wala rushwa ambao watatupotezea sifa yetu kwa wananchi.
Tukipoteza urais ndiyo tumekwisha na chama kinaweza kufa.”alisema.
Katika hatua nyingine, Kikwete aliwaonya viongozi ambao wanajihusisha
na uuzaji wa mali za chama kama vile viwanja na baadhi yao kuingia
mikataba yenye utata.
Hata hivyo, aliwataka makatibu hao na wenyeviti wa wilaya na mikoa
kuhakikisha wanawatembelea wanachama wao na kutafuta wengine wapya kwa
ajili ya kujiimarisha kwa chaguzi mbalimbali zijazo.
0 comments:
Post a Comment