Zitto Kabwe
WAZIRI Kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe, amesema Tanzania inapoteza jumla ya dola za Marekani kati ya milioni 500 na bilioni 1.25 kwa mwaka, kutokana na kampuni kubwa za kimataifa kukwepa kodi.

Alisema kuwa hiyo ni sawa na kusema Tanzania inapoteza dola takriban milioni mbili kila siku kwa uporaji huu,” alisema.

Kwa mujibu wa Zitto, wakati shinikizo la dunia sasa limeelekea kumaliza tatizo la ukwepaji kodi na utoroshaji wa fedha kutoka nchi za Kiafrika, Serikali ya Tanzania inavuta miguu.

Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA) na mmoja wa wabunge waliovalia njuga sakata la vigogo kuficha fedha katika benki za nje, alitoa kauli hiyo katika taarifa yake aliyoisambaza kwenye vyombo vya habari jana.

Alisema moja ya njia za serikali za nchi maskini kupata taarifa za kampuni kubwa za kimataifa (MNCs) zinazokwepa kodi ni mfumo wa kupashana taarifa (automatic exchange of tax information).

“Kufuatia shinikizo la nchi mbalimbali, hivi sasa nchi zinazoitwa ‘secrecy jurisdictions’ (tax havens), zimeanza kuweka sahihi makubaliano ya kutoa taarifa. Tanzania mpaka sasa haijaweka sahihi na serikali haijatoa taarifa yoyote kwa umma,” alisema.

Kwa mujibu wa Zitto, Ghana, Afrika Kusini na Nigeria ni nchi zinazotegemea sana rasilimali kama Tanzania ambazo zimeweka sahihi mkataba huu tayari.

Alisema kuwa asilimia 44 ya fedha za kigeni nchini zinatokana na mauzo ya madini nje. Kampuni za madini ndizo zinaongoza kukwepa kodi.

“Naitaka serikali kutoa taarifa kwa nini haichukui hatua kuzuia mwanya huu wa mapato ya umma. Serikali ichukue hatua mara moja kuhakikisha Tanzania inaingia makubaliano ya kupashana taarifa za kikodi.

“Huu si wakati wa kuvuta miguu katika suala nyeti la umma. Badala ya kukimbilia kutoza kodi wanyonge, tuhakikishe kampuni kubwa zinazonyonya rasilimali zetu zinalipa kodi inayotakiwa,” alisema.

Mapema asubuhi jana, akihojiwa na kituo kimoja cha redio, Zitto alisema sababu ya vigogo wengi kuficha fedha nje ya nchi ni ukubwa wa kodi inayotozwa hapa nchini inayofikia asilimia 30.

Alisema kodi hiyo ni kubwa zaidi ikilinganishwa na nchi zile wanakoficha fedha, mathalani Uswisi inatoza asilimia 0, Mauritius asilimia 17, wakati Cayman ikitoza kati ya asilimia 0 mpaka 3.

Zitto alifafanua kuwa baada ya nchi nyingi za Ulaya na Marekani kuona wananchi wakificha fedha zao katika nchi zao, walikaa pamoja na kuandaa mkataba wa kuwezesha kupeana taarifa za fedha zinazokuwa zinaingizwa na raia wa mataifa mengine.

Alisema anashangazwa kuona kwamba pamoja na nchi hizo kutoa ofa hiyo ya kubadilishana taarifa za kikodi ni nchi nne pekee za Afrika zilizosaini mkataba huo.

Zitto alizitaja baadhi ya benki ambazo Watanzania wengi wana fedha kuwa ni Uingereza, Jersey, Cayman Islands, Mauritius na Dubai. 
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top