IGP Said Mwema
JESHI la Polisi nchini limewafukuza kazi askari wake 56 katika
kipindi cha mwaka mmoja, kutokana na makosa ya kuomba na kupokea rushwa
pamoja na utovu wa nidhamu.
Kamishna msaidizi wa jeshi hilo, Patrick Byatao, alisema hayo jana
alipokuwa akitoa ufafanuzi juu ya mambo mbalimbali hususan masuala ya
nidhamu kwa askari wake katika warsha ya siku maalumu ya polisi
iliyofanyika mjini Bukoba.
Alisema kuwa askari waliofukuzwa ni kutoka katika mikoa mbalimbali
nchini ambao wamekutwa na tuhuma za utovu wa nidhamu ikiwemo kuomba
rushwa kwa wananchi ambapo katika kipindi cha mwaka 2012, waliwafukuza askari 35
na mwaka huu 21.
Kwa mujibu wa Byatao, wapo baadhi ya askari ambao wamekuwa wakitoa
visingizio vya kuomba rushwa kwa sababu mishahara yao ni midogo na
haitoshelezi mahitaji yao.
Alisema ni heri askari wa aina hiyo wakaacha jeshi, vinginevyo
wataendelea kuchukuliwa hatua kama hawatafuata masharti ya kazi yao.
Akitoa mada juu ya kuimarisha maadili ndani ya jeshi hilo, Mrakibu
Msaidizi wa Polisi kutoka makao makuu, Andrew Makungu, alisema
wameanzisha mkakakati wa kudhibiti vitendo vya ukiukwaji maadili kwa
askari wake ikiwemo rushwa.
Alitaja maeneo lengwa kuwa ni chumba cha kupokea taarifa za
mashitaka, usalama barabarani na upelelezi wa makosa ya jinai. Bado
juhudi zinaendelea ili kuboresha maeneo mengine.
Makungu alisema ubia wa kiutendaji wa jeshi hilo umekuwa ukiimarika
kila siku baada ya sehemu kubwa ya jamii kutambua nafasi yao katika
jukumu hilo.
Alisema mambo hayo yanaonekana kutokana na wananchi kufanya ulinzi wa
maeneo yao, kuchangia rasilimali kwa jeshi, kutoa taarifa sahihi za
uhalifu, kujenga vituo vya polisi na kuanzisha vikundi vya ulinzi
shirikishi. Hadi sasa viko vikundi 5,344 nchi nzima huku Mkoa wa Kagera
ukiwa na 431.
Naye mgeni rasmi katika warsha hiyo, Meya wa Manispaa ya
Bukoba, Anatory Amani, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali
mstaafu Fabian Massawe, alisema kuwa Jeshi la Polisi limekuja na
mkakati wa polisi jamii/ulinzi shirikishi unaoelekeza kuwapo kwa
mashauriano, majadiliano ya kiutendaji yanayosisitiza uwepo wa maadili
katika kazi, ikiwemo mapambano dhidi ya rushwa ndani ya jamii.
0 comments:
Post a Comment