Mawaziri wa mambo ya nje Afrika wanakutana mjini
Addis Ababa nchini Ethiopia kujadili uhusiano wa bara la Afrika na
mahakama ya kimataifa ya jinai ICC.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ethiopia, Tedros
Adhanom Ghebreyesus, ameilaani mahakama ya ICC kwa kusema ina mapendeleo
sana na hicho sio kitu kinachokubalika na kuwa ina uonevu kwa nchi za
Afrika.
Waziri huyo ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa kikao maalum cha AU kuhusu mahakama ya ICC.
Kikao hicho kinafuatia ombi la serikali ya kenya.
Umoja wa Afrika unaishtumu mahakama ya ICC kwa
kuwalenga viongozi wa bara hilo huku ikipuuzilia mbali uhalifu mwengine
dhidi ya binadamu unaotekelezwa katika maeneo mengine ulimwenguni.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho
waziri wa maswala ya kigeni kutoka Ethiopia Tedros Adhanom ameishutumu
mahakama hiyo kwa kukataa kuheshimu uwezo wa marais wa bara la Afrika na
kukitaka kikao hicho kushutumu mahakama hiyo.
Aidha amekitaka kikao hicho kuwasilisha ombi la kuahirisha kesi zinazowakabili Rais wa kenya Uhuru Kenyatta na makamu wake Wiliam Ruto kusikizwa katika mahakama hiyo.
Mkutano huu maalum umeitishwa baada ya ICC
kukataa ombi la wanachama 34 wa Muungano wa Afrika kurejesha kesi za
Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto nyumbani.
Miongoni mwa yatakayozungumziwa ni hoja ya kujiondoa kutoka kwa mahakama hiyo.
Baada ya miezi kadhaa ya kutofautiana kati ya
ICC na AU, viongozi wa Afrika wanakutana katika makao makuu ya AU katika
kile kinachosemekana ni kutafakari upya uhusiano wa bara hilo na
mahakama ya ICC.
Kwa mujibu wa AU, mahakama hiyo ya ICC imekosa
kushughulikia ombi lililowasilishwa na AU mwezi Mei kuhusu kesi za
Kenya. AU inasema kuwa ICC ina njama za kibaguzi dhidi ya viongozi wa
kiafrika.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na naibu wake
William Ruto wanakabiliwa na kesi za ukiukwaji wa haki za binadamu
katika mahakama hiyo.
Kesi yao inahusiana na ghasia za baada ya uchaguzi mkuu Kenya mwaka 2007/2008 ambapo zaidi ya watu 1100 waliuawa.
Hata hivyo viongozi hao wamekanusha madai hayo.
Bunge la Kenya ambalo lina idadi kubwa ya
wabunge wa mrengo wa Jubilee unaotawala nchi, tayari lieanzisha hoja ya
kuondoa Kenya kutoka katika mahakama ya ICC.
Lakini serikali ya Kenya imesema haijashinikiza
nchi za Afrika kujadili hoja ya kujiondoa ICC licha ya kuungwa mkono na
majirani zake kama Uganda na Rwanda.
Naibu mwenyekiti wa AU Erastus Mwencha, ameambia BBC kuwa swala hilo sasa ni zaidi ya kutaka tu kujiondoa ICC.
Wadadisi hata hivyo wanasema kuwa huenda AU
isikubali kwa ujumla kujiondoa ICC. Baadhi ya nchi kama Ghana na
Botswana tayari zimepinga hatua ya kujiondoa ICC.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment