Zitto Kabwe
MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto
Kabwe, amedai kuwa kuna wimbi la utoroshaji mkubwa wa fedha haramu nje
ya nchi kuliko fedha za msaada na uwekezaji kutoka kwa wafadhili.
Aidha, Zitto amedai kuwa makampuni makubwa saba kati ya kumi
yanayoongoza kwa kutorosha fedha na kuzificha katika nchi ambazo
zimeweka sera za unafuu wa kodi na zisizokuwa na sheria za udhibiti wa
uingizaji na upatikanaji wa mapato.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Zitto alisema
kati ya makampuni makubwa matatu ya simu hapa nchini, mawili yanahusika
na ukwepaji mkubwa wa kodi kwa kujisajili katika nchi za Uholanzi na
Ubelgiji, hivyo kuepuka kulipa kodi walizotakiwa.
Zitto alizidi kufichua kuwa moja ya kampuni kubwa za madini iliyoko
hapa nchini imesajili makampuni mengine tisa katika nchi hizo, huku moja
ya kampuni kubwa ya madini ikihusishwa na utoroshaji huo mkubwa.
Alisema nchi wahisani hutoa misaada inayokadiriwa kufikia kiasi cha
dola za Marekani bilioni 37 huku uwekezaji kutoka nje ukiwa ni dola za
Marekani bilioni 40 kwa mwaka.
Akizungumza juu ya mkutano wa 10 wa umoja wa kamati za mabunge za
hesabu za serikali kutoka nchi wanachama wa SADC, (SADCOPAC),
unaofanyika jijini hapa, alisema kumekuwa na matukio mengi ya kutorosha
fedha na rasilimali za taifa katika nchi nyingi, na kuitolea mfano
Tanzania ambayo imekumbwa na matukio hayo kwa kiwango kikubwa.
Alisema kumekuwa na utoroshaji wa fedha za taifa kupitia uuzaji wa
mazao ya biashara, huku watendaji wa serikali wakionekana kuzidiwa
ujanja.
“Mwaka 2011 Tanzania iliuza nje ya nchi tani 80,000 za korosho ambapo soko letu kuu ni India.
“Lakini utashangaa kuwa India wenyewe walisema kwa mwaka huo walipokea
tani 120,000 kutoka kwetu, na hii
inaonesha kuwa tani 40,000 zilitoroshwa bila kulipiwa kodi wala Benki
Kuu (BoT) haina taarifa nazo, hivyo hawawezi kuzirudisha nchini kwa
kuhofia kubainika,” alisema.
Aliongeza kuwa Tanzania inapoteza asimilia tano ya pato la ndani la
taifa (GDP) kwa usafirishwaji wa fedha haramu zinazotokana na ukwepaji
wa kodi na rushwa ambayo ni sawa na zaidi ya dola za Marekani bilioni
1.25 kila mwaka.
Aidha, amesema kuwa kiasi cha zaidi ya dola za Marekani bilioni 844
zimekuwa zikitoroshwa nje ya Bara la Afrika kila mwaka kwa kipindi cha
kuanzia mwaka 2000 mpaka 2010 wakati misaada kutoka nchi wahisani na
uwekezaji kutoka nje (FDI) zikikadiriwa kufikia kiasi cha dola za
Marekani bilioni 80 kwa mwaka.
“Theluthi mbili ya fedha haramu hutoroshwa kwa kughushi nyaraka za
malipo kwa kuongeza au kupunguza gharama halisi ya bidhaa
wanazosafirisha nje au kuingiza barani Afrika ambapo kila dola moja
inayokuja Afrika kama msaada dola saba hutoroshwa kwa njia haramu,”
alisema.
Alifafanua kuwa sheria za nchi hizo, hazimlazimishi mtu ama kampuni
kutoa maelezo ya namna alivyopata fedha hizo, na kama analipa kodi
sahihi, jambo linalowavutia watu na makampuni yasiyo na uaminifu kuficha
fedha hizo huko.
Zitto alisema kwa kuwa matukio ya aina hiyo yamesababisha athari kubwa
za kiuchumi, hivyo ni jukumu la kamati za mahesabu ya umma kwenye kila
nchi kufanya kazi ya kudhibiti utoroshwaji wa fedha haramu huku
akiainisha changamoto iliyopo kwenye baadhi ya nchi za Afrika ambazo
hazina kamati hizo, na zile zilizonazo za muda tu, kama Zambia na
Swaziland.
Kutokana na hujuma hizo, wajumbe wa mkutano huo wanaokadiriwa kufikia
300 wamewasukumia lawama wabunge wa nchi nyingi za Afrika kwa kuweka
mbele masilahi ya vyama vyao vya siasa badala ya masilahi ya wananchi.
Mbunge wa Afrika Kusini, Nikiwe Num, wakati akichangia mada kwenye
mkutano huo wa kamati za usimamizi wa hesabu za serikali za nchi za
Kusini mwa Afrika (SADCOPAC), alisema lazima wabunge wazibane serikali
zao kikamilifu, vinginevyo wimbi la hujuma litaongezeka.
Ameongeza kuwa kama wabunge hawatabadilika, wataendelea kulalamika tu,
badala ya kuchukua hatua dhidi ya watawala na kuweka kando tofauti zao
za kiitikadi.
“Mataifa ya Afrika yana katiba nzuri sana, tatizo hazifuatwi na
tukiendelea kuweka mbele masilahi ya vyama hatutaweza kuzisimamia
serikali kwani wabunge wengi wanatoka kwenye vyama tawala kila mara
tutakuja hapa tukilialia kuwa mambo hayaendi lazima tubadilike,” alisema
Num.
Awali Mwenyekiti wa SADCOPAC, Sipho Makama, kutoka nchini Afrika
Kusini alisema kuwa mkutano huo unazikutanisha nchi zote za SADC
isipokuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambayo kwa sasa hali si
shwari nchini humo kutokana na vita inayoendelea kati ya serikali na
waasi wa M23.
Zaidi ya wajumbe 300 wanahudhuria mkutano huo ambao ni wabunge wa
kamati za hesabu za serikali, wakaguzi na wadhibiti wa hesabu za
serikali, wahasibu wakuu wa serikali, makatibu wa kamati za PAC, maspika
wa mabunge ya SADC pamoja na wahisani kutoka taasisi mbalimbali za
kimataifa.
0 comments:
Post a Comment