Rais wa Urusi Vladimir Putin, ameonya Marekani na nchi za Magharibi dhidi ya kushambulia Syria ambapo alisema kuwa hatua zozote za kijeshi dhidi ya Syria itakuwa ni uvamizi.
Rais wa Marekani Barack Obama ametoa
wito wa kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Syria baada ya kusema kuwa
kuna thibitisho kuwa rais Assad ametumia silaha za kemikali dhidi ya
wananchi wake.
Lakini kwenye mahojiano na shirika la habari la
Associated Press, kabla ya mkutano wa wiki hii wa G-Twenty mjini St
Petersburg, bwana Putin alisema kuwa huenda akaunga mkono azimio la
Umoja wa Mataifa ikiwa kuna thibitisho kuwa silaha za kemikali
zilitumiwa dhidi ya raia.
Putin pia alipuuza wasiwasi kuwa wanariadha au
mashabiki wataadhibiwa ikiwa watatoa matamshi yatakayoonekana kuwa
propaganda kuhusu mapenzi ya jinsia moja wakati wa michezo ya olimpiki
itakayofanyika nchini humo.
Wakati huohuo , maseneta nchini Marekani
wameridhia mswada wa azimio linalompa idhini Rais Barack Obama
kutekeleza shambulio la kijeshi dhidi ya Syria. Mswada huo utapigiwa
kura wiki ijayo.
Awali Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani
John Kerry alifika mbele ya Baraza la Senate ambapo alitoa onyo kwa
maseneta wa Marekani kabla ya mdahalo wao kuhusu Syria unaotarajiwa
kufanyika wiki ijayo kwamba, hawapaswi kushindwa kutoa jibu la kile
alichokitaja kuwa ni matumizi ya silaha za kemikali ambayo hayawezi
kukanushwa yaliyofanywa na Rais Assad kwa watu wake mwenyewe .
Naye Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon
amesema kuwa ikiwa itathibitishwa kwamba silaha za sumu ya kemikali
zilitumiwa nchini Syria , baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lazima
liungane na kuchukua hatua.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment