Moshi mkubwa ukitoka katika meli hiyo baada ya wahusika kujitosa majini.
MELI iliyosajiliwa nchini Tanzania ya MV Gold Star juzi Ijumaa
ilikamatwa nchini Italia ikiwa na dawa za kulevya zenye thamani ya pauni
milioni 50 sawa na shilingi bilioni 126. 5 ambapo watuhumiwa waliokuwa ndani
ya meli hiyo waliamua kuichoma moto ili kupoteza ushahidi na kujitosa majini lakini walitiwa nguvuni na wanausalama wa Italia.
Meli hiyo ya mizigo ilikuwa imepakia tani 30 za madawa na ilikamatwa
jirani na Kisiwa cha Sicilia katika Bahari ya Mediterania nchini
Italia baada ya maafisa uhamiaji kupata taarifa kuwa meli hiyo ilikuwa imebeba kiasi kikubwa cha shehena ya madawa ya kulevya na hivyo kuifuatilia kwa muda mrefu kabla ya zoezi la kuikamata.
Maofisa wa polisi wa nchini humo wamedai
kuwa watuhumiwa hao tisa walikuwa raia kutoka Syria na Misri ambapo waliisajiri meli yao Tanzania.
Chanzo hicho kimeeleza zaidi kuwa meli hiyo ilifuatiliwa kwa karibu na helikopta na boti za usalama ziendazo kasi jambo lililowashitua waliokuwa ndani ya meli hiyo na kuwafanya wajitose baharini ili kukwepa mkono wa sheria ingawa walikamatwa baadaye kwa vile hawakuweza kuogelea hadi ufukweni kutokana na umbali uliopo kati ya eneo la tukio na ufukweni.
"Meli
ilizuiliwa baada ya kupata taarifa za kiintelijensia zilizoonesha kuwa
ilikuwa imebeba madawa ya kulevya-lakini hatukutarajia kiasi kikubwa namna hiyo na
wahusika kuichoma moto" alisema msemaji wa uhamiaji Italia.
"Nia yao bila shaka ilikuwa kujaribu kupoteza usahidi ili tusiweze kuwatia hatiani lakini mpango wao haukufanikiwa, moto ulizimwa na madawa ya kulevya yakapatikana baada ya upekuzi" alifafanua zaidi.
Boti maalumu ziliitwa kwa ajili ya kuzima moto uliokuwa ukiwaka katika meli na baada ya kufanikiwa kuuzima meli hiyo ilipelekwa katika bandari ya Sicilia ambako watuhumiwa hao walipelekwa kwa mahojiano zaidi.
Tukio hili linatokea katika kipindi ambacho Tanzania imekumbwa na wimbi la baadhi ya watu kukamatwa kwa tuhuma za kukutwa na madawa ya kulevya jambo linalozidi kuichafua nchi kimataifa ingawa katika mkasa huu meli inaonekana kusajiriwa Tanzania lakini watuhumiwa wote wanatajwa kutoka mataifa mengine jambo linalozidi kuibua changamoto nyingine kwa vyombo husika.
Chanzo:http://www.dailymail.co.uk/news/
0 comments:
Post a Comment