VYAMA vya CHADEMA na CUF vimezidi kumwandama Naibu Spika wa
Bunge, Job Ndugai, kwa hatua yake ya kuwanyanyasa na kuwadhalilisha
wabunge wa upinzani akiwemo kiongozi mkuu wa kambi hiyo, Freeman Mbowe.
Wakati Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, akilaani kitendo
hicho cha Ndugai kumzima Mbowe na kuamuru askari wamtoe nje kwa nguvu,
alikiita ni cha udhalilishaji na kisichokubalika; sekretarieti ya
CHADEMA imeitisha kikao cha dharura kwa ajili ya kupokea taarifa ya
masuala mbalimbali yaliyojitokeza bungeni na kisha kutoa uamuzi wa nini
kifanyike.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Prof. Lipumba alisema kuwa
kitendo hicho ni cha aibu hakikupaswa kufanywa na Naibu Spika wa Bunge
kwani angesimama Waziri Mkuu Mizengo Pinda asingeweza kumnyima nafasi ya
kuzungumza.
“Sisi CUF tunajiuliza, angesimama Pinda kuongea Naibu Spika angemnyima nafasi? Angethubutu kuamrisha askari wamtoe nje?
“Kwa nini haya yanatendwa kwa mpinzani na hayawezi kutokea kwa kiongozi wa serikali?” alihoji.
Lipumba pia alihoji kama serikali ina mamlaka makubwa katika Bunge
kuliko Bunge lenyewe hadi kiti cha Spika kiendeshe masuala kwa taratibu
za kupendelea serikali.
Alisema kwa kuwanyima haki wabunge wa upinzani hasa kiongozi wao wa
pande zote mbili ni njama za wazi za serikali na kiti cha Spika
kutelekeza maoni ya wananchi na kuyapatia kipaumbele yale ya CCM kwa
maslahi yao.
Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa kufanya hivyo kunaondoa uhalali wa
Bunge na kiti cha Spika katika kusimamia mchakato huo huku akitaja moja
ya njama za wazi kuwa ni pamoja na ile ya wabunge 166 wa Bunge la Katiba
wanaopaswa kupendekezwa na taasisi mbalimbali na kuteuliwa na rais.
“CUF tumesikitishwa na mabadiliko yaliyofanywa na lengo la CCM la
kupitisha muswada unaompa mamlaka ya uteuzi rais kwani hivi sasa kila
taasisi bila kujali uzito wake husika itapaswa kuteua majina tisa na
kumpa rais na kisha atateua jina moja au asiteue kabisa jina lolote,”
alisema.
Alifafanua kuwa sheria hiyo inampa rais mamlaka kuteua watu anaowataka kuwa wajumbe wa Bunge la Kutunga Katiba.
Prof. Lipumba alisema CCM na serikali yake inajua kuwa hujuma
wanazozifanya katika mchakato wa Katiba ndizo zitawapa Katiba
wanayoitaka wao kama chama na haitakuwa na uhalali wa wananchi.
Alisema kuwa ombi la wabunge wa upinzani kuwa muswada huu urudishwe
kwa wananchi na kwa kamati kujadiliwa upya lilikuwa na mantiki kubwa,
kwamba msimamo wao kupinga muswada huu unapaswa kuungwa mkono na kila
Mtanzania.
Lipumba pia alizungumzia kitendo cha kudhalilishwa kwa wabunge akiwemo
mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, kwa kupigwa waziwazi na askari
ndani ya Bunge na kisha kutupwa kama mzigo nje ya lango.
Alisema pia mbunge wa viti Maalum CUF, Mozza Abeid, kuvuliwa vazi
lake la hijabu ni udhalilishaji mkubwa kwa wanawake na usiokubalika.
Alisema CUF inaendelea na juhudi ya kuwasiliana na viongozi wa vyama
vingine ili kuweka mkakati wa pamoja wa kukabiliana na hujuma dhidi ya
mchakato wa kupata Katiba mpya.
CHADEMA wakutana
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,
mkurugenzi wa habari na uenezi wa CHADEMA, John Mnyika, alisema kikao
chao cha sekretarieti kitakuwa chini ya Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa.
Alisema kiongozi wa wabunge wa chama hicho atatoa taarifa ya
yaliyojiri wakati wa kujadili muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria
ya mabadiliko ya katiba wa mwaka 2013 ambayo itajadiliwa na wajumbe wa
kikao hicho.
Mnyika alisema jambo kubwa watakaloliangalia katika kikao hicho ni
tafsiri ya mambo yote yaliyotokea kabla muswada huo haujafikishwa
bungeni ikiwamo uamuzi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuingilia kati
mchakato huo kwa manufaa yake.
“Yaliyotokea Septemba 4 hadi 6 bungeni yalipangwa kwa sababu maalum na
hii ni baada ya CCM kuona kila mwanya waliotaka kuutumia kukwamisha
rasimu ya katiba umeshindikana sasa wakaamua walitumie Bunge,” alisema.
Mnyika alisema katiba ni ya wananchi na kwamba kitendo chochote cha
kuihujumu ni mbinu ya kuwanyima kupata haki ya msingi ya kusikilizwa.
Aliongeza kuwa kwa sasa mwelekeo wa kuwa na katiba mpya itakayotumika
mwaka 2015 haupo na kwamba hicho ndicho CCM inakitafuta kwa nguvu zote
baada ya kuona wananchi kutaka muundo wa serikali tatu.
Alisema CHADEMA haiamini katika katiba isiyojali maslahi ya wananchi
na kwamba uharaka wa kukimbilia suala hilo hauna maana kwa kuwa suala la
uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 linaweza kutungiwa kanuni zake huku
mchakato wa kupata katiba bora ukiendelea.
“Madai ya katiba ni zaidi ya vyama vya upinzani, tutafanya taratibu ya
kukutana na wadau mbali mbali nchini kwa ajili ya kutoa uamuzi wa
pamoja,” alisema.
Mnyika alisema njama za kuhakikisha wabunge wa upinzani hawapati
nafasi ya kujadili rasimu ya sheria ya mabadiliko ya katiba zilianza
mara baada ya rasimu kutolewa hali aliyoeleza kuzua hofu kwa CCM.
Alisema hata maazimio ya Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria
iliyokutana na wadau mbalimbali yaliathiriwa na kikao cha CCM
kilichokutana mjini Dodoma ambapo jukumu hili lilirudishwa kwa wabunge
wao kwa ajili ya kuhakikisha katiba ya Watanzania haifanikiwi.
“Kamati ya wabunge wa CCM ilipewa jukumu hilo na mtekelezaji mkuu
akiwa ni yule atakayekaa katika kiti cha spika kuhakikisha wabunge wa
upinzani hawatoi hoja zao,” alisema.
0 comments:
Post a Comment