Shambulizi la kigaidi lililoua watu 67 nchini Kenya wiki
iliyopita, limeanza kuchukua sura mpya baada ya kubainika kuwa mawaziri
wanne na mkuu wa majeshi walipewa tahadhari kabla kuhusu kutokea kwa
tukio hilo.
Taarifa hizo mpya zimekuja wakati ripoti nyingine
za uchunguzi zikibainisha kuwa huenda magaidi walioshambulia jengo la
Westgate walitoroka kupitia njia ya ardhini inayoanzia kwenye maegesho
ya magari chini ya jengo hilo.
Kuhusu mawaziri
Tahadhari hiyo iliyoanza kutolewa Januari mwaka
huu, iliwaonya viongozi hao ambao pia ni wanachama wa Baraza la Usalama
la Taifa, kuwa Kundi la Al-Shabaab lilikuwa likipanga shambulizi jijini
Nairobi.
Kwa mujibu wa ripoti ya kuzuia ugaidi iliyonukuliwa na Gazeti la The Saturday Nation,
imewataja Waziri wa Fedha, Julius Rotich, Waziri wa Mambo ya Ndani,
Joseph ole Lenku, Waziri wa Ulinzi, Raychelle Omamo, Waziri wa Mambo ya
Nje, Amina Mohammed na Mkuu wa Majeshi, Jenerali Julius Karangi kuwa
walikuwa na taarifa za shambulizi hilo.
“Taarifa ilitolewa kwao ikiwatahadharisha
kuongezeka kwa vitisho vya ugaidi na mipango ya kuanzishwa kwa
mashambulizi mfululizo katika miji ya Nairobi na Mombasa kati ya
Septemba 13 na 20, 2013,” inasema ripoti hiyo.
Ripoti hiyo inasema kuwa magaidi walikuwa
wakipanga shambulizi linalofanana na lile lililotokea Mumbai, India
ambapo walishambulia jengo na kuteka raia.
Pia, taarifa hiyo ilitolewa kwa Kamati ya Ushauri
ya Usalama wa Taifa katikati ya Septemba, mwaka huu ambapo taarifa za
kiintelijensia zilionyesha kuwa Al-Shabaab wameongeza harakati zao Kenya
na kwamba walikuwa wanapanga shambulizi.
Kamati hiyo ambayo ndiyo ngazi ya juu ya usalama
nchini Kenya, inajumuisha Rais, Naibu Rais, Waziri wa Ulinzi, Mambo ya
Nje, Mambo ya Ndani, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkuu wa Majeshi,
Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa na Mkuu wa Jeshi la Polisi.
Viongozi wote waliotajwa kupewa taarifa
hawakupatikana, hata ujumbe mfupi wa maandishi waliotumiwa na gazeti
hilo kwenye simu zao haukujibiwa.
Shambulizi la wiki iliyopita kwenye jengo la
kibiashara la Westgate jijini Nairobi, linalomilikiwa wa raia wa Israel,
liliua watu 67 na zaidi ya watu 170 kujeruhiwa.
Israel iliionya Serikali ya Kenya dhidi ya kuwapo
kwa shambulizi la kigaidi kwenye majengo yanayomilikiwa na raia wa
Israel wakati wa msimu wa sherehe za Kiyahudi kati ya Septemba 4 na 28.
Ubalozi wa Israel, Nairobi, umetoa angalizo kwa Wizara ya Mambo ya Nje kuwa Iran na Hezbollah kutoka Lebanon wamekuwa wakikusanya taarifa za kiintelijensia za kutaka kuwalenga Waisrael na Wayahudi duniani kote ikiwamo Kenya,” inaonya ripoti iliyotolewa Septemba 13, 2013.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Ubalozi wa Israel, Nairobi, umetoa angalizo kwa Wizara ya Mambo ya Nje kuwa Iran na Hezbollah kutoka Lebanon wamekuwa wakikusanya taarifa za kiintelijensia za kutaka kuwalenga Waisrael na Wayahudi duniani kote ikiwamo Kenya,” inaonya ripoti iliyotolewa Septemba 13, 2013.
Pia, raia wa Marekani, Uingereza pamoja na Ofisi
ya Umoja wa Mataifa ambayo haikufahamika iwapo ililengwa kushambuliwa.
Ripoti hiyo inataja hata majina ya watu ambao wangehusika kwenye
shambulio hilo.
Inaendelea kufichua kuwa, shambulizi la Westgate
ambalo tayari limetekelezwa na jingine la Kanisa ya Holy Family
Basilica, Nairobi yalikuwa yamepangwa tangu mwanzoni mwa mwaka huu na
walioyaandaa wanatajwa na ripoti hiyo.
Inasema kuwa shambulizi la Westgate lilitekelezwa
na Al-Shabaab chini ya uongozi wa Abdi Godane, huku ikidaiwa kuwa baadhi
ya wanamgambo waliratibu shambulizi hilo kutokea eneo la Bullo Marer,
Somalia.
Godane ndiye kiongozi mpya wa Al-Shabaab baada ya
kuuawa kwa Omar Shafik Hammami na kumtimua Sheikh Aweys, ambaye aliamua
kujisalimisha kwa Serikali ya Somalia.
Rais Uhuru Kenyatta ameahidi kuwaadhibu magaidi
waliotekeleza shambulizi kwenye jengo la Westgate na kuapa kuwa jeshi
halitarudi nyuma katika kuilinda mipaka ya Kenya.
Ripoti hiyo, pia imetoa tahadhari kuhusu kuibuka
kwa vikundi vya kidini vyenye misimamo mikali Kaskazini Mashariki na
mikoa ya pwani ya nchi ya Kenya.
“Kule Lamu, idadi isiyofahamika ya Al-Shabaab
imejificha karibu na kambi ya wafugaji kati ya Katsakakairu na Nyangoro
karibu na Witu,” inasema ripoti hiyo.
Mbali na kuyalenga makanisa Kaskazini mwa Kenya,
magaidi hao wanadaiwa kulilenga jengo refu la Time Tower na baadhi ya
sehemu maarufu za burudani kwenye mitaa ya Koinange na Kimathi jijini
Nairobi.
“Mbali na kumbi za starehe, wameshaliangalia jengo
la Times Tower na Nyayo. Katika mipango yao, waliangalia muda ambao
watu wanakuwa wengi, usalama, kamera za CCTV na sehemu watakayosimama
wakati wa kutekeleza shambulizi,” inasema ripoti na kuongeza kuwa:
“Pia, waligundua kuwa majengo yataingilika kirahisi kwa kutumia kadi bandia zinazotengenezwa River Road, Nairobi.”
Magaidi walivyotoroka
Mwananchi
Taarifa za kiuchunguzi zimeeleza kuwa baadhi ya wanamgambo wa
kundi la Al-Shabaab waliotekeleza shambulizi kwenye jengo la Westgate,
walitoroka kupitia mfereji mkubwa wa maji machafu chini ya jengo hilo.
Mfereji huo unaanzia sehemu inayotumika kuegesha magari kwenye jengo hilo na kutokea katikati ya Jiji la Nairobi.
Kwa mujibu wa gazeti la Sunday Mirror la
Uingereza, sehemu ya kutokea kwenye mfereji huo imezungukwa na vichaka,
vinavyoaminika kutumiwa na magaidi kujificha.
Baada ya kukimbia kutoka kwenye jengo walilolishambulia, walitoroka kupitia kwenye mfereji huo.
Akizungumza ndani ya handaki hilo, mwandishi wa
Sunday Mirror, Russell Myers alisema: “mfereji unaanzia Westgate mahali
ambapo shambulizi lilitokea Jumamosi wiki iliyopita.”
“Magaidi huenda waliweza kupitia hapa bila
kuonekana na kukimbia kuelekea jumba la makumbusho la Nairobi, kisha
wakabadilisha nguo na kuingia kwenye magari,” alisema Myers.
Mbali na taarifa hizo, pia imekwisharipotiwa kuwa
baadhi ya magaidi waliteketea hadi majivu ndani ya jengo hilo, huku
Serikali ya Kenya ikisema sita kati yao waliuawa katika mapambano na
wengine kutoroka sambamba na mateka waliookolewa.
0 comments:
Post a Comment