Serikali jana ilitangaza kuyafungia magazeti ya Mwananchi na
Mtanzania kuanzia Septemba 27, 2013 kwa kile ilichoeleza kuwa ni
mwenendo wa magazeti hayo kuandika habari za uchochezi na uhasama.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Habari
(MAELEZO), Assah Mwambene ilisema gazeti la Mwananchi limefungiwa kwa
siku 14 na gazeti la Mtanzania limefungiwa kwa siku 90.
Magazeti hayo yamefungiwa kutokana na kuandika
habari na makala zilizoelezwa zina nia ya kusababisha wananchi wakose
imani kwa vyombo vya dola na kuhatarisha amani.
“Gazeti la MWANANCHI limefungiwa kutochapishwa kwa
siku kumi na nne (14) kuanzia 27 Septemba, 2013. Adhabu hii imetangazwa
kwa Tangazo la Serikali (Government Notice )Namba 333 la tarehe 27
septemba,2013,” yasema taarifa hiyo.
Kwa taarifa zaidi, tazama nakala ya tamko
kamili la serikali juu ya kufungiwa kwa magazeti ya Mwananchi na
Mtanzania hapo chini.
TAMKO KAMILI LA SERIKALI
Serikali imeyafungia kutochapishwa Magazeti ya
MWANANCHI na MTANZANIA kuanzia 27 Septemba, 2013 kutokana na mwenendo wa
magazeti hayo kuandika habari na makala za uchochezi na uhasama kwa nia
ya kusababisha wananchi wakose imani kwa vyombo vya dola hivyo
kuhatarisha amani na mshikamano ulipo nchini.
Gazeti la MWANANCHI limefungiwa kutochapishwa kwa
siku kumi na nne(14) kuanzia 27 Septemba, 2013.Adhabu hii imetangazwa
kwa Tangazo la Serikali (Government Notice )Namba 333 la tarehe 27
Septemba, 2013.
Gazeti la MWANANCHI limepewa adhabu hiyo kutokana
na hivi karibuni kuchapisha habari zenye mwelekeo wa uchochezi na
uvunjifu wa amani,mfano tarehe 17 Julai, 2013 katika toleo Namba 4774
ilichapisha habari isemayo “MISHAHARA MIPYA SERIKALINI 2013” kwa
kuchapisha waraka uliozuiliwa kwa matumizi ya vyombo vya habari waraka
huo ulikuwa wa Siri haukupaswa kuchapishwa Magazetini.
Aidha, katika toleo la Jumamosi, tarehe 17 Agosti,
2013 lilichapisha habari yenye kichwa kisemacho “WAISLAM WASALI CHINI
YA ULINZI MKALI” habari hiyo ilikolezwa na picha ya mbwa mkali mwenye
hasira. Habari na picha hiyo ilitoa tafsiri ya kuwa Jeshi la Polisi
lilipeleka Mbwa katika maeneo ya ibada ya waumini wa dini ya
kiislam. Jambo ambalo halikuwa la ukweli.
Jeshi la Polisi katika doria siku hiyo
halikupeleka mbwa katika maeneo ya Misikiti. Serikali na jeshi la Polisi
linaheshimu na kuzingatia maadili ya dini ya Kiislamu na kwa hiyo Jeshi
lake haliwezi kupitisha au kuingiza mbwa katika maeneo ya ibada.
Hivyo basi,kwa gazeti hili kuchapisha habari
iliyokolezwa na picha ya mbwa ni uchochezi wa kulichonganisha Jeshi la
Polisi na waumini wa dini ya kiislam mbwa ni najisi hapaswi kuingia
katika maeneo ya ibada.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Gazeti la MTANZANIA limefungiwa kutochapishwa kwa siku tisini
(90) kuanzia tarehe 27 Septemba, 2013 kwa kuchapisha habari zenye
uchochezi. Gazeti hili limeonywa mara nyingi lirekebishe mtindo wake wa
uandishi wa kichochezi na lizingatie maadili na Sheria na Kanuni za fani
ya Habari.
Pamoja na kuonywa gazeti hili halikuonyesha
kuzingatia maelekezo ya Msajili wa Magazeti, mfano ;katika toleo na 7262
la 20 Machi, 2013 liliandika habari yenye kichwa kisemacho “URAIS WA
DAMU”, tarehe 12 Juni, 2013, toleo Namba 7344 lilichapisha makala
isemayo “MAPINDUZI HAYAEPUKIKI”.
Aidha, siku ya Jumatano tarehe 18 Septemba, 2013
katika toleo Namba 73414 ukurasa wa mbele lilichapisha Kichwa cha habari
kisemacho “SERIKALI YANUKA DAMU” taarifa hiyo ilikolezwa na picha
zilizo unganishwa kwa ustadi mkubwa kwa kutumia kompyuta kutapakaza
rangi nyekundu mithili ya damu nyingi kumwagika.
Katika habari hiyo gazeti hilo limedai bila
uthibitisho kuwa Jeshi la Polisi linahusika na wahanga waliomizwa na
watu wasiojulikana kwa kumwagiwa tindikali na waliyovamiwa na kujeruhiwa
vibaya.
Vile vile gazeti hilo limeishtumu serikali kuwa goigoi katika kushughulikia matukio yenye sura ya kigaidi.
Kwa ujumla wake habari hiyo ni ya kichochezi ina
lengo la kuwafanya wananchi wavichukie vyombo vya ulinzi na usalama
wavione kuwa haviwasaidii.
Kutokana na makosa yalitajwa hapo juu serikali
imelifungia gazeti la Mtanzania kutochapishwa kwa muda wa siku tisini
(90) kwa Tangazo la Serikali Namba 332 (Government Notice No.332) la
tarehe 27 Septemba, 2013,.
Serikali inawataka wamiliki,wahariri na wanahabari
kwa ujumla kuwa makini, kuzingatia weledi, miiko na madili yataaluma
uandishi wa habari.
Serikali inawataka wamiliki na hasa wahariri
kuhakisha kuwa habari wanazoziandika na vipindi wanavyoviandaa
vinazingatia taaluma,kuweka mbele maslahi ya taifa letu kwa kuwa na
uzalendo wa hali ya juu.
Serikali inavionya vyombo vya habari vinavyoutumia
uhuru wa habari bila wajibu kuwa haitasita kuvichukulia hatua kali
ikiwemo ya kuvifungia. Serikali haitakubali kuona vyombo vya habari kuwa
chanzo cha uvunjifu wa amani nchini.
Imetolewa na:
MKURUGENZI IDARA YA HABARI
WIZARA YA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO
28 SEPTEMBA, 2013
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment