Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete.
KUNA njama za kisirisiri za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhujumu
mchakato wa Katiba Mpya kama njia ya kumkomoa Mwenyekiti wao, Rais
Jakaya Kikwete, ambaye baadhi yao wanadai anawazunguka katika suala
hilo, Tanzania Daima Jumapili limebaini.
Miongoni mwa wanaopanga hujuma hizo ni wabunge na baadhi ya mawaziri
waandamizi, ambao wanaona kuwa iwapo Katiba Mpya itapatikana kabla ya
mwaka 2015, hawatakuwa na matumaini ya kurejea madarakani.
Ingawa katika vikao na kauli rasmi CCM inaonekana inaunga mkono
mchakato huu, mwenendo na kauli za baadhi ya mofisa wake waandamizi
vinaonesha kuwa wana nia tofauti.
Wanasema walishindwa kuzuia mchakato huu mapema kwa kuwa Rais Kikwete
hakuwashirikisha, bali aliamua tu kuwakubalia wapinzani, hasa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kabla ya vikao vya CCM kushirikishwa,
na sasa wanasubiri kuzuia rasimu ya Katiba Mpya kwenye Bunge la Katiba
lenye wajumbe wengi wa CCM.
“Lengo letu hapa ni kumhujumu yeye na CHADEMA yake; maana inaonekana
ameamua kuwabeba kwa kuwapa jambo ambalo halikuwa sehemu ya ilani ya
uchaguzi ya CCM,” alisema mbunge mmoja wa CCM kwa sharti la kutotajwa
jina.
Duru za siasa nchini zinaeleza kuwa vurugu zilizotokea juzi bungeni na
kusababisha kambi nzima ya upinzani kususia mjadala wa muswada wa
marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya Katiba ni sehemu ya mkakati wa
CCM kwa kutumia kiti cha Spika wa Bunge, kuhakikisha Katiba Mpya ijayo,
ama inachelewa au inabeba masilahi yao.
Hii ni mara ya pili kwa wabunge wa CCM kuthubutu kumhujumu Rais Kikwete bungeni katika mchakato wa kuandaa Katiba Mpya.
Novemba mwaka jana, wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni, walitoka nje ya Ukumbi wa Bunge kwa madai ya kutoafikiana na
baadhi ya vipengele vya Muswada wa sheria ya mabadiliko ya Katiba.
Muswada huo ulipitishwa na wabunge wa CCM, lakini CHADEMA waligoma, na
wakaenda kuonana na Rais Kikwete, ambaye alilazimika kukieleza chama
chake juu ya umuhimu wa hoja za CHADEMA, wakarejesha muswada bungeni kwa
ajili ya marekebisho.
Hata hivyo ulipitishwa tena kwa wingi wa wabunge wa CCM na kuviacha
vipengele vingi ambavyo Rais Kikwete alikuwa amekubaliana na CHADEMA.
Baadhi ya Wana CCM wamediriki hata kuhoji kwanini Rais Kikwete
alikubaliana na mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuhusu
muundo wa serikali tatu katika Muungano, jambo ambalo wanasema rais na
Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Joseph Warioba, walikula njama dhidi ya
chama chao.
Katika vurugu za juzi ambazo ni mwendelezo wa hujuma za CCM dhidi ya
Kikwete, Naibu Spika na wabunge wa CCM walikataa kusikiliza hoja ya
upinzani kuwa muswada huo umewabagua Wazanzibari, kwani Kamati ya Bunge
haikuwasikiliza, na badala yake iliwasikiliza vigogo wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar, wakati suala linalojadiliwa ni la Muungano,
linalopaswa kujadiliwa na wananchi, si viongozi pekee.
Zogo hilo lilizuka baada ya Mbunge wa Mkoani, Ali Khamis Seif, kuomba
mwongozo wa Spika, akitaka hoja ya muswada wa marekebisho ya sheria ya
mabadiliko ya Katiba iahirishwe hadi hapo Wazanzibari
watakaposhirikishwa kama wenzao wa Tanzania Bara.
Naibu Spika Job Ndugai aligoma kuwasikiliza. Hata aliposimama Kiongozi
wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, kutoa hoja, Ndugai
alikataa kumpa fursa ya kuzungumza. Alimwamuru akae chini; na baada ya
kuona Mbowe amekataa kukaa chini, aliamuru askari wa Bunge wamwondoe.
Amri hiyo ya Ndugai ilizua tafrani baada ya wabunge wa CHADEMA
kumzunguka Mbowe wakizuia askari hao kumwondoa. Katika tafrani hiyo,
askari walimbeba mzobe mzobe Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, na
kumtoa nje, huku askari mmojawao akidaiwa kumpiga ngumi.
Hatimaye wabunge wote wa upinzani walitoka bungeni na kuwaacha CCM
peke yao, ambao hata hivyo, hawakujadili muswada, bali kila aliyepata
nafasi ya kuchangia muswada alitumia dakika zote 10 kutukana wapinzani.
Juzi wabunge hao walipitisha muswada huo bila kuujadili, na bila kuzingatia hoja ya ushirikishwaji wa Wazanzibari.
Hatima ya muswada huo iko mikononi mwa Kikwete ambaye anakabiliwa na
wakati mgumu kama ataamua kuusaini au kulitaka Bunge litimize kwanza
hitaji hilo lililoleta sokomoko inayoweza kudhuru mchakato mzima huko
mbeleni.
Kama Rais Kikwete atatumie busara kama za awali, upo uwezekano mkubwa
muswada huo ukarejeshwa bungeni ili ujadiliwe baada ya kutimiza vigezo.
Akizungumzia hali hii, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape
Nnauye, alisema msimamo wa CCM uko wazi, na kwamba hayo yanayojadiliwa
pembeni si ya chama.
Nape alisema CCM haiwezi kuruhusu wabunge au wanachama wake wamhujumu
rais wala Warioba. Alisisitiza kwamba chama chake kinaunga mkono kazi
ya Tume ya Marekebisho ya Katiba, ingawa kina msimamo katika maeneo
kadhaa unaokinzana na rasimu iliyotolewa na tume hiyo.
Alisema hata hivyo, msimamo wa chama unabaki kuwa wa chama, na kwamba
wananchi watakapoamua aina ya Katiba wanayotaka ndio msimamo utakaokuwa
wa mwisho.
Alipuuza kauli za wanaosema kuwa Katiba Mpya haikuwa sehemu ya ilani
ya uchaguzi ya CCM, akisema kuwa alichofanya Rais Kikwete ni kutazama
hali halisi na matakwa ya wakati.
Kwa sababu hiyo, alisema hata katika suala la Katiba Mpya,
kitakachoamua hatima na aina ya Katiba Mpya ni mahitaji ya wakati, si
ilani ya CCM au chama chochote.
Kauli ya Dk. Slaa
Naye Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alisema walichofanya
wabunge wa CCM kupitisha muswada huo juzi ni kielelezo kuwa Katiba
inayoandaliwa ni mali ya CCM, kwani inatengenezwa kwa maoni ya CCM.
Akizungumza na gazeti hili jana, Dk. Slaa alisema kuna upotoshaji
unaofanywa na viongozi wa Bunge kwa kushirikiana na serikali katika hoja
ya ushiriki wa Wazanzibari.
Dk. Slaa aliwashangaa wabunge wa CCM kwa kushindwa kujadili jambo zito
lililokuwa mbele yao na badala yake wakaishia kuwashambulia wabunge wa
CHADEMA na CUF.
Alisema anaamini kuwa hali hiyo ina msukumo kutoka nje ya Bunge, na
akatahadharisha juu ya mhimili mmoja kuingilia uamuzi wa muhimili
mwingine. Alisema hali hii itawafanya Watanzania wasipate Katiba
waliyoitarajia.
Alisema madhara ya hali hiyo yamejionesha katika sura mbili kwa
wabunge kuonesha ushabiki wa kichama zaidi badala ya kupigania masilahi
ya taifa.
“Lissu alisema Wazanzibari hawajashirikishwa, sasa hawa wanakuja na
barua ya serikali. Tunafahamu walipata maoni ya baadhi ya viongozi wa
serikali wanaotokana na CCM lakini hawajawafikia Wazanzibari wengi wa
kawaida,” alisema Dk. Slaa.
Kutokana na hali hiyo, alisema wananchi wameshaanza kuchanganyikiwa
juu ya dhamira ya serikali katika kuheshimu maoni ya wananchi kupitia
rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Jaji Joseph Warioba.
Akizungumzia udhalilishaji aliofanyiwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani
Bungeni, Freeman Mbowe, Dk. Slaa alisema Tanzania inafuata kanuni za
mabunge ya Jumuiya ya Madola ambayo nafasi ya kiongozi wa upinzani
bungeni ni sawa na waziri mkuu kwa upande wa serikali.
“Kwa maana hiyo, anaposimama Kiongozi wa Upinzani bungeni au Waziri
Mkuu lazima jicho la anayeongoza kiti cha Spika limtupie jicho kwa kuwa
ni lazima atakuwa na hoja ya kusikilizwa.
“Nilishasema katika hili Ndugai alikuwa hatumii akili yake alikuwa
anaongozwa kutoka nje ya Bunge na hili Watanzania wanapaswa watambue
mabavu yaliyotumika ni kielelezo cha wazi cha ukosefu wa demokrasia
nchini,” alisema Dk. Slaa.
Alisema waliopitisha rasimu hiyo wameua matumaini ya Watanzania na sasa ni jukumu la wananchi kuamua hatima ya nchi yao.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF),
Zanzibar Hamad Masoud, alisema hawana taarifa yoyote ya wananchi
kushirikishwa katika muswada huo wa mabadiliko ya sheria ya Katiba.
Alisema hali hiyo inadhihirisha nia mbaya ya serikali katika kutatua
matatizo ya wananchi kupitia Katiba huku akilaumu uamuzi wa kamati
kufanya mambo yake kwa siri.
Maige alishambulia Bunge
Wakati wabunge wa CCM wakiwashambulia wenzao wa kambi rasmi ya
upinzani waliosusia muswada huo, Mbunge wa Msalala, Ezekil Maige (CCM),
amelishambulia Bunge, hususan kiti cha Spika kwa kushindwa kutumia
busara kuepusha vurugu bungeni.
Katika taarifa yake aliyoitoa kupitia mtandao wa Kijamii wa Wanabidii,
Maige ambaye amepata kuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, alisema
kuwa alitazama kwa mshangao na kutoamini kuhusu kilichojiri bungeni
juzi.
Alisema kwa bahati mbaya hakuwepo Dodoma siku hiyo kwani alikuwa mjini Arusha kikazi, lakini hakuona
sababu kabisa ya kufikia hapo kwani hali hiyo ingeweza kuepushwa na kiti cha Spika.
“Ingewezekana kabisa kuahirisha muswada na kutoa nafasi kwa Kamati ya
Katiba na Sheria kwenda Zanzibar kupata maoni ya wenzetu wa huko.
“Najua kuna maelezo mazuri ya kushirikishwa kwa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar. Lakini kikanuni, Baada ya Muswada kusomwa mara ya kwanza,
unakuwa mikononi mwa Bunge na kamati ndiyo inayokusanya maoni si
serikali,” alisema Maige.
Maige ambaye anakuwa mbunge wa kwanza wa CCM kukosoa kiti cha Spika,
alisema kwa kuwa hakuna ushahidi wa ‘public hearing’ kufanyika Zanzibar
na kuwasikia Wazanzibari wa kawaida (nje ya serikali), basi kulikuwa na
hoja kabisa ya kurekebisha kasoro hiyo kwa kutoa nafasi kwa kamati
kwenda Zanzibar.
“Suala la Katiba ni kubwa hivyo ni vema zikafanyika jitihada za
kutosha kuhakikisha tunakwenda pamoja (na wenzetu hasa wenye mtazamo
tofauti na sisi) badala ya kutumia wingi wetu kwani mwisho wa safari
tukienda hivi wapo watakaodai Katiba Mpya si yao, hivyo kuikosesha
‘social legitimacy’,” alisema.
Kwa mujibu wa Maige, hatua ya Ndugai kutomsikiliza Kiongozi Mkuu wa
Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, nako kulitibua mambo bila
sababu.
“Mbowe angepewa nafasi ya kusikilizwa, hata kama hoja yake
isipokubaliwa ingekuwa nafuu sana na shari na aibu ya jana ingeepukika.
“Tumesameheana, lakini tujifunze na tujitahidi sana kwenda kwa maelewano,” alisema Maige katika taarifa hiyo.
0 comments:
Post a Comment