Rais Jakaya Kikwete
Waziri wa Katiba na Sheria, Mathis Chikawe amesema Rais Jakaya
Kikwete hana mpango wa kuongeza muda wa uongozi wake baada ya 2015 kama
baadhi ya wanasiasa wanavyodai.
Kadhalika, waziri huyo amesema hakuna sheria
inayomlazimisha Rais kusaini muswada wa sheria yoyote inayopitishwa na
Bunge na wala inayoweka muda maalumu wa kutekeleza wajibu huo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Chikawe alisema
kwa vyovyote vile Rais Kikwete hawezi kuongeza muda wa kuwapo kwake
madarakani kwa kuwa anaheshimu Katiba ya nchi iliyomuweka madarakani.
Waziri huyo alitoa kauli hiyo baada ya kutakiwa na
gazeti hili kuzungumzia madai ambayo yamekuwa yakirudiwa mara kwa mara
na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kwamba amenasa taarifa za
siri za kuwapo kwa mipango ya kuongeza muda wa Serikali ya sasa kukaa
madarakani.
“Ngoja nikwambie ndugu yangu, watu wanaongea tu,
kwanza Rais mwenyewe hana mpango huo, anasema kazi aliyonayo ni ngumu na
haoni sababu ya kuongeza muda,”alisema Chikawe na kuongeza:
“Mara zote ukizungumza naye anasema tuharakishe
mchakato wa Katiba na ikibidi tuingie katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kama
Katiba yetu inavyosema kwa kuwa kazi aliyofanya inatosha kabisa.”
Mapema mwezi Mei mwaka huu, Profesa Lipumba
alisema kutokana na wasiwasi kwamba mchakato wa Katiba Mpya
hautakamilika 2014, hivyo Uchaguzi Mkuu hautaweza kufanyika.
Kuhusu hatima ya Uchaguzi Mkuu iwapo Katiba Mpya
itaanzisha mfumo wa Serikali tatu, Chikawe alisema: “Wananchi wasiwe na
wasiwasi ikifika wakati huo kila kitu tutajua, lazima tutakuwa na sheria
ya mpito ambayo itaweka mambo sawa mpaka kutufikisha katika Uchaguzi
Mkuu.”
Rais kusaini muswada
Chikawe pia alizungumzia hatima ya Marekebisho ya
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Mpya ambapo alisema hakuna sheria
inayomlazimisha Rais kusaini miswada inayopitishwa na Bunge.
“Hakuna sheria inayomlazimisha Rais asaini wala
kumpa muda wa kusaini, mwenyewe anatumia busara na hekima tu katika
kusaini sheria,”alisisitiza Chikawe.
Kauli ya Chikawe imekuja siku chache baada ya
wenyeviti wa vyama vya CUF, NCCR -Mageuzi na Chadema kutoa tamko la
kumtaka Rais Kikwete asisaini muswada huo mpaka pale yatakapokuwapo
maridhiano ya wadau muhimu kuhusu muswada huo. Alisema kwa kutokusaini
muswada huo, kunaweza kukaleta tafsiri mbili; kwanza ni wale wanaoweza
kutafsiri kuwa ni dharau kwa wabunge waliopitisha muswada huo, kwamba
walichofanya si sahihi na hakina maana.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Hoja ya pili alisema kwa kutosaini pia kunaweza kuzidisha
msukumo kwa wanachama wa chama chake, lakini pia kutoka kwa wananchi
ambao wanasubiri kwa hamu utekelezaji wa sheria hiyo.
Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba wa 2013 ambao ulipitishwa na mkutano wa Bunge uliopita baada ya
mvutano mkali, umeendelea nje ya Bunge, huku kukiwa na madai kwamba
ulipitishwa ukiwa na marekebisho ambayo yalifanyika kinyume na maoni ya
wadau.
Madai mengine ni kwamba wabunge wa CCM waliongeza
baadhi ya mambo kupitia majedwali ya marekebisho, hivyo kutoa mwanya kwa
Serikali inayoongozwa na chama hicho kupitia kwa Rais kuwa na mamlaka
zaidi ya uteuzi wa wajumbe husika.
Septemba 6 mwaka huu, wabunge wa CCM walitumia
wingi wao kupitisha muswada huo katika mkutano wa Bunge ambao
ulisababisha tafrani kiasi cha Mbowe na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph
Mbilinyi kutolewa nje ya Bunge kwa amri ya Naibu Spika, Job Ndugai.
Katika tafrani hiyo, baadhi ya wabunge wa upinzani
walirushiana makonde na askari wa Bunge, huku wabunge wote wa upinzani,
isipokuwa Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema, wakisusia vikao vya
muswada huo.
Mwananchi
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment