MIMI ni mjumbe tu, ninachosema hapa sio maneno yangu, hivyo
kujenga chuki na mimi ni kutokuelewa maana iliyokusudiwa na wahenga,
ndio maana wakatunga methali kuwa “mjumbe hauawi”.
Hata kama niliadimika katika safu hii, nawashukuru wafuatiliaji
waliokuwa wanajaribu kunitafuta kwa simu kuuliza mjumbe nipo wapi ili
wanitume. Leo nimetoka mikoani, na nimetumwa kuuliza kwanini
Operesheni Kimbunga ni ya Kibaguzi?
Eti imewashughulikia weusi na kuwaacha weupe. Mjumbe sio mfuasi wa
ubaguzi wa rangi ila ametumwa na watanzania kuomba kuwa serikali itende
haki kwa wahamiaji haramu wa rangi zote, dini zote na mataifa yote.
Nimetumwa leo kuulizia suala la kinachoitwa Operesheni Kimbunga
kinachoendeshwa na Serikali ya Tanzania kama mkakati kabambe wa
kuwahamisha wahamiaji wanaoitwa haramu.
Wengi wa hawa wahamiaji
wanatoka katika nchi za nje na nyingi zikiwa jirani zetu.
Kinachofanyika ni kuwakamata watu hao na kuwarudisha makwao kwa nguvu,
ingawa wengine walishaona hapa ndipo kwao. Mjumbe nimetumwa niulize je
Wachina, Wahindi, Wasomali na Wazungu mbona hawaguswi na zoezi hili?.
Watanzania wanajiuliza ni kigezo gani kinatumika kuwabaini wanaopaswa
kuhesabiwa kama wahamiaji haramu. Watanzania wanaona kuwa wanaoandamwa
na zoezi hilo ni wale waafrika tu, weusi, wenye nywele fupi, tena
ikatajwa wanaokaa mikoa iliyo mipakani.
Mjumbe nimetumwa kushangaa akili za viongozi wa serikali kujihusisha
na mikoa iliyopo mipakani kana kwamba wanaokaa mikoa ya kati au
kwingine huko hakuna wahamiaji haramu. Vipi Dar es Salaam, Arusha,
Singida, Tanga, Zanzibar na maeneo mengine?
Suala la nchi kuwahakiki raia wake ni zuri sana, ni suala jema
linalopaswa kuungwa mkono na kila mzalendo hata mjumbe na mimi nimo,
ila utaratibu huu unaotumika hadi sasa ni kama vile kukumbuka shuka
asubuhi.
Mapesa yetu lukuki yametengwa kila mara kuzunguzia suala la
vitambulisho vya taifa lakini imekuwa danganya toto.
Miaka 50 ya Uhuru, taifa halijui raia wake kwa vitambulisho, na
halioni aibu kutokuwa na vitambulisho vya kitaifa. Tanzania kila kitu
kinawezekana kwa sababu ya udhaifu wa serikali.
Wahamiaji haramu ni
wengi, lakini serikali imeamua kujikita na wahamiaji weusi, hapa walio
wengi tayari wanajua kuwa zoezi hili lipo kama vile kukomoa Warundi,
Wanyarwanda, Wamalawi, Wazambia na Wanamuziki wengi wa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo ambao wamekuwa wakisaka mkate wao wa kila siku
katika bar mbalimbali nchini kwa kupiga muziki na kupongezwa kwa ujira
mdogo kwa kukata viuno.
Waganda na wa Kenya hawatajwi sana katika
operesheni hii.
Operesheni Kimbunga sasa imeripotiwa kubisha hodi Makanisani
kuwasakama wachungaji wa kigeni, wanaokusanya sadaka kwa mahubiri yao
kutegemeana na dhambi za Watanzania. Wao wamekuwa wakifanya zoezi la
kupatanisha Wanadamu na Mungu ingawa na wao sio raia wa Tanzania na
wapo nchini isivyo halali.
Pengine serikali ilikosa umakini katika hili, hivyo wachungaji hao
wakatumia mwanya wa kuwa viongozi wa dini kuhubiri licha ya kukosa sifa
ya uraia wa kuzaliwa au wa kuandikishwa, hivyo wamehesebiwa kuwa ni
Wahamiaji haramu. Kazi ya chungaji haifanywi sana na wazungu, kazi ya
uchungaji inafanywa na watu weusi, na humo kuna kundi la wahamiaji
haramu.
Operesheni Kimbunga imeugua ghafla, inasumbuliwa na Ubaguzi wa rangi,
hapa ndio Mjumbe nimeombwa nijikite katika kuuliza hili.
Operesheni
kimbunga imewaacha wahindi, wazungu, wasomali, na wachina kibao nchini.
Hivi Wachina wote wanaofanya shughuli za umachinga ni raia wa
Tanzania?
Viwanda vingi Dar es Salaam vinalalamikiwa na wafanyakazi wa
kitanzania kuteswa na kupewa mishahara midogo huku wafanyakazi wa
kihindi wanaofungiwa ndani ndio wanaolipwa kiwango cha juu kidogo. Je
kwanini hawachukuliwi hatua za uhamiaji haramu?
Katika sehemu mbalimbali Jijini kuna wachina wanafanya kazi za
ulinzi, kufungua na kufunga mageti, wapo wahindi na wazungu
wanaojihusisha hadi na biashara ya ukahaba, na madanguro yanajulikana
yalipo, serikali ilipaswa kutuambia hawa ni wahamiaji halali kwa kazi
ipi?
Tunapotajiwa Operesheni ya wahamiaji haramu, macho yamekimbilia
kwa wafugaji wakubwa wanaotoka Rwanda na Burundi tumewaacha wahamiaji
wengi wanaokaa nyumba za serikali, wakiwa wamepangishwa katika majumba
ya NHC, yameandikwa msajili wa Nyumba.
Hawa hawaonekani kuwa ni
hawamiaji haramu, je tunafanya zoezi hili kuwaondoa weusi au kuwaacha
weupe?
Je tunaondoa wenye nywele fupi na kuwaacha wenye nywele ndefu?
Wasomali wengi wanajifungia katika majumba yao hadi wengine miguu
inavimba kwa kukwepa kutoka nje, lakini huko operesheni kimbunga
haipelekwi. Kimbunga kinaogopa kuingia katika nyumba za watu hao.
Mjumbe nimetumwa niulize, operesheni hii ni ya haki au ya kukomoana?
0 comments:
Post a Comment