Olusegun Obasanjo
Mkuu wa ujumbe wa uangalizi kutoka Muungano wa Afrika
nchini Zimbabwe, Olusegun Obasanjo amesema uchaguzi mkuu wa hapo
Jumatano ulikuwa huru na haki ambapo matokeo ya awali yanaoyesha Rais Robert
Mugabe wa chama tawala cha Zanu PF akiongoza kwa kura nyingi.
Chama hicho tayari kimedai ushindi. Msemaji wa
chama hicho Rugare Gumbo alisema chama hicho kilitarajiwa kushinda kiasi
ya asilimia 70 ya kura hizo.
Lakini mpinzani wa Mugabe, Morgan
Tsvangirai, amesema uchaguzi huo ni wa uongo na kusema udanganyifu
uliofanyika una maana uchaguzi huo haukubaliki.
Waangalizi kutoka Umoja wa Afrika na jumuia ya
maendeleo kusini mwa Afrika wanatarajiwa kutoa tamko rasmi hii leo
kuhusu uchaguzi huo.
Bw. Obasanjo amesema kulikua na visa kadhaa
wakati wa shughuli ya kupiga kura. Hata hivyo amesema visa hivyo
haviwezi kutajwa kuwa na uzito wa kubatilisha au kufuta matokeo ya kura.
Msimamo wa Muungano wa Afrika unatofautiana na ule wa kundi la uangalizi la Zimbabwe Election Support Network.
Kundi hilo ambalo ndilo kubwa zaidi
linalochunguza kura ya Zimbabwe limekashifu uchaguzi mkuu na kusema
ulikuwa na dosari nyingi. Hii ni kwa sababu watu milioni moja walizuiwa
kupiga kura.
Huku upande wa Rais Mugabe ulitangaza kushinda
uchaguzi na Morgan Tsvangirai akipinga ni dhahiri kwamba Zimbabwe ingali
na mgawanyiko mkubwa wa kisiasa.
Cghanzo: BBCSwahili
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment