IMEBAINIKA kuwa baadhi ya maofisa wa polisi na makachero wao
wamekuwa wanatumia vibaya majina ya viongozi wakuu wa serikali na Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kama kisingizio cha kupika kesi za ugaidi dhidi ya
viongozi wakuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Katika tukio la hivi karibuni, makada wa CHADEMA waliokuwa rumande
wakikabiliwa na mashitaka ya ugaidi, ambayo hatimaye yalifutwa na
mahakama, wametoboa siri kuwa miongoni mwa majina yaliyotumiwa na baadhi
ya polisi na makachero waliowatesa ni ya Rais Jakaya Kikwete; na Waziri
wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, wiki hii, makada hao -
Evodius Justinian, Oscar Kaijage, Rajabu Kihawa, Seif Magesa na Henry
Kileo, wamesema pia kuwa njama hizo za polisi na makachero wao,
zililenga kuwalazimisha vijana hao wawahusishe viongozi wakuu wa CHADEMA
(hasa Mwenyekiti, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa) na
ugaidi na utesaji watu ambao umekuwa unaendelea.
Wengine ambao polisi walitaka watajwe ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika.
Hata hivyo, vijana hao wanasema waligoma kuwahusisha, hata baada ya kuteswa kikatili.
Makada hao wanadai kwamba mateso waliyopata yaliratibiwa na viongozi wa Jeshi la Polisi, Advocate Nyombi na afande Pasua.
Mmoja wa makada hao, Kihawa, aliyekamatwa na kupelekwa Kituo cha
Polisi Dodoma, anadai kuwa alipokuwa anahojiwa, alilazimishwa aseme kuwa
viongozi wa CHADEMA ndio wanahusika na utekaji na tindikali.
Akiendelea kusimulia mkasa huo, Kihawa alisema kuwa baada ya kauli
hiyo, aliingizwa katika chumba namba 114, ghorofa ya pili, chenye kamera
nyingi katika moja ya hoteli maarufu Mjini Dodoma (jina tunalihifadhi
kwa sasa) akavuliwa nguo zote, akakalishwa kwenye chupa ya soda kisha
akapigwa sana.
“Nilipoteza fahamu lakini nilipozinduka nilikuta nimevalishwa nguo, na
nimekalishwa kwenye kiti na kuwekewa chakula karibu,” anasema, na
kuongeza kuwa hakula chakula hicho, lakini alipotoka nje ya chumba
hicho, kwenye ukumbi wa hoteli, aliwakuta vijana waliofukuzwa CHADEMA,
Juliana Shonza na Mtela Mwampamba na Habib Mchange wakinywa na kula.
“Walinikejeli sana, wakasema wanashangilia ushindi,” alisema.
Kutoka pale nilichukuliwa na Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda,
akaniingiza chumbani akadai anampigia simu Waziri Simba, akamwambia,
“mama, huyu kijana ninaye hapa. Ungeongea naye ili akubali kulegeza
msimamo, au umpigie mwanao Jakaya anipigie, pengine atabadili msimamo
wake kama tulivyokuwa tumekubaliana awali.”
Kihawa anadai kuwa mtu huyo aliyedaiwa kuwa Waziri Simba alimjibu
Shibuda kuwa asingeweza kuzungumza yeye kwa kuwa alikuwa hajisikii vema,
ila kwa suala la kuongea na Rais Kikwete, atafutwe Katibu Mkuu wa chama
hicho, Abdulrahman Kinana au Naibu Katibu Mkuu Bara, Mwigulu Nchemba,
ili awaunganishe Shibuda na rais.
Kwa mujibu wa Kihawa, baada ya kupewa ushauri huo, Shibuda alijibu:
“Mwigulu ni mropokaji, hawezi kuingizwa katika mkakati huu; na Kinana ni
mgumu kuingilika katika suala hili.”
Anasema alisikia mazungumzo yao kwenye loud speaker ya simu ya
Shibuda, na baada ya kukata simu Shibuda alimwambia kuwa alikuwa
anazungumza na Simba, ambaye alidai ni ‘mama mdogo wa Kikwete.’
Kihawa anasema wakati anahojiwa hayo hapo hotelini, maofisa wa polisi walisimama kwa mbali wakimsubiri.
Wengine waliokuwapo wakishuhudia mahojiano hayo ni Meya wa Ilemela,
Henry Matata na aliyekuwa Diwani wa Igoma, Adam Chagulani. Matata na
Chagulani walishavuliwa uanachama na CHADEMA.
Wahusika walipohojiwa na Tanzania Daima jana, kila mmoja alikuwa na kauli yake kama ifuatavyo:
Tanzania Daima Jumapili: Afande Nyombi,
vijana waliokuwa wametuhumiwa kwa kesi ya ugaidi kule Tabora, wamekutaja
wewe kuwa ulishiriki kuwatesa ukiwalazimisha wawataje viongozi wakuu wa
CHADEMA kuwa walishiriki kutenda ugaidi na utekaji. Unatoa ufafanuzi
gani?
Advocate Nyombi: Mimi si msemaji wa Jeshi la Polisi, siwezi kusema chochote.
Tanzania Daima Jumapili: Msemaji atajuaje
kama mliwatesa watu wakati wa mahojiano? Mbona huku ni kumwonea msemaji
wa Jeshi la Polisi kusemea kila kitu hata mambo ambayo askari fulani
ametenda kwa utashi wake?
Advocate Nyombi: Nimekwambia mtafute, msemaji katika hayo yote. Mimi siwezi kuongelea suala hilo, nakutakia Idd Mubaraka njema.
Tanzania Daima Jumapili: Afande Pasua,
vijana waliotuhumiwa katika kesi ya ugaidi kule Tabora wamekutaja wewe
kuwa ulishiriki kuwatesa, ukiwalazimisha wataje viongozi wa CHADEMA kuwa
walishiriki kutenda ugaidi na utekaji. Unatoa ufafanuzi gani?
Afande Pasua: Kwani wewe uko wapi?
Tanzania Daima Jumapili: Nipo Dar es Salaam, hapa ofisini.
Afande Pasua: Njoo ofisini tuongee tuyaweke sawa unayouliza. Umesema unatoka gazeti gani?
Tanzania Daima Jumapili: Nimekwambia Tanzania Daima.
Afande Pasua: Mashtaka hayo kwanza yalikuwa
ya serikali, mimi sifanyi kazi ya kubahatisha, mpigie msemaji wa Jeshi
la Polisi mimi si msemaji. Alikata simu.
Henry Matata
Tanzania Daima Jumapili: Mstahiki Meya,
vijana waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya ugaidi wanadai walihojiwa mbele
yako Dodoma. Je, unafahamu nini kuhusu suala hili?
Matata: Kijana Rajab Kihawa ndio namfahamu.
Huyu alikuwa mfanyakazi wangu, ila tangu aache kufanya kazi hapa
sijaonana naye. Lakini mimi nina ugomvi na wafanyakazi wote wa gazeti
lenu na gazeti lenu. Nisingependa kuongea na nyie. Tangu nifukuzwe
CHADEMA gazeti lenu linaongeza chumvi habari zinazonihusu. Mimi si meya
kwa kura za CHADEMA. CHADEMA walinifukuza, CCM wakaona nafaa, wakanipa
kura nikawa meya.
Tanzania Daima Jumapili: Ulikutana na Rajab Dodoma hotelini?
Matata: Nimekwambia sitaki kuongea na gazeti lenu.
bi Mheshimiwa, vijana waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya ugaidi
wamekutaja kuwa ulikuwepo wakati wanahojiwa Dodoma. Je, una kauli gani
kwa yao hii?
Chagulani: Mimi nilikuwa Dodoma mwezi wa nne lakini nilikuwa Kondoa kwa ajili ya uhamisho wa mke wangu. Hayo unayonieleza siyajui.
Waziri Simba hakupokea simu, na alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu hakujibu lolote.
Msemaji wa jeshi la Polisi, Advera Senso, alipoulizwa kama jeshi ndilo
linawatuma polisi kutesa watu wakati linawahoji, alisema: “Mhalifu
asitafute huruma ya jamii kwa kuzushia jeshi kwa uhalifu alioutenda
yeye, na endapo ikibainika anasingizia uongo na hilo ni kosa pia, kwani
Jeshi la Polisi linafuata taratibu za sheria.”
Shibuda alipoulizwa jinsi alivyohusika katika sakata hilo alisema kuwa
kwa sasa hawezi kuzungumza chochote kwa kuwa alikuwa Agha Khan
Hospitali akihangaikia mgonjwa wake.
“Niacheni kwa sasa kwa kuwa nahitaji utulivu wa akili niweze
kushughulikia afya ya mgonjwa wangu. Nadhani hata kama ni wewe sijui
katika mazingira kama haya ungeweza kweli kuongea?” alisema.
Msemaji wa Ikulu, Salva Rweyemamu, alipopigiwa simu kuulizwa ikiwa
wanayo taarifa ya watu wanaotumia vibaya jina la rais katika matukio ya
kihalifu aliomba jambo lolote linalohusiana na kazi, lisubiri kwa kuwa
alikuwa katika mapumziko ya sikukuu.
“Ndugu yangu, unajua leo ni sikukuu na ni usiku, nitafute wakati
mwingine, maana siwezi kuzungumzia mambo ya watu wa CHADEMA muda huu.
Niache nipumzike kidogo halafu tuwasiliane siku ya kazi,” alisema.
0 comments:
Post a Comment