Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali (DPP), Eliazer Feleshi
SIKU chache baada ya Mahakama ya Kisutu kumwachia mtu aliyedaiwa
kumteka na kumtesa kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven
Ulimboka, serikali imemshukia daktari huyo na kudai ndiye chanzo cha
kukwama kwa dola kukamata watu waliomteka.
Jana Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali (DPP), Eliazer Feleshi,
alidai kuwa vyombo vya dola vimeshindwa hadi sasa kuwakamata waliohusika
katika shambulio hilo kutokana na Dk. Ulimboka kukwepa kutoa
ushirikiano kwa Jeshi la Polisi.
Feleshi ambaye jana aliambatana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini,
Said Mwema, katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam,
alidai lawama zinazosukumwa kwa Jeshi la Polisi kwa madai ya kushindwa
kuwakamata waliomtendea unyama daktari huyo hazina msingi, kwa kuwa
mhusika mwenyewe hajafika polisi, licha ya kuitwa mara nyingi kutoa
maelezo.
Alisema kama Dk. Ulimboka angetoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi
kungekuwa na mafanikio makubwa katika kuwasaka na hata kuwatia mbaroni
waliohusika katika unyama huo.
“Kila mara mmekuwa mkilaumu polisi wanashindwa kukamata wahalifu
lakini tutakamataje kama wenye ushahidi hawataki kutoa ushirikiano?
Kwa mfano mdogo tu ni ‘ishu’ (suala) ya Dk. Ulimboka, hadi leo hajatoa
taarifa lakini polisi wanaendelea kusakamwa na kutukanwa tu,” alisema.
Hata hivyo, wakati Feleshi akitoa kauli hiyo, Dk. Ulimboka katika
andiko lake alilolitoa mara tu baada ya kurejea nchini kutoka Afrika
Kusini alikopelekwa kwa ajili ya matibabu, alimtaja mtu anayeaminika
kuwa mfanyakazi wa Idara ya Usalama wa Taifa, Ramadhani Ighondu, kuwa
ndiye aliyemteka na kumtesa.
Ulimboka akimtumia Wakili Nyaronyo Kicheere alisema Ighondu na wenzake
ni mhusika mkuu katika unyama aliofanyiwa, kauli ambayo imekanushwa
mara kadhaa na serikali.
Mapema wiki hii, raia wa Kenya, Joshua Mulundi, aliyekuwa akikabiliwa
na tuhuma za kumteka na kumtesa Dk. Ulimboka aliachiwa na Mahakama ya
Kisutu baada ya DPP Feleshi kumfutia shitaka. Hata hivyo Mulundi
alikamatwa tena na sasa amefunguliwa mashitaka ya kutoa maelezo ya uongo
kwa polisi.
Wakati DPP akisema hayo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said
Mwema, jana aligoma kuzungumzia shinikizo la kumtaka ajiuzulu kutokana
na kukithiri kwa matukio ya raia kumwagiwa tindikali, badala yake
amewataka Watanzania kuwa na ushirikiano wa pamoja kukabiliana na
uhalifu huo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, (IGP)
Mwema alishindwa kukubali kujiuzulu wadhifa huo na badala yake alitoa
majibu ya jumla huku akiwataka Watanzania kubadilika na kuona suala la
kulinda raia na mali zao ni jukumu la kila mmoja na si kazi ya polisi
pekee.
Mkuu huyo alisema kuwa Watanzania lazima waelewe kuwa suala la ustawi
wa jamii linatokana na uwepo wa amani na utulivu. “Nchi hii si ya mtu
mmoja bali ni ya kila Mtanzania, inashangaza kuona asilimia 89 ya
Watanzania wanaona suala la kulinda raia ni la polisi, si kweli ni
lazima tubadilike,” alisema.
Alisema kuwa jukumu la utu lipo pale pale, hivyo kama taifa wana
dhamana ya kuhakikisha suala la matumizi mabaya ya tindikali na dawa za
kulevya linakomeshwa.
Mwema alisema kuwa wanalaani vitendo vibaya na vya kikatili vinavyofanywa na mtu mmoja mmoja ambavyo vinaleta hofu kwa jamii.
Alisema kuwa juhudi mbalimbali zinafanywa kuhakikisha vitendo hivyo
vinakomeshwa na hata kumalizwa kabisa. “Tumeamua kuja na mkakati wa
pamoja kwa kuwa sasa matukio ya umwagiaji tindikali umeshamiri na
hatuwezi kusubiri adhurike mtu mwingine, bali tusaidiane wote kwa pamoja
kukomesha haya,” alisema.
Alisema kuwa lengo la kutengenezwa kemikali hiyo haikuwa kutumika
vibaya au kumdhuru binadamu, bali ni muhimu kwa ajili ya vyombo vya
usafiri na maabara.
“Hata kisu ukiangalia kimetengenezwa kwa ajili ya mambo ya msingi, lakini kikitumika vibaya kinaweza kudhuru watu,” alisema.
Huku akionyesha hatua zilizochukuliwa na jeshi hilo bila kutaja jina,
alisema kuwa ofisa wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege mmoja amesimamishwa
kazi baada ya kudaiwa kuruhusu kupita kwa mabegi tisa ya dawa za kulevya
yaliyokamatwa Afrika Kusini mwezi uliopita.
Mwema alisema kuwa ni muhimu wananchi wakatoa taarifa mapema pindi
waonapo mwenendo mbaya wa matumizi ya tindikali hiyo, kwa kuwa ni
uhalifu mpya.
“Wananchi ndio waathirika wa kwanza, ni vema wakatoa taarifa mapema
ili hatua ziweze kuchukuliwa, maana vyombo vya dola pekee haviwezi
kuhimili jambo hilo,” alisema.
Matukio ya kumwagiwa tindikali kwa sasa yameshamiri nchini kufuatia
baadhi ya raia kupata ulemavu na wengine vifo, huku Julai 19, mwaka huu
mmiliki na mfanyabiashara maarufu wa maduka ya Home Shopping Centre,
Said Mohammed Saad, akivamiwa na kumwagiwa maji usoni yanayodhaniwa kuwa
ni tindikali.
Ikiwa ni takriban wiki mbili tangu kutokea kwa tukio hilo, juzi
wasichana wawili raia wa Uingereza waliofika visiwani Zanzibar kujitolea
kufundisha somo la Kiingereza walimwagiwa tindikali majira ya saa 1:15
usiku, Mtaa wa Shangani eneo la mji Mkongwe.
Hata hivyo wasichana hao walisafirishwa jana kwenda nchini Uingereza kwa ajili ya matibabu zaidi.
Mwaka 2007 Mkurugenzi wa Halihalisi Publishers, Said Kubenea,
alimwagiwa tindikali, hatua inayomlazimu kwenda nchini India mara kwa
mara kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake.
Mwaka 2011 wakati wa uchaguzi wa ubunge Jimbo la Igunga, Musa Tesha,
alimwagiwa tindikali, huku mkoani Arusha, wilayani Arumeru, Sheikh wa
wilaya hiyo, Said Juma Makamba, alijeruhiwa kwa kumwagiwa usoni
kimiminika kinachoaminika kuwa tindikali.
Wakati Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Suleiman Soraga, Novemba mwaka jana alimwagiwa tindikali.
Mkemia Mkuu wa Serikali
Katika kikao cha jana, Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel
Manyere, alipiga marufuku usafirishaji wa tindikali bila kibali na
kuagiza wahusika kutunza kumbukumbu kuonyesha ukali wa tindikali na
kutoa mrejesho wa kiasi walichouza kuanzia mwezi huu.
Alisema kuwa wasafirishaji wanapaswa kuwa na vibali kisheria ambavyo vimetolewa na ofisi yake.
Profesa Manyere alisema kuwa wauzaji wa rejareja ni lazima wawe
wamesajiliwa na wanapaswa kutoa taarifa za mauzo wanayofanya kila baada
ya miezi mitatu kuanzia sasa.
Alisema kuwa kuanzia sasa wamiliki wa vyombo vya usafiri hawaruhusiwi
kuchukua kemikali hiyo na kwenda nayo nyumbani badala yake wapeleke
magari yao. “Wale wa lita moja moja hawaruhusiwi kuuziwa bali itapaswa
kuuzwa kuanzia lita tano na kuendelea,” alisema.
0 comments:
Post a Comment