Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe
WAKATI Jeshi la Polisi mkoani Iringa likimkamata na kumshikilia kwa muda wa saa tano kisha kumwachia huru Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, pamoja na wabunge watatu, kiongozi huyo amesema kuwa endepo kesi hiyo itafikishwa mahakamani itakuwa ya 10 kufunguliwa na jeshi hilo.

Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni na vilevile mbunge wa Hai alikamatwa jana asubuhi pamoja na Mnadhimu Mkuu wa Kambi hiyo, Tundu Lissu (Singida Mashariki), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini) na Diwani wa Kata ya Mitimirefu, Frank Nyalusi, wakidaiwa kuzidisha muda wa mkutano.

Akizungumza na gazeti hili jana, muda mfupi baada ya kuachiwa alisema kuwa kesi hizo kamwe haziwezi kukiyumbisha chama hicho na badala yake zimewazidishia mori ya kufanya mageuzi ya kisiasa nchini ili kuondoa minyororo ya ukiukwaji wa haki.

Alisema kuwa amekuwa akikamatwa na kufunguliwa kesi za ajabuajabu na jeshi la polisi katika maeneo mbalimbali nchini wakati akifanya operesheni za kueneza chama mikoani.

Naye Lissu alizungumzia tukio hilo la kukamatwa kwao akisema limefanyika kisiasa kwa maagizo ya Chama cha Mapinduzi (CCM) baada ya kamanda wa polisi kuagizwa na wakuu wa mkoa na wilaya.

Lissu alifafanua kuwa kisheria hakuna kosa la jinai kama hilo kwa wao kupitisha muda wa mkutano na kwamba endapo kulikuwa na uvunjifu wa sheria walipaswa kukamatwa siku ileile walipotelemka jukwaani.

“Hapa hakuna kosa ni siasa tu za kuelekezwa na CCM halafu polisi wanafuata maelekezo tu.

“Hata maelezo waliyotuandikisha hawaonyeshi kifungu chochote cha sheria tulichovunja.

“Sheria ya vyama kutozidisha muda iko kwenye masuala ya mikutano ya uchaguzi, huu si mkutano wa uchaguzi,” alisema.

Akizungumzia kukamatwa kwa viongozi hao, kamanda wa polisi mkoa wa Iringa, Ramadhan Mungi, alisema kuwa walizidisha muda wa mkutano wa hadhara uliofanyika juzi katika viwanja vya Mwembetogwa kwa zaidi ya dakika 25.

“Kutokana na kitendo hicho tumewashikilia na kuwahoji na wakithibitika kutenda makosa hayo jeshi la polisi litawafikisha mahakamani kujibu tuhuma hizo,” alisema.

Alisema kitendo cha kuzidisha muda ni kinyume cha sheria na kwamba CHADEMA waliomba kibali cha kufanya mikutano mitatu mkoani hapa, ratiba yao ilielekeza kuwa wangefika wilaya Mufindi na kuanza mkutano saa 4:00 hadi 6:00 lakini wakafika saa 9:20 alasiri.

Mungi aliongeza kuwa hata mkutano wa wilayani Kilolo waliotakiwa kuhutubia saa 6:00 hadi 8:00 mchana wao walifika saa 4:45 na kuhutubia hadi saa 11:20.

Alisema kuwa Iringa mjini waliomba kuanza mkutano wao saa 8:00 mchana lakini wakaanza saa 9:00 alasiri kumaliza saa 12:25 jioni zikiwa ni dakika 25 zaidi ya muda, kitendo alichokiita ni uvunjwaji wa sheria za nchi.

Katika mkutano huo uliofanyika juzi katika viwanja vya Mwembetogwa, Mbowe kabla ya kuanza kuhutubia alilitaka radhi jeshi la polisi kwa kuchelewa kuanza kwa mkutano huo na mara baada ya kumaliza aliomba tena radhi.

“Nalishukuru sana jeshi la polisi kwa kuonyesha ustaarabu kwa kuwa niliwaomba radhi kwa kuchelewa kuanza na naomba dakika 10 nyingine niweze kumalizia jambo muhimu sana kuhusu mchakato huu wa rasimu ya Katiba,” alisema Mbowe na kuwataka wananchi waliohudhuria mkutano huo kuwapigia makofi polisi.

Awali akiwa wilayani Kilolo, Mbowe alisema kuwa suala la serikali tatu halikwepeki kwani ndilo litaweka utaratibu mzuri wa kunufaika na rasilimali za taifa kwa pande zote mbili za Zanzibar na Tanganyika.

Aliwataka wananchi kuacha tofauti zao za kisiasa ili kuweza kujadili mambo yaliyo muhumu katika rasimu ya katiba.

Mbowe aliongeza kuwa majadiliano ya rasimu ya katiba mpya hayapaswi kufanyika kwa kificho kwa kuwa ni mali ya Watanzania wote.

“Tunapozungumza suala la Katiba ya nchi yetu tuache dini na tofauti zetu pembeni ili tuweze kutengeneza Katiba nzuri. Wananchi wanapaswa kushirikishwa,” alisema.

Alisema katika taifa kumekuwa na mmomonyoko mkubwa wa maadili kwa wananchi ambao unasababishwa na baadhi ya watu kujigeuza kuwa miungu watu.

“Tunataka kila mmoja awe na haki ya kumiliki ardhi badala ya watu wachahe kuhodhi kila kitu. Tumeona kuna watu wachache wanataka kutengeneza Katiba inayowalinda wao. 

Tunapozungumzia utawala hatumzungumzi Kikwete bali tunataka kuweka utawala ambao kila mtu atakayeingia madarakani aweze kufuata taratibu hizo,” alisema.

Kwa Katiba tuliyo nayo leo tunaweza kuwa na Rais chizi akaipeleka nchi kichizi hivyo hivyo na itabidi tukubali tu.

Alisema Katiba mpya itaweza kuwabana wabunge watakaochaguliwa ili waweze kurudi kuwatumikia wananchi wao badala ya kuhamia na kuishi Dar es Salaam.

“Watawala wetu siku hizi wanafanya mambo ya siri. Wanasaini mikataba ya siri, wanauza madini na gesi kwa siri na kufanya nchi kama ni mali yao. Katiba mpya itayamaliza mambo ya siri na kila mmoja atajua kinachoendelea,” alisema.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top