Wakati Kamati Kuu ya CCM imeamua kuumaliza mgogoro wa madiwani
wake wa Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera kwa kutoa onyo kwa viongozi
wake, ndani ya Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM), hakujatulia kwani
kuna mpango wa kumwondoa Katibu Mkuu wake, Martin Shigela.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya vikao vya
Kamati Kuu zimesema kwamba viongozi kadhaa wa chama hicho akiwamo Mbunge
wa Bukoba Mjini, Balozi Khamisi Kagasheki na Meya wa Manispaa ya
Bukoba, Anatory Amani wameonywa kutokana na mgogoro wa muda mrefu katika
wilaya hiyo.
Wengine waliotakiwa kupewa karipio ni pamoja na
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera, Costancia Buhiye na Katibu wake,
Averin Mushi ambao walitarajiwa kuhojiwa jana usiku.
Habari kutoka ndani ya vikao hivyo vinavyofanyika
Mjini Dodoma zilisema hata ule uamuzi wa kuwazuia Amani na Kagasheki
kufanya siasa umeonekana unaweza kuleta athari kwao na kwa chama
chenyewe, hivyo kuamua kutoa onyo na madiwani waliokuwa wamefukuzwa
uanachama kuachwa kuendelea na nyadhifa zao.
Vyanzo hivyo vya habari vilieleza kuwa suala hilo lilikuwa tayari limeamuliwa, isipokuwa ilikuwa ni lazima wahusika waitwe kufahamishwa uamuzi dhidi yao badala ya kusikia kwenye vyombo vya habari.
Vyanzo hivyo vya habari vilieleza kuwa suala hilo lilikuwa tayari limeamuliwa, isipokuwa ilikuwa ni lazima wahusika waitwe kufahamishwa uamuzi dhidi yao badala ya kusikia kwenye vyombo vya habari.
Hata hivyo, hadi jana wakati tunakwenda mitamboni
ni viongozi wawili tu, waliokuwa wamehojiwa na Kamati Kuu ambao ni
Buhiye na Mushi kwa kuwa tayari walikuwapo Dodoma wakiwa ni wajumbe wa
Halmashauri Kuu.
Balozi Kagasheki na Amani licha ya kwamba walikuwa
wamewasili hapa, suala lao liliahirishwa kutangazwa kuwasubiri
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bukoba Mjini, Yussuf Ngaiza na Katibu wa CCM
Wilaya hiyo, Janeth Kayanda waliochelewa kufika mjini hapa baada ya
gari lao kuharibika.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
alisema uamuzi wa Kamati Kuu ungetolewa baada ya kumalizika kwa hatua ya
kuwahoji viongozi hao jana.
Mgogoro wa Manispaa hiyo unatokana na miradi
iliyopangwa na Meya Amani, ambayo inapingwa na baadhi ya madiwani wa CCM
wa Manispaa akiwamo Balozi Kagasheki, ambaye pia ni Waziri wa Maliasili
na Utalii.
Hali ya siasa mkoani humo ilichafuka zaidi baada
ya Halmashauri ya CCM ya Mkoa wa Kagera kuwafukuza madiwani wanane kwa
kosa la kumpinga Meya huyo na kupanga kumng’oa madarakani.
Madiwani hao ni Richard Gaspar (Miembeni), Murungi
Kichwabuta (Viti maalumu), Alexander Ngalinda ambaye pia ni Naibu Meya
(Buhembe) na Deusdedit Mutakyahwa (Nyanga), Robert Katunzi (Hamugembe),
Samwel Ruhangisa (Kitendaguro), Dauda Kalumuna (Ijuganyondo) na
Ngaiza(Kashai).
Hata hivyo, uamuzi huo wa kuwafukuzwa
ulisimamishwa na Sekretarieti ya CCM ambayo ilisema kuwa Kamati Kuu
ndiyo iliyokuwa na madaraka ya kutoa uamuzi wa mwisho dhidi yao na
kuwataka kuendelea na kazi wakisubiri hatima yao.
Katika hatua nyingine, kikao cha Halmashauri Kuu
ya Taifa ya CCM (NEC), ambacho kilikuwa kimalizike jana kimeongezewa
siku moja zaidi na kitafungwa rasmi leo.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Nape alisema hatua hiyo imechukuliwa ili kuwapa nafasi wajumbe wake kuipitia Rasimu ya Katiba.
UVCCM kwawaka moto
Baraza Kuu la UVCCM linakutana mjini Dodoma wiki hii pamoja na mambo mengine ni kupitisha jina la Katibu Mkuu mpya wa umoja huo.
Uteuzi huo unafanywa na Mwenyekiti wa Umoja wa
Vijana, Sadifa Juma Khamis, ambaye inaelezwa kuwa ameamua kumwondoa
Martine Shigela.
Habari za ndani kutoka katika umoja huo, zinasema
mbali na muda wa Shigela kumalizika, kumekuwapo na mgogoro ndani ya
UVCCM, baina yake na Sadifa tangu alipochaguliwa mwaka jana.
Habari hizo zinasema majina matatu yamependekezwa
kwa nafasi hiyo, akiwamo Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro, Sixtus Mapunda
anayepewa nafasi kubwa. Wengine wanaotajwa kupendekezwa na Mwenyekiti na
kusubiri baraka za Baraza Kuu ni wakuu wa Wilaya wawili, Elibariki
Kingu (Igunga) na Anthony Mtaka (Mvomero).
Kutokana na unyeti wa nafasi ya Katibu Mkuu wa
UVCCM, jana makundi ya umoja wa vijana yalikuwa yameanza kujikusanya
mjini hapa kujadili, huku baadhi yakichambua ama kwa kuafiki au kupinga
majina hayo.
Kuna taarifa kuwa uamuzi uliochukuliwa ni
mwendelezo wa mvutano wa makundi ya wagombea urais kupitia CCM katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Alipoulizwa jana kuhusu suala hilo, Sadifa alikataa kulizungumzia kwa undani akisema lisubiri vikao vimalizike.
“Kwanza vikao havijajadili jina la mtu anayefaa
kuwa katibu mkuu, siwezi kulizungumzia. Subiri vikao vikimalizika
nitakuwa tayari kuzungumza,” alisema Sadifa.
Mwananchi
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment