JESHI la Polisi na Idara ya Madini,
mkoani Kigoma, limemnasua kiaina ofisa usalama wa uwanja wa ndege,
Cleophace Lukindo, aliyedakwa na maofisa wenzake akivusha madini ya
dhahabu bila kuwa na vibali.
Tukio hilo lilitokea Agosti 22
uwanjani hapo wakati Lukindo akitaka kupita bila kukaguliwa tayari kwa
ajili ya kusafirisha madini hayo kwa ndege ya Shirika la Ndege Tanzania
kuelekea jijini Dar es Salaam ndipo wenzake wakamtilia mashaka na
kumkamata.
Madini hayo yalikuwa na uzito wa kilogramu tisa huku thamani yake ikielezwa kuwa takriban sh milioni 400.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, tukio hilo
limekuwa likifichwa na uongozi wa uwanja pamoja na jeshi la polisi
mkoani humo kwa kile kinachodaiwa kuwa ofisa huyo amekuwa akitoa vitisho
kwa wafanyakazi wenzake.
Katika hatua ya kushangaza gazeti hili
jana lilidokezwa kuwa madini hayo yamekabidhiwa na idara ya madini kwa
raia mmoja wa Jamhuri ya Kidemkrasia ya Congo (DRC) baada ya kutozwa
faini kutokana na kitendo hicho cha kutaka kuyavusha kinyemela.
Hata hivyo, taarifa hizo zimekuwa za kukinzana kati ya meneja uwanja, Tesha, na Kamanda wa Polisi, Frasser Kashai.
Wakati Tesha akidai waliyakabidhi
madini hayo polisi pamoja na mtuhumiwa, Kashai alisema kuwa Idara ya
Madini Kigoma ndiyo iliamua kuyarudisha madini hayo kwa mmiliki huyo
raia wa DRC.
"Unajua sisi hatushughuliki na madini,
tulipomkamata mtuhumiwa tulimhoji kwa kushirikiana na watu wa madini
lakini kwa taratibu zao walimtoza faini raia huyo kwa kutaka kuyavusha
bila kuwa na leseni kwa kumtumia ofisa huyo," alisema.
Kashai aliongeza kuwa Idara ya Madini
ilithibitisha kuwa raia huyo wa DRC anayo leseni ya umiliki wa madini
hayo lakini kosa lake hakuwa na vielelezo vya kuyasafirisha.
Alisema kwa sasa wao wanaendelea na
utaratibu wa kumchunguza ofisa huyo kwani wakati wa kukamatwa kwake
alifanya fujo ya kumjeruhi mwenzake na kuvunja kufuli.
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari,
ofisa huyo anadaiwa kuwekewa mtego na maofisa wenzake wawili baada ya
kubaini mpango wake huo wa kutaka kuvusha mzigo huo kwa kutumia leseni
ya mtu mwingine.
Taarifa zilidokeza kuwa ofisa huyo
licha ya kuwa na leseni hiyo isiyokuwa ya kwake, hakuwa na nyaraka
zingine za kuonyesha alikopata mzigo, anaupeleka wapi na kiasi chake.
Chanzo hicho kilidokeza kuwa baada ya
kufika eneo la ukaguzi, ofisa mwenzake, Yusuf Mpame, na askari polisi
Koplo Theophil walimtaka aonyeshe vibali na nyaraka hizo ili
wathibitishe kuwa mzigo huo ulikuwa unasafirishwa kihalali.
Hata hivyo, Lukindo baada ya kuona
wenzake wamemshtukia na kutaka kumkamata alitumia nguvu kumkaba ofisa
mwenzake Mpame ambaye alimnyonga shingo na kisha kung'ata lakini
akanusuriwa na Koplo Theophil na Jeremiah.
Chanzo: mjengwablog
0 comments:
Post a Comment